Ijumaa, 20 Desemba 2013

IJUE NA KUITUMIA NAFASI YAKO KAMA MLINZI KWENYE ULIMWENGU WA ROHO

Na: Patrick Sanga Shalom.

Napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mungu kwamba leo nimeweza kumalizia sehemu ya mwisho ya ujumbe huu maalum ambao nililazimika kuugawanya katika sehemu sita tofauti. Namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha katika hili na kwa ajili yako wewe msomaji kwa kutenga muda wako kuusoma na zaidi kuniombea. Naam karibu sasa tumalizie sehemu ya mwisho ya ujumbe huu wa pekee…

Biblia katika Isaya 56:10 “Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia, huota ndoto, hulala, hupenda usingizi’. Mpenzi msomaji jaribu kufikiri kwamba umeajiri walinzi kwa lengo la kulinda nyumba au Ofisi yako kutokana na umuhimu wako na mali zako pia. Baada ya mwezi mmoja jirani yako anakuambia, ndugu ‘Walinzi wako ni vipofu, hawana maarifa ya ulinzi, hulala na hupenda sana usingizi nk. je utajisikaje na utachukua hatua gani?



Naam hii ndiyo hali halisi ya walinzi wengi ambao BWANA amewaweka kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusudi lake.Shetani kwa kujua thamani na nafasi ya mlinzi/walinzi kwenye ulimwengu wa roho na mwili pia amewapofusha wengi macho yao kama alivyofanya kwa Samsoni. Naam anaendelea na ataendelea kufanya hivyo daima. Hii ni kwa sababu kufanikiwa kwa kazi zake kunategemea upofu wa walinzi wa BWANA kwenye maeneo yao ya ulinzi. Kadri wanavyokuwa ‘vipofu’ ndivyo wanavyomtengenezea fursa za kufanya kazi yake kwa urahisi.

Fahamu jambo hili kwamba, lengo la Shetani kupofusha macho ya Walinzi kwenye ulimwengu wa roho ni a)Kuwafanya washindwe kulitumikia kusudi la Mungu b)Kutumia upofu wao kupanda vitu vyake kwenye maeneo yao ya ulinzi na mwisho ili kuchinja na kuharibu (Yonana 10:10).

Katika kumalizia ujumbe huu wa pekee sana naomba nikukumbushe dondoo zifuatazo za msingi sana:

a) Mlinzi anapaswa daima kusogea mbele ya baraza la BWANA ili apate kusikizishwa na Mungu mambo ya watu wa eneo lake. Naam Mlinzi ndiye anayepaswa kuleta ufumbuzi wa changamoto kwenye eneo lake la ulinzi kwa kuwa ki – nafasi yeye ndiye mwenye maelekezo ya watu wa eneo lile.

b) Mlinzi ndiye mwenye fursa ya kuruhusu au kuzuia vitu kuingia kwenye eneo lake la ulinzi. Hivyo ni muhimu sana kwa mlinzi kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu, kwa kuwa mara kwa mara Mungu husema na Mlizi/Walinzi juu ya eneo husika.

c) Kumbuka vita ya kiroho ni vita ya matakwa (a war of will) kati ya Mungu na Shetani na kwa sababu hiyo kila upande utatumia walinzi wake kufanikisha mambo yake. Vita ya Mlinzi katika ulimwengu wa roho ni ya pekee sana, maana katika ulimwengu wa roho vita ya kiroho hupigwa kwa kuzingatia nafasi aliyo nayo mtu katika ulimwengu husika. Hivyo ni lazima Mlinzi awe makini kuhakikisha mawazo ya BWANA wake yanatimia (Yeremia 29:11).

d) Naam kufanikiwa kwa kusudi la Mungu duniani kunategemea utiifu wa Walinzi wake aliowaweka kwenye maeneo mbalimbali katika ulimwengu wa roho wakiwa katika ulimwengu wa mwili.



Ni imani yangu kwamba endapo umefanikiwa kusoma ujumbe huu kuanzia sehemu ya kwanza mpaka mwisho a) Ufahamu wako kuhusu nafasi ya mlinzi katika ulimwengu wa roho utakuwa umeongezeka b) Utakuwa umejua nini maana ya mtu kuwa mlinzi kwenye ulimwengu wa roho c) Utakuwa umejua au umeanza kujua umepewa kuwa mlinzi kwenye eneo gani d) Naam mwisho utasimama kwenye nafasi yako ili kuhakikisha kusudi la BWANA linatimizwa kwenye eneo lako la ulinzi.

Mambo mengi mabaya ambayo yanaendelea kwenye ndoa zetu, familia zetu, jamii, kanisa, nchi zetu nk yanachangiwa sana na walinzi ambao ni vipofu, laiti kila mlinzi angekuwa macho kwenye eneo lake la ulinzi, adui asingepanda magugu na kuharibu ngano (Asomaye na afahamu). Paulo aliwaambia hivi kanisa la Rumi ‘hii ni saa ya kuamka kutoka usingizini’(Warumi 13:11), pia kwa kanisa la Thesalonike alisema ‘Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe na kuwa na kiasi’.

Naam kupitia ujumbe huu, Mungu anakuita tena na tena, uamke kutoka usingizini kwa ajili ya ufalme wake na jina lake. Biblia inasema “Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza Kusudi Lake” (Wafilipi 2:13).

Endapo hukupata fursa ya kusoma kuanzia ujumbe wa kwanza bonyeza link zifuatazo kuusoma.

Sehemu ya kwanza bonyeza link hiihttp://sanga.wordpress.com/2011/11/20/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-ya-ulinzi-katika-ulimwengu-wa-roho/

Sehemu ya pili bonyeza http://sanga.wordpress.com/2011/12/07/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-2/

Sehemu ya tatu bonyeza http://sanga.wordpress.com/2012/02/03/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-3/

Sehemu ya nne bonyeza http://sanga.wordpress.com/2012/06/01/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-4/

Sehemu ya tano bonyeza http://sanga.wordpress.com/2012/11/05/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-5/

Sehemu ya sita bonyeza http://sanga.wordpress.com/2012/11/15/ijue-na-kuitumia-nafasi-yako-kama-mlinzi-kwenye-ulimwengu-wa-roho-part-6/

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni