Alhamisi, 17 Oktoba 2013

SARA MVUNGI;SIJAWALAZIMISHA WATOTO WANGU KUOKOKA.





Makala na Imelda Mtema

Sara amebarikiwa kupata watoto wawili, Nicolas (22) na Neema (1O). Anaishi Kigogo, jijini Dar. Kigogo anaishi na Neema, Nicolas anaishi na babu yake Afrika Kusini.
Ili kujua jinsi gani anavyoishi na mwanaye huyo, ungana nami katika mahojiano niliyofanya naye:
Staa na Mwana: Mambo dada Sara habari za hapa nyumbani?
Sara: Salama tu karibu nyumbani.
Staa na Mwana: Kwanza kabisa wasomaji wa Staa na Mwana wangependa kufahamu kuna tofauti yoyote maisha wanayoishi watoto wako na watoto wengine ambao siyo wa staa?
Sara: Hapana, hakuna tofauti maisha ya wanangu ni ya kawaida sana. Mimi mwenyewe sipendi waishi maisha tofauti na watu wa kawaida.
Staa na Mwana: Kwa nini? Maana mastaa wengine hutofautisha watoto wao na watoto wa kawaida.
Sara: Kwangu mimi sioni kama ni malezi kwa sababu mimi mwenyewe nililelewa maisha ya kawaida kabisa.
Staa na Mwana: Nini ambacho unajivunia kutoka kwa watoto wako?
Sara: Kwa kweli ni watoto ambao wananipenda sana na kunithamini, wao ndiyo kila kitu maana hakuna faraja ambayo ninayo zaidi ya watoto wangu.
Staa na Mwana: Kwa nini iwe watato na si baba yao?
Sara: Hakuna, maishani ni mimi, watoto wangu na Mungu tu.
Staa na Mwana: Kwani huishi na baba yao?
Sara: Ndiyo, nipo peke yangu na wanangu. Baba yao ana maisha yake.
Staa na Mwana: Tuyaache hayo, wanao huwa nawaona kwenye nyimbo zako wanaimba, huwa wanapenda wenyewe au unawalazimisha?
Sara: Hapana ni wenyewe tu, hata kuingia kwenye wokovu waliingia wenyewe. Sijawalazimisha kuokoka tena kwenye kuimba, Hasa Neema anaimba sana.
Staa na Mwana: Sasa kama huyo Neema ni muimbaji vipi kuhusu masomo?
Sara: Anasoma vizuri tu kwa sababu kuimba siyo muda wote.
Staa na Mwana: Unafikiri wanao wamejifunza nini kutoka kwako?
Sara: Uvumilivu kwani watoto wangu wanajua mapito niliyopitia mimi mama yao, ni magumu. Wamejifunza mengi sana, zaidi ni kutokata tamaa.
Staa na Mwana: Ukiwa mbali na wanao, nini unahisi kimepungua?
Sara: Nawamisi sana husasan Neema, ninapokuwa sina amani huwa ananiimbia nyimbo za kunifanya niwe na furaha sasa ninapokuwa mbali, namkumbuka sana.
Staa na Mwana: Ni kitu gani umewaandalia wanao kwa maisha yao ya baadaye?
Sara: Nafanya kazi kwa nguvu zote ili wasome vizuri wawe na maisha yasiyokuwa na viulizo huko mbeleni.
Staa na Mwana: Haya asante Sara.
Sara: Karibu tena.
CHANZO ; GLOBAL PUBLISHER

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni