Jumapili, 26 Januari 2014

HOJA YA ASKOFU GAMANYWA: FALSAFA YA UMILIKAJI KWA MUJIBU WA BIBLIA (3)


Rais wa WAPO Mission International, Askofu Sylvester Gamanywa.
Katika makala yaliyopita tulisoma habari kuhusu “Mpango wa pili wa Mungu ukombozi wa binadamu” ambao uliambatana na “Majibu ya maswali nyeti kuhusu falsafa ya kumiliki” aidha niliahidi katika makala hii kwamba nitaweka bayana tofauti kati ya “Hi Falsafa ya umilikishaji kwa mujibu wa Biblia na “Injili ya utajirisho”. Leo naanza na muhutasari wake:Utoaji unaotambulika
Nianze kuweka tahadhari mapema kuhusu habari za utoaji wa fedha kama sadaka na matoleo kwenye mikusanyiko ya ibada za kidini. Kimsingi, utoaji unaotambulika rasmi Lazima ulenge taasisi yenye mfumo rasmi wa mapato na matumizi ya fedha kwa mujibu wa sheria za nchi. Mathalani, makanisa yenye usajili wa kisheria, na uongozi unaotambulika kikatiba, na washirika wanachama wanaochagia gharama za huduma za kikanisa kupitia makusanyiko ya kiibada.

Kupitia mfumo huu, mapato ya matumizi yanakuwa katika bajeti iliyoidhinishwa na vikao rasmi vya uongozi wa kikanisa, na kuna uwajibikaji katika utunzaji wa fedha zinazokusanywa kutoka kwa washirika ambao umeanishwa ndani ya katiba na miongozo ya kikanisa.

Isitoshe, lazima kuwepo na watu maalum maarufu kama “wadhamini wa mali na fedha” ambao kwa mujibu wa sheria za nchi na kwa niaba ya taasisi, kazi yao kubwa ni kuidhinisha bajeti ya mipango na kupokea ripoti za fedha za taasisi.
Mtindo wa utoaji wa “Injili ya utajirisho”
Utoaji katika mitindo ya “Injili za Utajirisho”; ni “utoaji huru” usio na mipaka wala udhibiti na uwajibikaji kwa sababu; mali na fedha hizo hupewa “watu binafsi” waliojitambulisha kuwa ni “wapakwa mafuta maalum” wakidai kwamba wanayo mamlaka maalum ya “kuvunja laana za umaskini wa kipato” kwa watoaji.
Mapato na matumizi ya fedha zinazopokelewa na hawa “watumishi wenye upako maalum” huishia katika mamlaka binafsi ya wapokeaji; na hakuna aina yoyote ya uwajibikaji wa kifedha kwenye uongozi wa kitaasisi kwa mujibu wa sheria.
Wakusanyaji na wapokeaji wa matoleo/sadaka ya injili ya utajirisho, kwa kupitia “mwavuli wa maombezi” hukusanya fedha kutoka kwa watu binafsi katika jamii, au kupitia mikutano ya hadhara au kupitia vyombo vya habari. Lakini fedha hizo hubaki kuwa ni mali yao binafsi na sio fedha za taasisi kwa malengo ya kitaasisi.
Pengine niweke wazi zaidi hapa, hoja yangu ya msingi haiku kwenye “wapokeaji kama watu binafsi” kupokea fedha kutoka kwa “watu binafsi na kuzitumia kibinafsi”; (hii na mada nyingine) hoja yangu hapa ni “kishawishi kinachotumika kukusanya fedha“ kutoka kwa watu binafsi katika jamii. Kishawishi chenyewe ni madai kwamba, wakusanyaji kwa jina la “wapakwa mafuta” kuwa na “upako wa kuvunja laana ya umaskini wa kipato” katika maisha ya watoaji lakini kwa sharti la “kutoa fedha kama kanuni pekee ya kuvunjiwa laana ya umaskini” !!
Athari za nadharia hii, hususan katika Bara la Afrika, ni kwamba, wako mamilioni ya watu wengi ambao (wamekutana, ama ana kwa ana, au kupitia vyombo vya habari) wakisikiliza Injili ya Utajirisho na kushawishika wakatoa mali na fedha zao, kwa “matarajio ya kuvunjiwa laana za umaskini wa kipato”! Lakini baada ya kuwa wamekwisha kutoa fedha zao, na kufanyiwa “maombezi ya kuvunjwa laana ya umaskini wa kipato”; bado maisha yao huendelea kuwa duni siku zote; wakati ambapo“maisha binafsi ya “wapakwa mafutwa wa injili ya utajirisho” ndio huonekana kuwa mazuri kiuchumi kuliko jamii ya watu waliochukua fedha zao!


Tofuati kati ya “Injili ya utajirisho” na “Falsafa ya kumilikisha” kwa mujibu wa Biblia


Misingi ya falsafa ya kumilikisha inalenga kuwafungua binadamu kujitambua kuwa suala la kuvunjwa laana ya umaskini wa kipato ni kazi iliyokwisha kufanywa na Bwana Yesu alipotundikwa juu ya msalaba zaidi ya miaka 2014 iliyopita:
"Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake." (2 KOR. 8:9)



Kwa mujibu wa maandiko haya, tunasoma kwamba, Yesu Kristo mwenyewe alifanyika “maskini wa kipato” kwa ajili yetu, ili kila amwaminiye apate “kufanyika tajiri”! Kimsingi, kazi ya “kuvunjwa kwa laana ya umaskini wa kipato” alikwisha kuifanya Yesu Kristo mwenyewe.

Utoaji unaofanyika katika Agano Jipya ni “Shukrani kwa kazi iliyokwisha kufanywa na Yesu Kristo kwa ajili yetu” na sio malipo au kigezo cha “kuvunjiwa laana ya umasikini wa kipato” katika maisha binafsi ya mtoaji.
Hatutoi ili tubarikiwe kwa utoaji wetu, bali tunatoa kwa kwa shukrani kwa sababu tumekwisha kubarikiwa kwa kazi aliyoifanya Yesu Kristo kwa ajili yetu.
Mamlaka ya kumiliki haitokani na juhudi zetu binafsi za kibinadamu, bali inatokana na nafasi tuliyopewa kwa neema na Yesu Kristo kupitia kazi aliokwisha kuifanya kwa ajili yetu.

Maombezi ya aina yoyote inayolenga watu kufunguliwa katika vifungo vya pepo wabaya, magonjwa na umaskini inatakiwa kuwa ni matokeo ya Injili ya wokovu wa Yesu Kristo ambapo wahusika wanawajiibka kutubu dhambi na kumpokea Yesu Kristo na wafanye hivyo pasipo masharti ya kutanguliza fedha kama kanuni ya kufunguliwa!
Kumbuka kwamba Yesu Kristo mwenyewe alipowaagiza mitume wake kuhuburi Injili yake aliwaonya akisema:

“Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure toeni bure.” (Mt.10:8)
Kupitia Falsafa ya kumilikisha tunakwenda kudhihirisha siri kubwa ya ufanisi wa kanisa la kwanza la mitume ambapo ndilo sisi tumejengwa kiiimani juu ya msingi wake. Humo tunajifunza jinsi ya “kutawala badala ya kutawaliwa”, jinsi ya “kufanyika Baraka” badala ya kutaka “kubarikiwa kibinafsi peke yake”, na jinsi ya kuzalisha uchumi endelevu ili kuwezesha wengine badala ya kujilimbikizia utajiri kibinafsi peke yake.
Itaendelea toleo lijalo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni