Jumatano, 30 Oktoba 2013

KWA TAARIFA YAKO : ALIYEIMBA "MFALME DAUDI" THE BIG NOVEMBER CRUSADE UNAJUA ALIKO?

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu


KWA TAARIFA YAKO hii leo mdau wetu ni kuhusiana na mwimbaji aliyewahi kuwika jijini Dar es salaam kutokana na uimbaji na uhamasishaji wake katika kumtukuza Mungu, huyu si mwingine bali ni Allen Kinsalla Lopez mwimbaji huyu alipachikwa jina la "Mfalme Daudi" kutokana na ghani yake ama rap yake ya "Mfalme Daudi, mfalme Daudi alicheza x2 aliicheza nguo zote zikaanguka, tuchezetuchezze kwa BWANA YESU tucheze, turukee turuke kwa BWANA YESU turukee……"rap hii ilipata umaarufu sana wakati wa mikutano ya "The Big November Crusade" iliyokuwa ikifanyika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam.

Mwimbaji huyu bwana Allen Kinsalla ambaye pia alikuwa ni mwimbaji wa kwaya ya Uinjilisti Sayuni Kinondoni Lutheran, yeye pamoja na kundi la kusifu na kuabudu ama stage band ilivyozoeleka katika mkutano huo walikuwa wakipenda sana kuimba pambio "Yale alotenda ndani yangu" na mapambio mengine ambayo yalikuwa yakiwakaribisha katika uwepo wa Mungu, mamia ya wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji vyake ambao walikuwa wakifika katika mkutano huo.




Kwasasa mwimbaji huyo mwenye asili ya Congo Kinshasa anaishi nchini Marekani pamoja na familia yake kwa maana ya mkewe na watoto wawili. Mwimbaji huyu alikuwa kipenzi cha wanafunzi wa Ushirika wa kikristo wa wanafunzi Tanzania(UKWATA) mkoa wa Dar es salaam na Pwani wakati ambao kwaya ya Sayuni ilikuwa ikialikwa kila mwaka kwenye makambi ya pasaka, matamasha, joint mass pamoja na sherehe mbalimbali za wanafunzi hao wanapohitimu masomo yao(Graduation za UKWATA).
Allen ambaye amelelewa na kundi la Sayuni, ambalo pia lilibahatika kubadili vionjo vya muziki wao kwakuimba mapambio na nyimbo za kilingala zilizokuwa zikiletwa na mwimbaji huyo, KWA TAARIFA YAKO kati ya mapambio yaliyowagusa wana UKWATA na watu wengine waliokuwa wakipata huduma za kwa ya ya Sayuni ni pamoja na "Bwana Yesu anakuja, Baba ninalia usiniache, Upendo wangu na Yesu, Nzambe malamu, Nkembo na yawe ama Tumsifu Yesu, Asante Bwana Yesu na nyinginezo. Kutokana na uimbaji wao mzuri imefanya hata kanda ya kwaya hiyo iitwayo "Simba wa Yuda" kutokea kupendwa sana ingawa kwasasa haipo madukani kutokana na ubora wake.
KWA TAARIFA YAKO kutokana na uimbaji mzuri wa kwaya hiyo pamoja na uhamasishaji wa Allen uliifanya kwaya hiyo kualikwa katika mkutano wa Taifa wa UKWATA uliofanyika shule ya sekondari Tosamaganga mjini Iringa ambako wanafunzi waliotoka na kwaya hiyo jijini Dar es salaam waliweza kuwaambukiza kwa haraka wanafunzi kutoka mikoa mingine uimbaji wa kwaya ya Sayuni hadi kufikia siku mbili kabla ya mkutano kuisha kwaya hiyo ilimaliza kanda zote ilizokuwa nazo hali ambayo haikutarajiwa kwa wanafunzi kununua kanda.

Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO hii leo kama ulikuwa unajiuliza alipo mwimbaji Allen Kinsalla Lopez a.k.a Mfalme Daudi, kwasasa yupo nchini Marekani. vinginevyo tukutane wiki ijayo katika kipengele hiki.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni