Alhamisi, 24 Oktoba 2013

MOTO WA MILELE HAKUWEKEWA MWANADAMU



Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe

Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo: Moto wa Milele Hakuwekewa Mwanadamu

Mpendwa msomaji, ninatanguliza shukrani zangu za dhati kwako, kwa jinsi ulivyoamua kuisoma “note” hii. Nasema tena, asante sana. Sasa basi ninakusihi uisome “note” hii hadi mwisho, ili uchote baraka zote za Mungu zilizokusudiwa kwako.

Mpendwa msomaji, najua kabisa ungependa kwenda mbinguni, mahali pema peponi, na kukaa na Mungu milele, mara tu baada ya kuiaga dunia hii. Nia yako ni njema sana. Kila mmoja wetu anapenda kwenda mbinguni, hakuna anayependa kwenda katika moto wa milele. Mimi pia, ninapenda kwenda mbinguni, sipendi kabisa kwenda motoni. Hata Mungu anapenda sisi sote twende mbinguni aliko. Kuonyesha jinsi Mungu anavyopenda twende mbinguni, muda mfupi kabla ya Yesu Kristo kupaa kwenda mbinguni, alisema katika YOHANA 14:1-3, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”. Mungu hapendi kabisa yeyote kati yetu aende motoni. Moto wa milele, haukutengenezwa kwa ajili yetu wanadamu, bali ni kwa ajili ya Ibilisi na malaika zake. Biblia inasema katika MATHAYO 25:41, “………..Moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake”.

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Mungu anapenda sisi sote twende mbinguni aliko

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Baada ya kufahamu kwamba Mungu anapenda twende mbinguni, ni muhimu kufahamu pia kwamba Mungu ni mtakatifu, na mbinguni aliko, wako watakatifu tu. Yeyote mwenye dhambi, kamwe hawezi kumwona Mungu na kukaa naye milele, kwa sababu Neno la Mungu linasema katika WAEBRANIA 12:14, “Tafuteni kwa bidii…………huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”. Dhambi, hata iwe ni dhambi moja tu, inatosha kabisa kumtenganisha mwanadamu na Mungu milele na milele. Adamu na Hawa walipokuwa katika bustani ya Edeni, walifanya dhambi moja tu. Walikula matunda waliyokatazwa kuyala (MWANZO 3:9-13). Matokeo yake yalikuwa nini? Adamu na Hawa walifukuzwa kutoka katika bustani ya Edeni na kutenganishwa na Mungu. Mungu akaweka makerubi, yaani malaika wa vita, wenye upanga wa moto kuhakikisha hawarudi tena katika bustani ya Edeni. Ndivyo ilivyo, mpendwa msomaji, dhambi moja tu inatosha kutufanya tusiingie Paradiso. Neno “Paradiso”, kwa lugha ya asili, maana yake ni bustani iliyojaa raha. Kama Adamu na Hawa walivyotolewa katika bustani ya raha ya Edeni kwa sababu ya dhambi moja, sisi nasi hatuwezi kumwona Mungu mpaka tuwe na maisha yaliyo mbali kabisa na dhambi.

Mpendwa msomaji, hebu basi jaribu kujihoji sasa. Je, unaweza kusema kwamba hujafanya dhambi tangu kuzaliwa kwako? Je, kweli huna dhambi hata moja? Je, kweli hujasema uongo tangu kuzaliwa? Je, hujakuwa na hasira au chuki tangu kuzaliwa? Jibu ni dhahiri, umefanya dhambi moja au zaidi kwa namna moja au nyingine. Huenda umekuwa ukivuta sigara au bangi, au kubugia madawa ya kulevya; au kushiriki masengenyo, kunywa pombe, matusi, wizi, fitina, rushwa, ushirikina, kutoa mimba au kuua kwingineko, ugomvi, ulawiti, wivu, uzushi, uasherati, uzinzi, kucheza dansi n.k. Kwa hakika kila mwanadamu amefanya dhambi ya namna moja au nyingine tangu kuzaliwa kwake. Tukikana ukweli huu, Neno la Mungu linasema kwamba tutakuwa tunajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. Tunasoma katika 1 YOHANA 1:8, 10, “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukisema kwama hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”. Wote tumefanya dhambi kwa namna moja au nyingine wakati fulani katika maisha yetu. Mama anapomwambia mwanaye, “Nyamaza usilie, fisi huyo atakuja kukula”, wakati fisi huyo hayuko, huo ni uongo tosha wa kumfanya asimwone Mungu!

Sasa basi tufanyeje ili tuingie mbinguni na kukaa na Mungu milele? Hakuna jinsi, lazima tuwe mbali na dhambi kabisa katika maisha yetu hapa duniani, maana Neno la Mungu linasema kwamba,

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Sasa basi tufanyeje ili tuingie mbinguni?

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani. Tunasoma katika ZABURI 16:3, “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao”. Tukiishi maisha ya utakatifu hapa duniani, ndipo tunapoweza kuokoka kutupwa katika moto wa milele, au sivyo tutamlazimisha Mungu kututupa katika moto huo aliowekewa Ibilisi na malaika zake waliotenda dhambi tangu mwanzo. Sasa basi, swali linakuja, “Je, kweli inawezekana kuokoka tukiwa hapa duniani, na kuishi maisha yanayompendeza Mungu yaani kuishi maisha yaliyo mbali na dhambi?” Watu wengi wakiambiwa kujibu swali hili, upesi hujibu kwamba haiwezekani kuokoka tukiwa bado duniani. Huenda hata wewe mpendwa msomaji, jibu lako ni hilihili, kwamba haiwezekani kuokoka hapa duniani. Au siyo! Kama na wewe jibu lako ni hili, ni vema tuzidi kuelimishana jambo muhimu linalowachanganya watu wengi.

Kwa uwezo wa kibinadamu, ni kweli kabisa haiwezekani kuokoka hapa duniani, lakini kwa uwezo wa Mungu, jambo hili linawezekana kabisa. Biblia inasema katika MARKO 10:26-27, “Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu”. Watu wengi watakwenda motoni, kwa sababu wanafikiri tunatakiwa kuishi maisha yaliyo mbali na dhambi kwa kujitahidi kwa nguvu au uwezo wetu. Kwa nguvu zetu, kamwe hatuwezi kushinda dhambi. Mtu anaweza kusema hataki kunywa pombe tena, na akadhamiria kunywa chai au kahawa tu, lakini akikutana na rafiki yake akamwambia, “Twende zetu tukapate moja moto, moja baridi”, tayari kishawishi kinamwingia anajikuta anakunywa tena. Tunaweza kusema kwamba tuache uasherati na uzinzi kwa kuogopa Ukimwi, lakini wapi! Tunajikuta tunarudia tena kufanya yaleyale kama tusipopata uwezo wa Mungu wa kutuwezesha.

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . Kwa wanadamu haiwezekani, bali … yote yanawezekana kwa Mungu

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Kamwe, hatuwezi kuacha dhambi kwa nguvu zetu, ni mpaka tupate msaada wa Mungu, kwa Yesu Kristo. Si kwa uwezo wetu, wala kwa nguvu zetu bali kwa Roho wa Mungu asema Bwana wa Majeshi (ZEKARIA 4:6). Tunaweza mambo yote, katika Yeye atutiaye nguvu (WAFILIPI 4:13). Mtu anaposhindwa masomo darasani, humwendea yule mwenye uwezo kiakili ili amsaidie. Vivyo hivyo, ni muhimu kufahamu kwamba ni Yesu Kristo pekee aleyeishi duniani bila kufanya dhambi. Alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, lakini hakufanya dhambi kamwe (WAEBRANIA 4:14-15; YOHANA 8:46). Huyu tukimwendea kwa imani, Yeye ndiye pekee wa kutuwezesha kushinda dhambi. Tunaweza kushinda dhambi na kuishi maisha yanayompendeza Mungu pale tunapowezeshwa kwa uwezo wa Mungu. Biblia inasema katika WAKOLOSAI 1:10-11, “Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa;………..mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadri ya nguvu ya utukufu wake……..”

Sasa basi, tufanyeje ili tupate kuwezeshwa kushinda dhambi? Jibu, ni rahisi sana! Tutatakiwa kuungama dhambi zetu zote kwa kumaanisha kuziacha, kisha Yesu mwenyewe atatupa rehema ambayo ni uwezo wa kushinda dhambi. Jambo hili linafanyika kwa sala tu, kwa njia ya imani. Hatupaswi kuanza kufikiri kichwani, “Hivi kweli mimi nitaweza kuacha pombe, sigara au uasherati? Nisije nikawa najidanganya!” Kumbuka si kwa nguvu wala kwa uwezo wetu, bali kwa kuwezeshwa. Mara tu tunapotubu dhambi zetu, kwa kumaanisha kuziacha, rehema au uwezo wa Mungu hutushukia kutoka mbinguni, na ghafla utaona kiu ya pombe, sigara, uasherati, uzinzi, na kila namna ya dhambi; imehama kabisa, na unapenda tu kufanya mapenzi ya Mungu. Biblia inasema katika MITHALI 28:13,“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Baada tu ya kutubu dhambi zetu, Mungu hutusamehe mara moja, na wokovu unaambatana na msamaha!

Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”. Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja. Je, kweli utasamehewa? Jibu ni Ndiyo! Yesu mwenyewe anasema katikaYOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”. Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu. Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi? Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi. Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa? Najua uko tayari. Basi sema maneno haya, “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani. Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa. Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni. Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen”. Sasa ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen”. Tayari umeokoka. Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI!!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

UBARIKIWE NA BWANA YESU

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni