Ijumaa, 18 Oktoba 2013

IJUWE FURAHA YA MUNGU KWA WATENDAKAZI

Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
SOMO: FURAHA YA MUNGU KWA WATENDAKAZI

Tunajifunza somo la msingi katika mfululizo wa masomo ya Shule ya Uinjilisti, kwa kuligawa katika vipengele vinne:-

( 1 ). KAZI TULIYOPEWA WATU TULIOOKOLEWA

( 2 ). UINJILISTI NI NINI?

( 3 ). NANI ANAHUSIKA NA UINJILISTI?

( 4 ). FURAHA YA MUNGU KWA WATENDAKAZI

( 1 ). KAZI TULIOPEWA WATU TULIOOKOLEWA

Siku chache kabla ya Yesu Kristo kupaa mbinguni, alitukabidhi kazi ya muhimu sana ya kufanya. Kazi hiyo, ni kuenenda ulimwenguni mwote na kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, na kuwafanya mataifa au watu wasiookolewa, kuwa wanafunzi wa Yesu, na kuwafundisha kuyashika yote tuliyoamuriwa, baada ya wanafunzi hao kubatizwa kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Akasema kwamba, tukishiriki kufanya kazi hii, atakuwa pamoja nasi siku zote, hata ukamilifu wa dahari hata wakati atakaporudi tena ( MARKO 16:15; MATHAYO 28:19-20 ). Hili ni Agizo Kuu la Yesu Kristo kwetu. Wengi wetu tuliookolewa, hatumwoni Yesu Kristo akiwa pamoja nasi siku zote, kwa sababu hatushiriki kikamilifu kuifanya kazi aliyotupa Yesu katika Agizo Kuu hili. Kufanya kazi hii, ni kufanya kazi ya Uinjilisti.. Hili sasa, linatuleta katika kipengele cha pili cha somo letu.

( 2 ). UINJILISTI NI NINI?

Uinjilisti ni uvuvi wa watu ( MATHAYO 4:19 ). Kwa kuzaliwa na kutenda, watu wote ni wenye dhambi na hivyo, wamekwisha kuhukumiwa na kutupwa katika ziwa la moto. Uinjilisti, sasa, ni kuwapelekea watu hawa habari njema yaani Injili, kwa kuwahubiria kwamba, yeyote kati yao atakayemwamini Yesu, atasamehewa hukumu aliyokwisha kupata ya moto wa milele. Tukifanikiwa kuwafanya watu hawa watoke katika ziwa hilo la moto, kwa kufanya hivyo tumewavua kutoka ziwani,kama kuwavua samaki ( YOHANA 3:18, 36; UFUNUO 21:8; YUDA 1:22-23 ). Hata hivyo,Uinjilisti hauishii hapo. Kama vile mvuvi wa samaki asivyowaacha samaki wake aliowavua kwenye ufuo wa bahari au ziwa, mahali ambapo wataoza, basi huwachukua mara moja na kuwahifadhi vizuri; au kama mvuvi huyo wa samaki, asivyowaacha samaki wake kwenye ufuo wa ziwa na wakatembea hapo, mwisho wakarudi ziwani, vivyo hivyo, Uinjilisti au uvuvi wa watu, unakamilika kwa kuhakikisha wale waliokata shauri kumwamini Yesu na kuokolewa, wanaendelea Kanisani au nyumbani mwa Bwana,mahali ambapo watajifunza mafundisho ya mitume na kuukulia wokovu ( LUKA 14:23; YOHANA 15:16; MATENDO 2:41-42; 28:30-31; WAGALATIA 4:9-11, 19-20 ).

( 3 ). NANI ANAHUSIKA NA UINJILISTI?

Watu wengine, kwa kukosa mafundisho, wanafikiri kwamba kazi ya uinjilisti, inafanywa tu naWainjilisti, Wachungaji, Walimu au Mitume na Manabii waliowekwa na Mungu maalum kwa kazi hiyo na kupewa karama mbalimbali. Hii ni mbinu ya Shetani ya kufanya kazi hii ifanyike kwa viwango vya chini, ili yeye afurahi kuona wengi wanaangamia. Wainjilisti, Wachungaji, Walimu, au Mitumne na Manabii; ni Makomanda au viongozi wa Jeshi, na watu wengine waliookoka ni askari wa jeshi hili la Kristo Yesu ( 2 TIMOTHEO 2:3 ). Je, ni jeshi gani la nchi yoyote linaloweza kushinda ikiwa watakaopigana ni makomanda wa jeshi hilo tu na askari wengine hawashiriki kupigana? Jeshi la namna hiyo, ni lazima litashindwa vibaya. Askari wa kawaida, ndiyo wengi sana na katika nchi yetu, Tanzania, wanaitwa wapiganaji, maana bila wao, makomanda hawawezi kufanya kazi hiyo wenyewe. Kazi ya makomanda ni kuwa mstari wa mbele wa mapigano, na kuwaongoza maaskari wengine kuleta ushindi.Hivi ndivyo walivyofanya Kanisa la kwanza. Uinjilisti, haukuachwa kwa Mitume tu, pamoja na karama walizokuwa nazo; bali wote, wanaume na wanawake katika Kanisa la kwanza walishiriki katika kufanya Uinjilisti ( MATENDO 2:17-18 ).. Hata pale ambapo mitume walibaki Yerusalemu, wengine wote katika Kanisa, walitawanyika nakwenda kulihubiri Neno. Ndiyo maana, Kanisa la Kwanza, liliupindua ulimwengu wa nyakati zao ( MATENDO 8:1, 4 ). Mafundisho mengine ya Biblia, pia yanaoana na jambo hili. Kila mtu aliyeokoka, amefanywa kuwa mfalme na kuhani ( UFUNUO 5:9-10; UFUNUO 1:5-6 ).Utukufu wa Mfalme ni wingi wa watu wake, na uchache wa watu wake ni uharibifu wake ( MITHALI 14:28 ). Mtu ambaye hana hata mtu mmoja katika milki yake, hawezi kudai kwamba ni mfalme. Mfalme wa nani? Mfalme wa hewa? Vivyo hivyo, mtu aliyeokoka ambaye hana mtu yeyote katika milki yake aliyempata kwa uinjilisti, huyu ni mfalme wa hewa. Kazi ya Kuhani pia, ni kumpatanisha mtu aliyetenda dhambi, na Mungu wake, kwa kumfanya mtu yule kupata msamaha wa dhambi kutoka kwa Mungu (MAMBO YA WALAWI 6:1-2, 6-7 ). Kwa misingi hiyohiyo, kila mtu aliyeokoka, kwa kufanywa Kuhani; amepewa na Yesu Kristo, huduma ya upatanisho, kuwapatanisha wenye dhambi pamoja na Mungu wao ( 2 WAKORINTHO 5:17-18 ). Kama Kristo alivyotumwa na Baba, anatutuma sisi pia kufanya huduma ya upatanisho. Tusipofanya uinjilisti kwa wenye dhambi, tunawafungia katika dhambi. Tukiwa wavuvi wa watu, tunafanya watu hao waondolewe dhambi, maana watamwitaje Yesu bila kumsikia mtu akiwahubiri? ( YOHANA 20:21, 23; WARUMI 10:13-14 ). Tukiwafungia watu katika dhambi kwa kuacha kufanya uinjilisti, tunamuwekea Mungu moshi machoni pake na kumfanya atoe machozi, na vile vile tunampa siki anywe na kumfanya apate ganzi kwenye meno. Siyo vema kwetu kumfanyia hivyo Mungu ikiwa kweli tumeokolewa ( MITHALI 10:26 )

( 4 ). FURAHA YA MUNGU KWA WATENDAKAZI

Hakuna lolote tunaloweza kulifanya kwa Mungu na kumfurahisha, kama kuwa watenda kazi wanaofanya Uinjilisti, kwa kuwaleta watu kwa Yesu, na kuwalea katika uchanga wao kiroho, mpaka waukulie wokovu. Kila mtu aliyeokoka, angependa na kufurahi kuwa Mtendakazi, kama angejua ni kwa kiasi gani Mungu katika Utatu (Baba, Mwana na Roho Mtakatifu) anavyomfurahia mtendakazi mmoja anayefanya kazi ya uinjilisti. Ili tufahamu furaha ya Mungu kwa watendakazi ni muhimu tujifunze Mungu ni nani kwetu tuliookoka, na sisi ni akina kwake:-
1. Mungu Baba ni Mkulima (YOHANA 15:1)-Mkulima anapopita kwenye shamba liwe la migomba, mikahawa, michungwa, mipapai, minazi n., hufurahia sana kuona tawi linalozaa na kulishughulikia sana. Tawi lisilozaa, huliondoa na kulitupa motoni (YOHANA 15:2). Mkulima akiona tawi la migomba lililozaa mkungu na ndizi nzuri, atalitembelea tawi hilo wakati wote, na kuweka mti ili kulikinga tawi hilo na upepo n.k. Ndivyo alivyo Mungu kwa mtendakazi wake.
2. Mungu ni Bwana wa Majeshi (YAKOBO 5:4)-Amiri Jeshi Mkuu, huwafurahia mno askari wapiganaji hodari ambao wanaufanya ufalme wake kukua na kulindwa. Hawa humpa nguvu na sifa, hivyo huwatunuku medali maalum za kitaifa. Ndivyo alivyo Mungu kwa watendakazi wake.
3. Mungu ni mwenye mali - Mungu anafananishwa na mtu mwenye mali aliyesafiri ambaye amewaachia watumwa wake mali ili waifanyie biashara na kupata faida. Mtu mwenye mali wa namna hii akirudi, atamfurahia sana mtumwa yule aliyepeta faida kuliko yule aliyeificha tu, na hakuzalisha chochote (MATHAYO 25:14-30). Ndivyo alivyo Mungu kwa mtendakazi wake.
4. Yesu ni Mfanyabiashara mwenye vyombo vya uvuvi- Mfanyabiashara mwenye vyombo vingi vya uvuvi, huajiri wavuvi na kuwapa vyombo vya uvuvi. Wanaporudi kutoka katika uvuvi, humfurahia sana yule aliyeleta samaki wengi na kumpenda mno. Asiyeleta samaki, ana hatari ya kunyang’anywa chombo na asipewe tena. Ndivyo alivyo Yesu kwa mtendakazi wake aliye mvuvi wa watu (MATHAYO 4:19).
5. Yesu ni Mfugaji mwenye zizi la Kondoo –Baada ya kupotea Kondoo wengi katika zizi lake, anawatuma watu kuwatafuta. Atamfurahia mtendakazi atakayerudi na Kondoo wake wengi waliopotea (LIKA 15:3-7)
6. Mungu ni mume wetu (YEREMIA 3;14)- Mume humfurahia sana mke anayezaa sana na kuwalea vizuri wanae. Asipozaa, upendo kati yao huingia dosari, na ndoa huingia mashakani ikiwa ni mataifa. Ndivyo alivyo Mungu kwa mtendakazi wake.
7. Yesu ni Mpanzi wa Mbegu (MARKO 4:3)- Hakuna linalomfurahisha Mpanzi kama mbegu ile iliyotoa mazao mengi. Baada tu ya kupanda, mpanzi huanza kuangalia mbegu itakayoota na kutoa mazao mengi. Hiyo huipenda mno. Ndivyo alivyo Yesu kwa mtendakazi wake.
8. Yesu ni Mwalimu (YOHANA 13:13)- Mwalimu humfurahia sana mwanafunzi wake anayefanya kama yeye mwenyewe kutokana na jinsi alivyomfundisha. Ikiwa mwalimu anamfundisha mtu udereva lakini mtu yule ni mzito wa kufanya kama mwalimu wake, hapendezi kwake. Mtendakazi anayefanya Uinjilisti kama mwalimu wake Yesu, anamfurahisha mno.
9. Roho Mtakatifu ni Bwana wa mavuno – Anamfurahia sana mtu yule anayevuna roho za watu na kuzileta ghalani mwake, kuliko yule anayeacha mavuno yaozee shambani (MATHAYO 9:38; MATENDO 13:2; YOHANA 4:35-36).
10. Mungu ni Baba kwetu (MATHAYO 6:8-9) –Baba yeyote, hufurahi sana kuona watoto wa mtoto wake. Mungu pia hufurahi kuona watoto wa mtendakazi. Kwa sababu Mungu anamfurahia mtendakazi:-

( a ). Uwezo wa majibu ya maombi yake huongezeka (YOHANA 15:16)

( b ). Atang’aa kama nyota milel (DANIELI 12:3).

( c ). Watoto wa mtendakazi humuongezea Ushindi juu ya Shetani (ZABURI 127:4-5)

( d ). Watoto hao watakuwa ni taji ya kujionea fahari, furaha na utukufu wake wakati wa kuja kwa Yesu(1 WATHESALONIKE 2:19-20)

JE UNAPENDA KUINGIA MBINGUNI ?

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni