Jumatatu, 21 Oktoba 2013

JE, NIKWELI YESU ALIBADILI MAJI KUWA POMBE?

Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe

Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO: YESU ALIBADILI MAJI KUWA POMBE?

L


eo, tunaendelea tena kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu. Leo, tunajifunza YOHANA 2:1-11. Kuna mengi ya kujifunza katika mistari hii ingawa kichwa cha somo letu ni “YESU ALIBADILI MAJI KUWA POMBE? Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vinane:-

(1)RIPOTI YA UTENDAJI WA KAZI YA MUNGU KILA SIKU (Mst. 1);

(2)KUALIKWA YESU ARUSINI (Mst. 2);

(3)KUTINDIKA KWA DIVAI (Mst. 3);

(4)WAJIBU WA KUKUBALI KUKEMEWA (Mst. 4);

(5)SAA YA MIUJIZA (Mst. 4);

(6)LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI (Mst. 5-9);

(7)KUITENDA KAZI YA MUNGU BILA UKUU (Mst. 8-9);

(8)YESU ALIBADILI MAJI KUWA POMBE? (Mst. 9-11).



(1) RIPOTI YA UTENDAJI WA KAZI YA MUNGU KILA SIKU (Mst. 1)

Hapa tunajifunza utendaji wa kazi ya Mungu aliokuwa anaufanya Yesu. Kulikuwa na ripoti yake ya utendakazi KILA SIKU! “Na siku ya tatu palikuwa (Mst. 1), pamoja na “Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate“ (YOHANA 1:43); ni maneno yanayotufundisha kutoa ripoti ya utendaji wetu kila siku. Ni muhimu kila mmoja wetu kujiulizaKILA SIKU, “Je leo nimefanya nini katika utendaji wa kazi ya Mungu? Nimefanya nini leo kwa ajili ya Ufalme wa Mungu?“ Ikiwa majibu yetu ni kwamba hatukufanya lolote ila tumefanya mambo ya dunia hii tu yanayopita, au tumefanya mambo ya kujibariki tu na siyo kuwabariki wengine kiroho; tujue kwamba hatuishi kwa kufuata mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu hakuwa na siku hata moja ya kupoteza! Kila siku ilikuwa ni siku ya kumtendea kazi Mungu. Sisi nasi, ni wajibu wetu kuukomboa wakati. Hatuna muda mrefu wa kuishi. Tukipoteza siku moja na tukaiacha ipite bila kumtendea Mungu kazi, siku hiyo hairudi tena, tumepoteza kitu cha thamani kubwa (WAEFESO 5:15-16; WAKOLOSAI 4:5). Ripoti za watendakazi wengi zinasomeka “SIKUFANYA LOLOTE“ siku ya Jumatatu, Jumatano, Jumapili na siku nyinginezo, kwa visingizio mbalimbali. Huku siyo kumfuata Kristo Yesu!(2) KUALIKWA YESU ARUSINI (Mst. 2)

Ikiwa tunahitaji arusi au ndoa zetu zifanikiwe, hatuna budi kumwalika Yesu katika vipindi vyote kabla ya arusi na baada ya arusi. Tunaanza kumwalika Yesu katika maombi ya kutafuta mchumba, hatuchukui yeyote yule tu. Katika uchumba wetu pia, hatuna budi kumwalika Yesu kwa maombi ya nguvu kabla ya kuwaendea wazazi wa msichana, au siyo kunaweza kujitokeza vikwazo visivyo na msingi vya kutukosesha ruhusa ya wazazi. Ikiwa tutapuuza na kutochukua uzito wowote wa kumwalika Yesu katika uchumba wetu, hatuwezi kufanikiwa. Vivyo hivyo inatupasa kumwalika Yesu katika maandalizi ya arusi na pia baada ya arusi. Ndoa zetu zitajaa kila namna ya upendo ikiwa tutamwalika Yesu katika ndoa zetu KILA SIKU. Lolote gumu katika ndoa zetu, ni kwa sababu hatuchukui muda wa kutosha kumwalika Yesu katika ndoa zetu kwa maombi. Tunajifunza jambo jingine katika MST. 2. Yesu alialikwa pamoja na wanafunzi wake. Mtu akimtumikia Yesu na kumfuata pale alipo Yesu ndipo naye atakapokuwa (YOHANA 12:26; UFUNUO 3:21).
(3) KUTINDIKA KWA DIVAI (Mst. 3)

Divai katika Biblia, ni alama ya furaha, amani na mafanikio (ZABURI 104:15; MHUBIRI 10:19; YOELI 2:18-19; AMOSI 9:13-15). Katika Arusi hii, walifikiri wana divai ya kutosha, ghafla, wakaona imetindika (imepungua). Tunapokuwa katika vipindi vya mafanikio, amani na furaha, wengi wetu hujisahu na kuona kwamba vipindi hivyo havitakuwa na mwisho. Tajiri mmoja alifikiri namna hii, lakini ghafla akakuta furaha imetindika na akajikuta ametupwa motoni katika mateso (LUKA 16:19-31). Hakuna amani, mafanikio au furaha yoyote ya kudumu tunapokuwa hatuna Yesu katika maisha yetu bali tunadumu kutenda dhambi (ISAYA 59:8). Katika arusi hii furaha ilidumu kwa sababu walimwalika Yesu. Sisi nasi, inatupasa kumwalika Yesu mioyoni mwetu.

(4) WAJIBU WA KUKUBALI KUKEMEWA (Mst. 4)

Maneno Mama, tuna nini mimi nawe?, ni maneno yanayoonyesha kuudhiwa kwa Yesu. Katika lugha ya asili haitajwi Mama bali Mwanamke. Kiingereza KJV Bible vilevile ni WOMAN. Hivyo Yesu alisema “Mwanamke,(siyo mama!) tuna nini mimi nawe?”. Maneno “Tuna nini mimi nawe”, ni maneno ya ki-Biblia ya vita (WAAMUZI 11:12; 2 SAMWELI 16:9-10; MATHAYO 8:29). Kulikuwa na vita ya maneno kati ya Yesu na mamaye. Yesu hakufurahishwa na jambo alilolifanya mamaye la kumtaka aanze kufanya miujiza hadharani kabla ya saa yake haijawadia. AKAMKEMEA au AKAMKARIPIA. Hata hivyo, mamaye hakuwa na kinyongo, hasira, kuzira, kununa, kuudhika, kuchukia, kulipa kisasi au lolote la jinsi hiyo alipokemewa na Yesu. Wengi wetu hatuko kama Mariamu. Hatujui wajibu wetu wa kukubali kukemewa au kukaripiwa na viongozi wetu. Kukemewa na mwenye haki (Kiongozi wetu) ni mafuta kichwani petu, ni fadhili kwetu watoto wa Mungu. Asiyekubali au asiyefurahia kukemewa ni mtoto wa haramu, siyo mtoto wa Mungu (ZABURI 141:5; WAEBRANIA 12:5-11). Hata tukikemewa na Kiongozi wetu mbele ya wote Kanisani, ni mafuta na fadhili kwetu (1 TIMOTHEO 5:20; TITO 1:12-14). Tukiwekwa chini ya nidhamu na Kiongozi wetu, hatuna budi kuzidi kunyenyekea na kufanya yote bila kunung’unika.



(5) SAA YA MIUJIZA (Mst. 4)

Kuna saa maalum ya miujiza yetu. Tunapaswa kuomba na kung’ang’ania bila kukoma kama Mariamu. Hata hivyo maombi yetu lazima yaambatane na SUBIRA. Wengi hawako tayari kusubiri. Wakiona miujiza yao inachelewa basi wanaiacha imani yao ya kwanza. Jambo hili halimpendezi Mungu na hutukosesha baraka kuu. Subira upande wetu, ndiyo inayoonyesha kwamba Mungu ni Mkuu kwetu na mwamuzi watu; wala sisi siyo wakuu kwake Mungu na waamuzi kwake (YAKOBO 5:11). Vivyo hivyo kwetu wahubiri ni lazima tujue saa ya miujiza na siyo kufanya maombezi tu wakati wote. Miujiza mara nyingi hufuata baada ya mafundisho (LUKA 5:17). Tunajifunza jambo jingine. Mariamu alianza kumweleza Yesu akitaka muujiza divai ilipopunguka (ilipotindika). Yesu alifanya muujiza baada ya divai kwisha kabisa, ili wasidhani divai ya zamani ilichanganywa na maji. Saa ya miujiza iliwadia baada ya divai kwisha kabisa. Miujiza itangoja kwanza mategemeo yetu penginepo yaishe kabisa. Ikiwa bado tunategemea hirizi, au yeyote mwingine, miujiza yetu itachelewa.



(6) LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI (Mst. 5-9)

Mariamu alijua siri ya kupata miujiza, “Lolote atakalowaambia Yesu, fanyeni”. Wengi wanachelewa kupata miujiza yao, sababu hawako tayari kufanya yote wanayofundishwa katika Neno la Mungu; bali wanachagua ya kufanya. Hatuwezi kufanikiwa kuziona baraka za Mungu na kupata mafunuo makubwa na karama kuu za Roho Mtakatifu, ikiwa tunachagua ya kufanya. Ikiwa ni ubatizo wa maji tele, baada ya kuokoka, tusisite, bali tubatizwa, ikiwa ni kutupilia mbali mavazi ya kidunia, tusisite, bali tufanye hivyo, ikiwa ni kutoa fungu la kumi la mapato yetu, tufanye hivyo bila kusita, na yote mengineyo.



(7) KUITENDA KAZI YA MUNGU BILA UKUU (Mst. 8-9)

Yesu katika arusi hii, hakuwa MKUU WA MEZA. Hata hivyo pamoja na nafasi yake ya chini, alitumia karama zote alizokuwa nazo kuitenda kazi ya Mungu bila kinyongo. Hatupaswi kungoja ukuu katika Kanisa ili tufanye kazi ya Mungu bila kinyongo. Hatupaswi kungoja ukuu katika Kanisa ili tufanye kazi ya Mungu kwa bidii yote, wala hatupaswi kudhani kwamba ni Viongozi wa Zoni au wa Makanisa ya Nyumbani tu wanaopaswa kufanya kazi kwa bidii. Namna yoyote ya kusema “Mimi siyo Kiongozi wa Kanisa, kwa nini nihangaike?“ ni jambo lisilofuata mfano wa Yesu Kristo.



(8) YESU ALIBADILI MAJI KUWA POMBE? (Mst. 9-11)

Muujiza wa kubadili maji kuwa divai, ulikuwa muujiza mkubwa. Nzio moja ni karibu na galoni 9. Nzio tatu ni galoni 27. Mabalasi sita yalikuwa na ujazo wa nzio kama 18 au galoni 18 x 9 au 27 x 6 ambayo ni sawa na galoni 162 au debe 40½ (karibu mapipa 7). Hivyo divai aliyoitengeneza Yesu ni karibu mapipa 7! Divai hii haikuwa kileo au pombe maana aliudhihirisha utukufu wake. Ingekuwa amewapa watu kileo, ingekuwa aibu kwake badala ya utukufu (HABAKUKI 2:15-16). Ilikuwa ni divai mpya au divai tamu yaani juisi ya zabibu, tofauti na divai iliyochanganyika au kuchachuka ambayo ni pombe (MITHALI 9:4-6; 23:29-30; 3:9-10; YOELI 3:17-18). Hatupaswi kunywa mvinyo au divai iliyochanganyika ambayo ni kileo, hata katika ushirika unaoitwa mtakatifu (MITHALI 23:20; ISAYA 5:11; 65:11-12; YEREMIA 35:5-6). Mwanzo wa miujiza ya Musa hadharani ilikuwa pamoja na kubadili MAJIkuwa DAMU tofauti na Yesu (KUTOKA 7:20). Hii ndiyo tofauti ya torati na Injili. Torati inabadili furaha kuwa uchungu, vitisho, mauaji. Injili ya Yesu ni habari njema ya furaha kwa wabaya (YOHANA 1:17).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni