Ijumaa, 18 Oktoba 2013

WATUHUMIWA WA UCHOMAJI KANISA MBAGALA WAACHIWA



Na Happy Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaachia huru, Hamed Sekondo na wenzie wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha, kisha kulichoma moto Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Mbagala, baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibu.

Uvamizi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, ambaye alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ya jinai namba 294/2012 ilikuwa imekuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi wa ama kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Akisoma uamuzi wake, Lema alisema upande wa Jamhuri katika kuthibitisha kesi yao, ulileta mashahidi 14 na kwamba awali kesi hiyo wakati inafunguliwa mahakamani hapo mwaka jana, ilikuwa na jumla ya washtakiwa 10.
Alisema kuwa hivi karibuni mshtakawa mmoja, Ramadhan Mbulu, alifariki dunia na hivyo kufanya kesi hiyo kubakiwa na washtakiwa tisa ambao kwa kipindi chote walikuwa wakiishi gerezani kwa sababu kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha lililokuwa likiwakabili halina dhamana.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea, Yahya Njama.

“Baada ya kusikiliza na kuchambua ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na upande wa Jamhuri, mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu, hivyo inawaachilia huru kwa sababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yake,” alisema.
Lema aliongeza kuwa ushahidi wote walioutoa ni dhaifu na umeshindwa kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa wana kesi ya kujibu.
Upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Tumain

Kweka na Inspekta wa Polisi, Hamis Saidi.
Mwaka jana eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam lilikumbwa na vurugu kubwa zilizodaiwa kufanywa na baadhi ya waumini wa Kiislamu, ambao walikuwa wakipinga dini yao kudhalilishwa kwa kukojolewa kitabu cha Kurani, hatua iliyosababisha kuchoma moto makanisa.
www.mwakasegebibilia.blogspot.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni