Jumanne, 24 Desemba 2013

JE UNAJUA UMUHIMU WA KWENDA KANISANI JUMAPILI?


Pastor Carlos Kirimbai
MUHIMU SANA KWENDA IBADANI JUMAPILI.

Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA. (ZAB. 122:1 SUV).

Mungu aweke ndani yako hali ya kufurahia kwenda ibadani kila J2.

wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. (EBR. 10:25 SUV).

Kutokwenda ibadani kwa sababu yoyote ile sio tabia nzuri hata kidogo. Kusali peke yako, au kwa njia ya TV haijakaa poa. Uwe na kanisa ambalo unakwenda kuabudu. Uwe na mchungaji ambaye atawajibishwa na Mungu kwa habari ya ustawi wa roho yako. Uwe na mahali ambapo unalishwa ufahamu na maarifa.

nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu. (YER. 3:15 SUV).

Mahali pa pekee ambapo unaweza kupata huduma ya kichungaji ni kanisani. Unapokuwa huendi kanisani unapungukiwa na hii huduma ya kichungaji maishani mwako. Uwe sehemu ya kanisa. Muulize Mungu ni kanisa gani unataka niwepo ni Mchungaji gani unataka niwepo chini yake. Na akishakuweka hapo usimruhusu shetani kwa sababu yeyote akutoe.

Kondoo wa Mzee Yese waliyokuwa wanachungwa na Daudi walikuwa salama na mashambulizi ya dubu na simba. Hawakuwa kondoo wa Daudi walikuwa kondoo wa baba yake. Kondoo sio mali ya mchungaji maana kanisa sio mali ya mchungaji. Kanisa ni mali ya Mungu maana Yeye ndo amelinunua kwa damu yake mwenyewe. Kama Yese alivyomwasign mwanae Daudi wajibu wa kuchunga kondoo zake, Baba wa Mbinguni ameasign watu wajibu wa kulichunga kundi lake sehemu sehemu. Usalama wako dhidi ya mashambulizi ya adui unategemeana kuwa mahali ambapo Mungu amekuweka chini ya Mchungaji ambaye Mungu kakuchagulia. Mungu ndiye atupaye wachungaji sio sisi tunajichagulia. Mungu akakupe mchungaji anaoupendeza moyo Wake atakaye kulisha ufahamu na maarifa na atakaye tumika na Mungu kupambana na kila shambulio la adui kinyume nawe katika ulimwengu wa roho.

Wachungaji pia wana neema ya Kimungu juu yao kukunyakua toka mdomoni mwa adui.

Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi, mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua. (1 SAM. 17:34, 35 SUV).

Mchungaji ana neema ya kumpiga adui na kupokonya kondoo toka mdomoni mwa adui.

Hata kama kondoo kamezwaje bado mchungaji anaweza kumpokonya toka mdomoni mwa adui.

Haya ndiyo asemayo BWANA; Kama vile mchungaji apokonyavyo kinywani mwa simba miguu miwili, au kipande cha sikio; ndivyo watakavyopokonywa wana wa Israeli, wakaao Samaria katika pembe ya semadari, na juu ya mito ya hariri ya kitanda. (AMO. 3:12 SUV).

Unaona hii kitu. Mchungaji anaweza akampokonya toka kinywani mwa simba kondoo ambaye amemezwa hata kama ni tumiguu tuwili tu tumebaki au hata ni sikio tu limebaki. Usimdharau mchungaji wako maana hujajua neema aliyo nayo ya kuleta msaada wa Mungu kwako.

Kumbuka:

Na sisi tulio watu wako, Na kondoo za malisho yako, Tutakushukuru milele; Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (ZAB. 79:13 SUV).

Wewe ni mtu Wake na kondoo wa malisho Yake.

Kwa maana ndiye Mungu wetu, Na sisi tu watu wa malisho yake, Na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! (ZAB. 95:7 SUV).

Jueni kwamba BWANA ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (ZAB. 100:3 SUV).

Kama tu watu Wake basi tu kondoo Wake, wa mkono Wake na kila kondoo anahitaji mchungaji na anahitaji kundi na zizi. Kondoo sio mnyama solitary, wa pekee yake. Kondoo sio mnyama pori wa kujitafutia malisho yake mwenyewe. Kondoo ni mnyama wa kufugwa anahitaji kuchungwa, kutunzwa, kuangaliwa.

Ooooooo Mungu akatupe wachungaji wanaoupendeza moyo wake watakaojitoa kwa ajili ya kondoo na sio kudai kondoo wajitoe kwa ajili yao.

Najua unamwamini. Mungu sana ila kama hawa wasingekuwa na umuhimu Mungu asingewaweka. Hatutakiwa kuwa tegemezi kupita kawaida kwa wachungaji wetu lakini pia hatutakiwi kuipuuzia neema ya Mungu iliyo juu yao.

Mchungaji Mkuu Yesu Kristo anakuchunga kupitia huduma hii ya wachungaji waliyo chini yake.

Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka. (1 PET. 5:1-4 SUV).

Kwa hiyo wachungaji wote wanafanya kazi yao chini ya Mchungaji Mkuu wa kondoo Yesu Kristo.

Unahitaji kuchungwa na unahitaji usimamizi (supervision) ya kiroho na utayapata haya toka kwa mchungaji wako kanisani unapoabudu ambapo Mungu amekuweka.

Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. (MDO 20:28 SUV).

Unahitaji uangalizi na kulishwa na hiyo ni kazi ya huduma ya kichungaji.

Huduma ya kichungaji ni muhimu sana na kuwa na anuani ya kiroho ni muhimu sana. Kuwa sehemu ya kundi fulani ni muhimu sana. Kuwa kwenye zizi fulani ni muhimu mno.

Chukulia hili kwa uzito wake na utamwona Mungu kipekee maishani mwako. Huu ni utaratibu ambao Mungu ameuweka ukiuheshimu utaziona baraka za Mungu katika udhihirisho wake maishani mwako.

NENDA KANISANI KAABUDU NA UWE UNAFANYA HIVYO KILA MILANGO YA KANISANI KWENU INAPOGUNGULIWA HUSUSA J2.

Mungu akubariki sana. Nakupenda na nakuombea na natamani uwe baraka mahali ambapo Mungu amekuweka na kwa mchungaji au wachungaji ambao Mungu amekuweka chini yao.

SHALOM.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni