
Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
MASOMO YA MAKANISA YA NYUMBANI
SOMO LA 10: IMENIPASA KUWAMO KATIKA NYUMBA YA BABA YANGU
NENO LA MSINGI:
LUKA 2:49:
“Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa IMENIPASA KUWAMO KATIKA NYUMBA YA BABA YANGU?”
I
shara mojawapo kubwa itakayoonekana kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili na kufanyika mtoto wa Mungu, ni shauku ya kuzijua njia za Mungu, kufurahi kumkaribia Mungu na kumtafuta Mungu kila siku.
ISAYA 58:2:
“Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki; wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu.”
Mtoto wa Mungu atapenda kujisomea Biblia, na kufanya maombi kila mara anapopata nafasi nyumbani mwake. Maisha yetu ya kiroho nyumbani, ni lazima yaambatane na kujisomea Biblia na kuyatafakari yaliyomo, pamoja na kufanya maombi mara kwa mara. Hata hivyo, haitoshi tu kujisomea Biblia na kufanya maombi nyumbani na kudhani kwamba hakuna umuhimu wowote wa kwenda Kanisani. Kwenda Kanisani, ni agizo la Mungu kwa kila mtu aliyeokoka. Ni lazima tukutane pamoja na wenzetu katika kusanyiko mahali alipopachagua Mungu. NI AMRI YA MUNGU kwa kila mtu aliyeokoka kwenda Kanisani na kukusanyika pamoja na wenzake. ANGALIA MAANDIKO:
KUMBUKUMBU LA TORATI 12:5
“Lakini mahali atakapopachagua BWANA, Mungu wenu,………………..apaweke jina lake, maana ni makao yake, ELEKEZENI NYUSO ZENU HAPO, NAWE WENDE HUKO.” Maneno haya “Nawe wende huko”, katika Biblia ya Kiingereza ya tafsiri inayoitwa “New International Version”, yanasomeka “TO THAT PLACE YOU MUST GO.” Tungeweza kutafsiri “MAHALI HAPO, NI LAZIMA UENDE.”
Unaona! Mungu anasema ni lazima twende Kanisani, katika Nyumba ya Bwana. Angalia zaidi Maandiko:
WAEBRANIA 10:25
“Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine……. na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”
Yesu Kristo mwenyewe alionyesha wazi jinsi ilivyo lazima kwa kila mkristo kuwamo nyumbani mwa BWANA au Kanisani. Yusufu na Mariamu walipomtafuta kwa huzuni Yesu Kristo baada ya kumkosa kwa siku tatu, walipomwona; Yesu aliwaambia:
LUKA 2:49:
“Akawaambia, kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa IMENIPASA (ni lazima kwangu) KUWAMO KATIKA NYUMBA YA BABA YANGU?”
Ikiwa Yesu Kristo kwake ilikuwa ni lazima kwenda Kanisani, basi ni zaidi sana kwa kila mtu anayesema Yesu Kristo anakaa ndani yake. Biblia inasema kwamba yeyote anayesema Yesu Kristo anakaa ndani yake, imempasa kuenenda VILEVILE kama Yeye (Yesu) alivyoenenda alipokuwa duniani [1 YOHANA 2:6]. Ikiwa wewe umeokolewa na ni mkristo unayefuata chapa zake Yesu, basi kwako itakuwa niLAZIMA kwenda Kanisani na utafurahia kufanya hivyo. Daudi alifurahi mno alipoambiwa aende nyumbani mwa BWANA au Kanisani [SOMA ZABURI 122:1].
Ukitaka kufanikiwa kama Daudi, inakubidi uwe na furaha kumkaribia Mungu kwa kwenda Kanisani. Watakatifu wa zamani walikuwa na shauku ya ajabu ya kwenda Kanisani na waliona Nyumba ya BWANA ikipendeza mno kwao. Kwao siku moja Kanisani ilikuwa ni bora kuliko sikuelfu (zaidi kidogo ya miaka mitatu) katika shughuli za dunia au hema za uovu [SOMA ZABURI 84:1-2, 10].
Mtu anaonyesha jinsi ambavyo amekomaa kiroho kwa jinsi ambavyo ana shauku kubwa ya kwenda Kanisani. Ikiwa mtu anajiona kuwa ni Nabii na hana haja ya kwenda Kanisani, huyo ni nabii wa uongo. Nabii wa kweli Ana binti Fanueli, kila siku alikuwa Kanisani [SOMA LUKA 2:36-37].
Ikiwa mtu anajiona amekua sana kiroho, na kufikia kiwango cha mitume kumi na wawili wa Yesu; na kujiona kuwa hana haja ya kwenda Kanisani, basi huyo ni mtume wa uongo. Mitume wa Yesu kila siku walikuwa Kanisani [SOMA LUKA 24:53]. Ikiwa mtu anajiona kuwa ana karama zilizo kuu kama Petro na Yohana, na kuona kuwa hana haja ya kwenda Kanisani; mtu huyu hawajui Petro na Yohana. Watu hao walikuwa wanakwenda Kanisani na walitunza mno hata muda uliopangwa wa kukusanyika Kanisani. [SOMA MATENDO 3:1].
Mtume Paulo naye alijua mno ulazima wa kwenda kusali Kanisani na alimwona Yesu kwa njia ya kipekee akiwa yuko Kanisani akisali [SOMA MATENDO 22:17].
Watu waliookoka katika Kanisa la Kwanza walijua mno ulazima wa kuwa Kanisani kila siku.
MATENDO 2:46
“Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu ………………”.
Haikuwa Jumapili tu, kama watu wengine wanavyofanya leo. Haikuwa tu siku fulani ya sikukuu! SIKU ZOTE! Mtu aliyeokolewa, anaonyesha tofauti iliyopo kati yake na wasiomcha Mungu kwa jinsi ambavyo anakwenda Kanisani zaidi ya siku moja kwa wiki. Wako wakristo wa jina (ambao hawajaokolewa) wanaokwenda kila Jumapili kanisani. Ni lazima kuwepo tofauti. Kila siku ya ibada Kanisani inatubidi kwenda ili kukusanyika pamoja na wenzetu. Ni lazima kujihadhari na masumbufu ya dunia (hema ya uovu) ambayo yanatufanya twende Kanisani mara moja kwa wiki au mara moja kwa mwezi. Ni lazima tuombe kufunguliwa katika hali hiyo ili kila mmoja ahudhurie siku zote za Ibada Kanisani.
SABABU SITA ZA ULAZIMA WA KUKUSANYIKA PAMOJA KANISANI
1. MUNGU KAMA BABA YETU, HUSEMA NASI KIPEKEE TUNAPOKUSANYIKA PAMOJA KAMAWATOTO WAKE
Baba anaweza kusema na mtoto mmoja mmoja juu ya mambo kadha. Hata hivyo, mambo ya undani mno yanayohusu watoto wake, Baba hupenda kuyazungumza baada ya kuwakusanya kwanza watoto wake ili wasikie wote. Angalia mfano huu katika Biblia:
MWANZO 49:1-2:
“Yakobo akawaita wanawe, akasema, KUSANYIKENI, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni msikie, enyi wana wa Yakobo. Msikilizeni Israeli, BABA YENU.”
Watu tuliookoka, ni wana wa Israeli wa kizazi hiki. Baba yetu aliye mbinguni hupenda tukusanyike wote pamoja, ili azungumze nasi kipekee. Wakati wote hupenda tukusanywe kwanza ili atueleze mambo muhimu tunayopaswa kuyafahamu. Angalia anavyosema katika:
ZABURI 50:5:
“Nikusanyieni wacha Mungu wangu waliofanya agano nami kwa dhabihu.”
Mungu husema nasi mmoja mmoja tunaposoma Neno lake na kuomba, kila mtu akiwa nyumbani kwake. Hata hivyo, tunapokusanyika pamoja, Mungu husema nasi kwa namna ya kipekee.
1. MUNGU HUJITUKUZA KIPEKEE KATIKA KUSANYIKO
Watoto wake Mungu wanapokusanyika pamoja kwa jina lake, yaani kutokana na agizo lake; na kumsifu Mungu na kumwabudu Kanisani, Mungu hujitukuza kipekee kati yao. Utukufu wa kipekee wa Mungu hudhihirishwa, kusanyiko la watu wa Mungu linapojihudhurisha mbele za Mungu. Angalia mifano katika:[1WAFALME 8:10-11; 2 NYAKATI 5:13; KUMBUKUMBU LA TORATI 4:10-12].
2. MUNGU HUTUFUNDISHA KIPEKEE KANISANI
Yesu Kristo alikuwa akifundisha katika hekalu au Kanisani kila siku [YOHANA 8:2; MARKO 14:49]. Mafundisho ya Yesu hekaluni yalikuwa yamejaa mafunuo ya kipekee katika Neno la Mungu. Baada ya Yesu kuondoka kwetu, Roho Mtakatifu ameweka WENGINE (sio sote) kuwa WAALIMU ili kuwakamilisha watakatifu [WAEFESO 4:11-15; 1 WAKORINTHO 12:28-29]. Yesu alituonyesha mfano wa kwenda Kanisani na kuwasikiliza waalimu wakilitafsiri Neno la Mungu na kutufundisha, na kisha kuwauliza maswali:
LUKA 2:46:
“Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.”
Sisi nasi inatupasa kumfuata Yesu kielelezo chetu. Pamoja na kujifunza nyumbani kwetu, inatubidi tukusanyike pamoja Kanisani ili tuwasikilize waalimu waliowekwa na Roho Mtakatifu na kuwauliza maswali.
3. MUNGU HUZIFUNUA DHAMBI TUNAZOZITENDA BILA KUJUA,TUNAPOKUWA NYUMBANI MWAKE
Dhambi ni nini?
(a) Dhambi ni kufanya yasiyotupasa kuyafanya;
(b) Dhambi ni kutokufanya yanayotupasa kuyafanya.
Pasipo kufahamu na tena bila kukusudia, unaweza ukatenda dhambi bila kujua kuwa ni dhambi. Mbele za Mungu ukifanya dhambi pasipo kujua kuwa ni dhambi bado unakuwa na hatia:
MAMBO YA WALAWI 5:17:
“Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, AJAPOKUWA HAKUYAJUA, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake.”
Kwa sababu hiyo, Mungu mwenyewe anatushauri kwamba tutunze miguu yetu na kuitumia vema kutupeleka nyumbani kwa Mungu (Kanisani); ili tusikie yale yanayotupasa kuyafanya, na pia yale yasiyotupasa kuyafanya; ili tusijikute tunafanya kama wafanyavyo wapumbavu.
MHUBIRI 5:1:
“Jitunzeni mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; maana ni heri kukaribia ili usikie, kuliko kutoa kafara ya wapumbavu; ambao hawajui kuwa wafanya mabaya.”
Kwa kuwa Mungu anatupenda, hutufunulia waziwazi dhambi hizo tunapokuwa tunamsikiliza Mtumishi wake Kanisani na kutuepusha na hatia. Unapokuwa peke yako tu nyumbani, ni rahisi kuyashikilia tu yale uliyoyazoea na kuona siyo dhambi, na hata Mungu akisema nawe kwa Roho wake, mara nyingi huwezi kuchukua hatua. Inahitaji njia ya wazi zaidi. Mungu hufanya hivyo Kanisani na kutufunulia yote kwa njia ya wazi kwa kuwatumia watumishi wake.
4. MUNGU HUTUPA MAJIBU YA MASWALI YETU NA KUYAFUMBUA MATATIZO YETU KANISANI
Unapokuwa unalitafakari Neno la Mungu mwenyewe nyumbani, unaweza ukabaki na mafumbo mengi. Mungu anafahamu hali hiyo. Unaweza pia ukawa na matatizo katika kuyafahamu mapenzi yake katika jambo fulani linalokuhusu. Mungu anafahamu hali hiyo. Unapokwenda Kanisani, Mungu hutafuta njia ya kukupa ufumbuzi wa tatizo lako katika ujumbe wa Neno la Mungu au kwa njia nyingi nyinginezo Kanisani, iwe ni ushuhuda wa mtu mwingine, uimbaji n.k.
ZABURI 73:16-17:
“Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; ikawa taabu machoni pangu; hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu nitautafakari mwisho wao.”
5. KARAMA MBALIMBALI ZA ROHO HUTUMIKA KANISANI KWA KUJENGANA:
Katikati ya watoto wa Mungu, pana tofauti za karama, tofauti za huduma na tofauti za kutenda kazi. Tunapokutanika pamoja, inakuwa ni rahisi mmoja kumjenga mwenzie kadri ya alivyopewa na Roho kwa neema. [1 WAKORINTHO 12:4-7; 1 WAKORINTHO 14:26].
AINA MBILI ZA MAKUSANYIKO KATIKA BIBLIA:
(a) Kanisa la Nyumbani:
[MATENDO 12:12; WAKOLOSAI 4:15; 1 WAKORINTHO 16:19]
- Makusanyiko ya watu wachache katika nyumba za waaminio kwa lengo la kuwa
karibu zaidi, kufahamiana kindugu na kusaidiana kiroho na kimwili; huku tukidumu katika Neno la Mungu na kuomba.
(b) Kanisa Kuu:
[MATENDO 2:42, 46-47; MATENDO 15:4; MATENDO 14:27; 1 WAKORINTHO 1:2; 1 WATHESALONIKE 1:1:]
Kusanyiko kuu linalojumuisha waaminio wote katika siku ya BWANA Jumapili na siku nyinginezo zilizopangwa.
Ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha anahudhuria katika Kanisa la Nyumbani, na Kanisa Kuu bila kukosa; kama ilivyokuwa desturi ya watakatifu wengine katika Kanisa la Kwanza. Huku ndiko kufurahi kumkaribia Mungu na kumtafuta KILA SIKU.
UCHAGUZI WA KANISA KUU
Tunapaswa mno kuwa waangalifu katika kuchagua Kanisa ambapo tutatambulika kwamba ni Washirika, na kuhudhuria hapo katika ibada za Jumapili na siku nyinginezo za wiki. Uchaguzi wetu ukiwa mbaya unaweza kabisa ukatugharimu kukosa uzima wa milele. Jambo hili linaweza likakushitua sana! Lakini ebu jaribu kuwaza pamoja nami. Je! mtoto mchanga anayenyonya akiwekwa juu ya matiti ya mama aliyekufa kwamba anyonye, mtoto huyo ataendelea kuishi? Jibu ni hapana: Mtoto huyo naye lazima atakufa. Biblia inasema kumcha BWANA ni MWANZO wa hekima [MITHALI 9:10]. Unapokata shauri kuokolewa, unakuwa ndiyo mwanzo wa kuwa na hekima. Hata hivyo inakupasa kuelimishwa ili uzidi kuwa na hekima, au siyo giza zito litakufunika [SOMA MITHALI 9:9]. Kwa hiyo jambo la kufanya ni kutafuta Kanisa ambalo limejaa hekima ya Mungu. Ukikaa hapo, na wewe utakuwa na hekima ya kukuwezesha kuingia mbinguni.
MITHALI 13:20a:
“Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima.”
Kanisa vuguvugu, litamfanya yeyote anayeingia pale awe vuguvugu na mwishowe atapikwe siku ya mwisho. Kanisa lililo mbali na kweli yote ya Mungu, litawafanya wale wote waingiao hapo waongozwe mbali na kweli na kuangamia. [EBU SOMA KWA MAKINI: MITHALI 16:29; MITHALI 22:24-25; 1 WAKORINTHO 8:10-11; WAGALATIA 5:7-9; YEREMIA 23:15; WARUMI 11:16]. Katika maandiko haya unaona jinsi ilivyo rahisi mtu kufuata nyayo za mahali pale alipo au watu alio pamoja nao. Neno la Mungu ni kweli.
Katika Ufunuo wa Yohana sura ya pili na sura ya tatu, tunaelezwa juu ya makanisa saba. Inakuwa ni vigumu mno kushinda na kupewa matunda ya uzima ukiwa katika Kanisa la Efeso; Pegamo; Thiatira; Sardi na Laodikia. Ukiwa katika Kanisa la Filadelfia ambalo linalitunza Neno la Mungu lote kwa gharama yoyote, utakuwa na nafasi kubwa mno ya kushinda.
Katika hekima ya dunia, wazazi huzunguka kumtafutia mtoto wao shule ambayo waalimu wake wana sifa ya kufundisha kwa bidii, ufahamu mkubwa; na wenye rekodi nzuri ya kupasisha wanafunzi wengi katika mtihani wa mwisho. Katika shule ya namna hiyo kunakuwa na nafasi nzuri ya mtoto huyo kushinda mtihani. Katika mambo ya rohoni ambayo ni ya milele ni lazima tuwe na maarifa hayo na zaidi!
MAMBO MATANO YA KUANGALIA KATIKA UCHAGUZI WA KANISA LAKO
1. USICHAGUE KANISA KWA SABABU LIKO JIRANI NA UNAPOISHI
Biblia inatuagiza kuutafuta Ufahamu wa Neno la Mungu kama:
(a) Fedha;
(b) Hazina iliyositirika (iliyofichika) [SOMA MITHALI 2:3-4]
Je fedha zinatafutwaje? Ukitaka kuzipata fedha inakubidi uwe tayari kuzitafuta hata ziwe mbali namna gani! Watu wanatoa nauli kwenda kufanya kazi ofisi au kiwanda kilicho mbali mno na pale wanapoishi. Watu wamehama makwao na kwenda maili nyingi sana na kujenga huko wakitafuta fedha, lakini hawako tayari kufanya hivyo wakitafuta Ufahamu wa Neno la Mungu. Je mkulima akitaka kulima mahali karibu na yeye tu, atapata fedha zinazotokana na mazao ya Kilimo? Watu, wako tayari kuyafuata mabonde yenye rutuba hata kama yako mbali namna gani! Ukitaka kulima mpunga kwenye Uwanja wa nyumba yako kwa kukwepa shida ya kulima mbali, unajua matokeo yake!
Je hazina iliyofichika inatafutwaje? Ni lazima uwe tayari kuchimba chini sana kwa gharama yoyote. Huwezi kupata madini ya thamani bila kuwa tayari kugharimika. Tanzania imetumia mamilioni ya fedha kufanya utafiti wa kupata petroli. Watu katika utafiti huo wana kwenda mbali sana na kuchimba chini sana. Kuchagua Kanisa kwa kuwa liko jirani na wewe, siyo kuchimba chini sana. Siyo kutafuta hazina iliyositirika. Katika MATHAYO 13:44-46, Yesu anaufananisha Ufalme wa Mungu na:-
(a) HAZINA ILIYOSITIRIKA KATIKA SHAMBA: (Msitari wa 44)
Mungu anasema ukimtafuta kwa bidii ndipo ataonekana kwako. Ufalme wa Mungu ni hazina iliyositirika katika shamba. Ni lazima uwe tayari kuitafuta kwa bidii hata kama iko mbali kiasi gani. Katika msitari wa 44, mtu yule alipoiona hazina hiyo aliuza VYOTE ALIVYO NAVYO na kulinunua shamba hilo. Ni lazima uwe tayari kutumia nauli au kutembea mwendo mrefu, kutafuta kweli ya Ufalme wa Mungu. Ukiridhika na vitu vinavyoonekana karibu, ujue hayo ni mawe tu na siyo hazina ya thamani.