Jumapili, 26 Januari 2014

MWALIMU LILIAN NDEGI AKAMIA KUUKOMBOA UZAO WA MWANAMKE

Ritha Chuwalo,
GK Guest Contributor

Mwalimu Lilian Ndegi akizungumza jambo kuhusu kitabu chake.
Wito umetolewa kwa wanawake wajawazito, wakina mama walio katika malezi pamoja na mabinti kusoma kitabu cha Mungu na Uzao Wangu kilichoandikwa na Mwalimu Lilian Ndegi wa Kanisa la Living Water Centre chini ya mtume Onesmo Ndegi lililopo Kawe jijini Dar-es-salaa, Tanzania.

Akitoa wito huo katika uzinduzi wa kitabu hicho hivi karibuni, Mwalimu Lilian Ndegi amesema kuwa, kitabu hicho ni msaada mkubwa kwa wakinamama wajawazito kwani watapata maarifa ya Ki-Mungu yatakayowasaidia kuwaondoa katika uharibifu wa mimba tangu inapotungwa, inapolelewa, pamoja na wakati wa kujifungua mtoto na kwamba hiyo inawahusu pia na mabinti ili kuwasaidia kuwa na uzazi mwema hapo baadae.

Akifafanua zaidi amesema kuwa Serikali ya Tanzania imeweka utaratibu mzuri wa kujenga vituo vya afya kuwasaidia wakina mama wajawazito, na kwamba mila na desturi nazo zina kanuni zake, lakini wakati umefika kwa Kanisa kujihoji Mungu anasema nini juu ya uzao wa Mwenye Haki na kwamba litembee katika kanuni zipi ili kuweza kupata ushindi mkubwa katika Uzazi.
Aidha amesema kitabu hicho kimebeba ujumbe wa Mungu wenye kusudi maalum juu ya maisha ya kiroho na kimwili, utakaofungua ufahamu wa watu na kuliona pendo kuu la Mungu juu ya maisha yao na uzao wao maana Mungu anaanza kushughulika na uzao wa mwenye haki kizazi hata kizazi.
Mwl. Lilian Ndegi ameongeza kuwa kama ambavyo ilikuwa kwa Ibrahim kupitia kitabu hicho cha Mungu na Uzao Wangu, wazazi na walezi kwa ujumla watajifunza mambo muhimu ambayo Mungu anawaagiza kufanya, kama sehemu ya wajibu wao kwa mfano; Mume kumtunza mkewe siku zote, kuwalea na kuwatunza watoto pamoja na kuziona athari za kinywa katika ulimwengu wa roho zinavyoweza kuathiri maisha ya uzao wao kutokana na kuwanenea maneno au kuwapa majina yasiyofaa kama vile kumwita mtoto majina kama Mateso na kadha wa kadha.


Mtume Onesmo Ndegi akinadi kitabu mara baada ya kuzinduliwa.

Kwa upande wake mgeni rasmi ambae ni mkuu wa makanisa ya Living Water Center nchini Tanzania, Mtume Onesmo Ndegi ambaye pia ni mume wa Lilian Ndegi, amewaasa Wanaume kuwa chachu ya mabadiliko katika ndoa zao, badala ya kujifanya wana misimamo isiyobadilika, na kuwataka kubadilika wao kwanza katika mitazamo yao juu ya wake zao na ndipo itakapo kuwa chachu kwa wake zao kubadilika kitabia na mienendo katika ndoa.

Aidha ametoa wito kwa vijana wa kiume kuwa na Mungu zaidi katika ujana wao ili kumpata mke mwema atokae kwa BWANA atakaeweza kuwa msaidizi wa kweli katika maisha kiroho na kimwili, huku akimshukuru Mungu kwa ajili ya Mke wake Lilian alie mtaja kuwa wa maana sana katika maisha yake na kwamba amefanyika baraka na msaada si tu katika huduma, bali pia kwenye familia kwa ujumla.


Mtume Onesmo Ndegi akimpongeza Mkewe, Lilian Ndegi.

Mtume Ndegi amewataka wanaume wote kuiga mfano huo wa kuwasifu wake zao na kuwashukuru pamoja na kuomba msamaha wanapokosea, ili ndoa zao zijengwe katika misingi ya urafiki na penzi la kweli na sio ubabe kama ilivyo miongoni mwa wanajamii wengi.
Kitabu cha Mungu na Uzao Wangu kimezinduliwa tarehe 19 jan 2014 ambapo pamoja na mambo mengine Mwl. Lilian Ndegi ameelezea kwa kina juu ya Uzao wa mwenye haki, Nalikujua kabla ya Mimba Haijatungwa Tumboni mwa Mama Yako, Nafasi ya Mwanamume Wakati wa Ujauzito Mpaka Malezi, Magonjwa na Mateso Mengineyo Katika Kipindi cha Ujauzito, Mtazamo wa Wazazi juu ya Uzao Wao, Mtazamo wa Mungu juu ya Uzao wa Mwenye Haki, Mwanamke anahitaji ujasiri Mwingi wakati wa Kujifungua pamoja na uzazi wa Mpango ndizo sura 8 za kitabu hicho.



Mtume Ndegi na mkewe wakikata keki kuashiria uzinduzi wa kitabu cha Mungu na Uzao Wangu hivi karibuni jijini DSM.

Mwl. Lilian Ndegi akimlisha keki Mch.Naomi Mhamba wa Living water Centre Kawe Dar es Salaam



Mtume Onesmo Ndegi akisalimiana na mhariri wa kitabu cha Mungu na Uzao Wangu, Mzee Ernest Tarimo



Sifa kwa kwenda mbele, Mkurugenzi wa makanisa ya Living Waters Tanzania, Mchungaji Grace Mbwiga (wa kwanza kushoto)


Upendo Nkone akisindikizwa na wenyeji wake kumsifu Mungu.


Sifa zikiendelea kurudishwa kwa BWANA Yesu muweza wa yote,



Mtangazaji wa WAPO Radio FM, MC Ritha Chuwalo (wa kwanza kushoto) akifurahia jambo pamoja na umati.


Salamu za kipekee, Mtume Onesmo Ndegi na Bwana Diesco Rugambage mara baada ya salamu na kuahidi.




Katibu Mkuu makanisa ya Living Waters Tanzania Mch. Peace Matovu madhabahuni akimkaribisha Mgeni rasmi Mtume Ndegi hayupo pichani.
Hiki ni kitabu cha pili kikitanguliwa na kitabu chake cha kwanza JE UNASAMEHE? Ambavyo vyote vinapatikana madukani jipatie nakala yako kwa jumla na rejareja kwa kupiga simu namba 0754465578 au 0655465578 ma kwa kuwasiliana na mwandishi kwa barua pepelilyonesmo@gmail.com web: www.lwc.or.tz.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni