Alhamisi, 10 Oktoba 2013

Je, bahasha za zaka zina faida kuliko hasara au zina hasara kuliko faida kiroho?


Bahasha za Zaka Makanisani Zinatoka Wapi?





Je, ni huduma kwanza au ni roho kwanza?
Wapendwa nawasalimu katika jina la Bwana wetu, Yesu Kristo.


Katika safari yetu ya kiroho tunakutana na mitihani na changamoto mbalimbali ambazo, ama zinatujenga au, kwa bahati mbaya, wakati mwingine zinatubomoa.


Lakini tunapokutana na changamoto kutoka kwa watu wasiomjua Mungu, hilo halitusumbui sana, maana tunajua kuwa kwa hao hilo ni jambo la kawaida. Mtihani mkubwa unakuja pale tunapopambana nazo kutokea kwa wale wanaomjua Mungu, na hasa kama ni vongozi wetu wa kiroho.


Nimekuwa nikijiuliza juu ya suala moja ambalo, nafikiri, limekuwa likifanyika kimazoea zaidi kuliko kimaandiko. Hili ni suala la ulipaji wa zaka.

Kutoa zaka ni agizo la Mungu kwetu. Imeandikwa: Leteni zaka kamili (Malaki 3:10.
Hata hivyo, kanuni ya utoaji kibiblia, naamini ni ileile. Biblia inasema kwamba: Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. (2 Wakorintho 9:7).

Najua kuwa katika andiko hili, pale anaposema “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake,” hapo anaongelea sadaka. Suala la zaka halina kukusudia moyoni mwako, maana siwezi kusema, nimepata laki moja, lakini safari hii ngoja nitoa 5000/= tu. Kwa upande wa zaka ni lazima iwe kamili.

Lakini sehemu inayosema: “si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” hiyo inahusu zote, yaani sadaka na zaka.
Ni muhimu sana kutoa sadaka na zaka kwa kupenda; kutoa kwa sababu ninampenda na kumtii Mungu wangu si kwa sababu nimelazimishwa au ninataka kuonekana kwa mchungaji wangu kwamba na mimi ni mtoaji.
Kutoa kwa kupenda na bila huzuni kunatokana na sababu moja tu, nayo ni kuelewa kile anachokisema Mungu, pamoja na umuhimu au faida zake.

Lakini liko jambo moja linaloendelea katikati ya waumini kwenye nyumba za ibada. Jambo lenyewe ni hali ya kunung’unika na kulalamika. Kwa upande fulani, eneo la utoaji limekuwa ni kikwazo katika ukuaji wa kiroho wa watu wengi. Kweli kabisa watu wengi wamerudi nyuma na kuacha kabisa wokovu kwa sababu ya masuala ya utoaji.

Nikirudi kwenye suala la msingi katika somo hili juu ya zaka, ninajiuliza maswali yafuatayo:


(a) Ni wapi katika Biblia kunakosema kwamba waumini wanatakiwa kuwa na bahasha za zaka?
(b) Hivi ni kweli kwamba bahasha au risiti za zaka (kama wafundishavyo baadhi ya watumishi) ni muhimu pale ninapopata tatizo, kwamba eti ninaweza kuziinua na kumwambia Bwana, “Tazama, nimekuwa mwaminifu kutoa zaka. Naomba unisaidie katika hili na hili”? Je, Mungu anahitajikuona risiti? Kwani Yeye mwanadamu anayesahau?
(c) Je, si kweli kwamba inaelekea msisitizo uko kwenye kanisa (au mtumishi) kupata fedha kuliko muumini kupata kibali kwa Bwana?
(d) Je, kuwapo kwa bahasha hakuwi kikwazo zaidi kwa waumini (hasa wachanga) kuliko kuwa baraka?
(e) Kama watu wanarudi nyuma kwa sababu ya jambo ambalo hata Biblia hailiagizi, si bora kuliacha kwa ajili ya kuponya roho za watu hawa ambazo ni za thamani kuliko mapato ya kanisa?

Ni jambo linalotia uchungu sana kuona watu wakija kwenye wokovu kwa shauku kubwa ya kumjua Bwana Yesu na kupokea pumziko lakini baada ya siku chache wanavunjwa moyo na wanafukuzwa na hali zilizomo makanisani, ikiwa ni pamoja namna uendeshaji wa suala la utoaji zaka unavyofanyika.


Ninaweza nisiwe sahihi, lakini yafuatayo ndiyo ninayofikiri.


(a) Suala la bahasha za zaka, japo si lazima liwe kosa, lakini haliko kokote kwenye Biblia na si jambo la lazima.
(b) Suala la bahasha za zaka liko kwa ajili ya kutia utisho mioyoni mwa watu ili watoe hata kama mioyo yao haiko sawa mbele za Mungu na ndani yao kuna manung’uniko.
(c) Mtu anayetoa zaka kwa uaminifu na kwa moyo mkunjufu kwa kila pato analopata bila hata ya kuwa na bahasha ya zaka anafanya vema zaidi kuliko mwenye bahasha anayetoa zaka huku ananung’unika.
(d) Uaminifu wetu katika utoaji wa zaka unatakiwa kupata msukumo kutokana na sisi kumpenda na kumtii Bwana na si kwa sababu mchungaji ataangalia rekodi na kukuta mwezi huu sijatoa zaka.
(e) Naamini kuwa suala la zaka halina tofauti na utoaji wa sadaka zingine. Katika sadaka za kawaida huwa hatuna bahasha wala majina, lakini watu wanatoa.
(f) Nafikiri bahasha za zaka ni ishara ya kutomwamini Roho Mtakatifu kwamba atawagusa watu ili watoe sawasawa na mahitaji ya watumishi na kanisa.
Nimeshaona hata makanisa ambayo, muumini anatakiwa kubainisha mapema kipato chake anachotarajia kupata kwa mwezi. Baada ya kukibainisha, kila mwezi anatarajiwa kutoa kile kiasi. Asipokitoa, anaandikiwa deni.

Swali ni kuwa, je, zaka si inatokana na kile nilichopata? Kama sikupata nitatoa nini? Na kama nimepata pungufu, kwa nini nilazimike kutoa kiasi ambacho nilikibainisha?
Naamini kuwa roho za watu ni za thamani zaidi kuliko ongezeko la matoleo ya zaka. Tafadhali watumishi wa Mungu, msiwe sababu ya watu kuacha wokovu kwa sababu ya msisitizo wa zaka uliopita kiasi.

Kama mmeweza kuamini kwamba pale mnapowafundisha watu kuacha uongo, uzinzi, uchawi, n.k. watu hao wanabadilika bila ya ninyi kuwafuatilia mgongoni kila waendako, bila shaka hata suala la utoaji wa zaka linaweza kuenda sawasawa bila ya kulazimika kufuatilia jina la mtu mmojammoja kwamba ametoa au hajatoa.
Na hata pale mnapofundisha, ni vizuri sana kama mafundisho hayo yatakuwa kwa lengo la kumwonyesha mtu wajibu wake na sio kumsuta na kumlaumu na kumjaza ‘hofu mbaya’.
Ni wazi kuwa watu wasiotoa hawataisha. Wataendelea tu kuwapo. Lakini hapo ndipo ufundishaji na maombi vinapochukua nafasi yake, na bila shaka, Roho Mtakatifu atambadilisha kila mtu ‘kwa wakati wake.’

Hata dhambi zingine zote huwa hatuachi mara moja. Zingine zinaendelea kuwasumbua watu kwa muda mrefu, lakini kadiri mtu anavyodumu katika Neno, mafundisho na maombi, anafika wakati wa ushindi.

Inauma sana suala la zaka kuwa sababu ya watu kurudi nyuma; kurudi kwenye dini; kurudi duniani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni