"Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapofanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana." (Yoshua 1:8) Mtu mmoja aliwahi kuniuliza swali hili: "Je kutafakari maana yake nini?" Kila mara ninapofundisha somo hili nakutana na swali la jinsi hii . Naamini kuwa swali hili linawatatanisha wengi kwa sababu bado hawajatofautisha kati ya kusoma neno na kutafakari neno. Kusoma neno ni tofauti na kutafakari neno. Kulitafakari neno ni zaidi ya kulisoma neno. Watu wengi huwa wanasoma neno zaidi kuliko kulitafakari. Kutafakari maana yake nini? Maana ya karibu sana ya neno kutafakari ni kuwaza. Ni kusoma neno huku unalicheua na kulitafuna rohoni mwako. Kutafakari ni njia mojawapo kubwa ya kuweza kuilisha roho yako. Yesu Kristo alisema "Imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu." (Mathayo 4:4) Mkate ni chakula cha mwili wa nje ulio wa nyama na damu; neno la Mungu ni chakula cha mwili wa kiroho. Kinywa kinapokea chakula na meno yanatafuna.na kukivunjavunja huku kikilainishwa na mate, tayari kwa kumeza. Kusoma neno ni kama kinywa, kazi yake ni kulipokea neno. Kutafakari ni kuvunjavunja hilo neno huku Roho wa Mungu akililainisha liwe tayari kumezwa na roho yako. Kutafakari neno kunamletea mtu siri ya ajabu ya uhakika na ushindi ndani ya Kristo.
Sisi ni watenda kazi pamoja na neno la Mungu hapa ulimwenguni. Tunaliwakilisha Neno la Kristo mahali tulipo na ulimwenguni pote. Na kwa sababu hiyo, Imeandikwa, "Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote." (Wakolosai 3:16) Huwezi ukawa na Neno la Kristo moyoni mwako bila ya kuitumia siri ya kutafakari. Kukariri neno la Kristo hakutoshi peke yake kukuletea uhakika na ushindi kiroho na kimwili kama vile kutafakari kunavyofanya ndani ya mtu. Kutafakari ni kuwaza. Kulitafakari jina la Yesu Kristo ni kuliwaza jina hili.
Tatizo kubwa sana ambalo linawapata watu ni tatizo la mawazo. Na huu ni ugonjwa mkubwa sana ambao umewakwamisha wengi katika maisha yao ya kiroho. Kutafakari na kuwaza ni jambo la rohoni, - ni jambo la rohoni! Si jambo la akili kama wengi wanavyodhani. Mtu anapowaza, au kutafakari jambo huwa ni jambo linalofanyika rohoni mwake, ingawa utadhani linafanyika katika ubongo. Je! Wewe unayesoma somo hili sasa hivi unawaza nini rohoni mwako, unatafakari nini? Mara nyingi utaona mtu anaposoma Neno mawazo yake mara nyingi yanakuwa mbali sana, kwa hiyo hakuna anachoelewa katika hayo anayosoma. Pia, hata wakati watu wanasikiliza neno la Mungu, mara nyingi mawazo yao yanakuwa mbali sana na neno linalofundishwa. Hii inajidhihirisha hasa ukimwuuliza mtu huyo muda mchache baadaye, juu ya neno lililofundishwa maana hatakumbuka. Unapoumwa huwa unawaza nini? Wengi wanautafakari ugonjwa, na wengine hata kukata tamaa anapoona hauponi haraka. Wengine wanapoumwa wanawaza na kutafakari kufa kuliko kuishi. Unapokuwa una matatizo huwa unawaza nin? Unapokosa maelewano na mwenzako, nyumbani, kazini au mahali popote, huwa mawazo yako yanawaza nini? Unapokuwa huna fedha au vitu fulani vya kimwili huwa unawaza au kutafakari nini? Tunaweza kusema mengi lakini swali kubwa ni hili; "Kila wakati huwa unawaza nini na kutafakari nini?" Je! unafahamu ya kuwa matendo yako na maneno yako , ni matokeo ya mawazo uliyonayo? Mtu husema anachokitafakari au kukiwaza, na pia hutenda anachokitafakari au kukiwaza moyoni mwake. Ukitaka kumfahamu mtu alivyo rohoni mwake, sikiliza maneno anayosema na angalia matendo anayoyatenda. Sijaona katika biblia ambapo mtu wa Mungu ameambiwa aitafakari shida yake, awaze juu ya ugonjwa wake au udhaifu wake. Kumbuka kuwa maneno ni chakula cha roho, hali ya roho yako inategemea sana ni maneno gani unayasikia kila wakati na kuyatafakari. Unapotafakari shida, magonjwa, hofu, unaifanya roho yako ijengeke katika hayo. Ukilitafakari jina la Yesu Kristo roho yako inajengeka katika jina hili. Watu wengi sana wamejengeka katika kumwogopa shetani kuliko Mungu. Hii hali ipo hata kwa watu wa Mungu. Hayo ni matokeo ya kumtafakari shetani na majaribu anayowajaribu, kuliko kumtafakari Mungu na uweza wake. Neno la Kristo linakosa nafasi katika roho za watu, kwa sababu roho za watu zimejaa mawazo ya dunia hii na shida zake. Roho za watu zimejaa mawazo yanayopinga na kwenda kinyume kabisa na neno la Kristo. Roho za mtu ni uwanja wa vita. Ukishinda vita katika mawazo, utakuwa umeshinda vita katika mwili, katika roho na katika maneno. Wakati mmoja nilianza kujiuliza kwa nini Nabii Ezekieli aliambiwa ale gombo la chuo, na mtume Yohana aliambiwa ale kitabu kilichofunguliwa. Sikuelewa kwa nini hawakusoma tu maneno ambayo yalikuwa yameandikwa bila kula gombo la chuo na kitabu kilichofunguliwa. Mungu alikuwa ana uwezo wa kuwaambia wayasome maneno aliyokuwa anawaonyesha - lakini badala yake aliwaambia wale - kwa nini? Nilikuwa siioni tofauti ya kusoma na kula. Kuna tofauti kubwa kati ya kusoma ujumbe wa Mungu na kula ujumbe wa Mungu. Soma Ezekieli 2:7 10; 3:1 - 3 na Ufunuo wa Yohana 10:1 - 2; 8 - 11. Mtu anapokula chakula, huwa kinatafunwa na kulainishwa kabla ya kumezwa. Na kikimezwa na kuingia tumboni, kinanyonywa na kuingia katika mishipa ya damu inayozunguka mwili mzima na kukisambaza chakula hicho katika sehemu zinazohitajika. Mtu anapotembea, ukweli ni kwamba ni chakula kile alichokula ndicho kinachotembea. INGAWA yeye ndiye anayeonekana anatembea. Kwa hiyo Ezekieli na Yohana walipokula ujumbe wa Bwana uliokuwa umeandikwa katika gombo la chuo na katika kitabu kilichofunguliwa, ujumbe huo uliingia ndani yao kama vile ambavyo wangekula nyama. Ujumbe huo uliingia kwenye damu yao na ukajenga misuli. Kila sehemu ilikuwa imejaa ujumbe wa Mungu. Ujumbe huo ndio uliowafanya wapate nguvu ya kutembea, na kuishi na kusema.
Kwa mtazamo mwingine tunaweza kusema, Ezekieli na Yohana walikuwa ni ujumbe wa Mungu uliokuwa unatembea. Na sisi tukilitafakari neno la Kristo; na likijaa ndani yetu kwa wingi, tunakuwa ni neno la Kristo linalotembea; tunakuwa ni neno la Kristo linalosema; tunakuwa ni neno la Kristo linaloponya. Tunafika mahali ambapo kuishi kwetu kunakuwa ni neno (Kristo) - kama vile Paulo alivyosema "Kuishi ni Kristo" (Wafilipi 1:21). Tukilitafakari jina la Yesu Kristo, tunakuwa ni jina la Yesu Kristo linalotembea,,, Je! unauona umuhimu juu ya jambo ninalokuambia la kutafakari? Mtu anashindwa kuwa mtendaji wa Neno kwa kuwa moyoni mwake hakuna neno. Anabaki kuwa mtendaji wa maneno mengine aliyonayo mawazoni mwake tu. "Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome); tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakorintho 10: 3 - 5). Hii ina maana kuwa fikra zako ziwaze sambamba na Neno (Kristo).
Katika kuishi kwetu na kuenenda kwetu tuwe tunatafakari nini mioyoni mwetu, ili roho zetu zipate chakula safi cha kiroho?
"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema, ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote YATAFAKARINI HAYO" (Wafilipi 4:8). Mambo yote haya yaliyotajwa utayakuta katika neno la Mungu. Kwa kutafakari neno la Kristo usiku na mchana katika mambo yote ndipo utakapoifanikisha njia yako ya wokovu na ndipo utakapositawi sana kiroho na kimwili. Na biblia inasema mtu anayelitafakari neno la Mungu usiku na mchana; anakuwa mtu wa namna hii. "KILA ALITENDALO LITAFANIKIWA" (Zaburi 1:3)
Jina la Yesu Kristo ni la kweli; Jina la Yesu Kristo ni la haki; tena ni safi; tena ni la kupendeza; tena lina sifa njema na nzuri. Tafakari juu ya jina hili usiku na mchana - au waza juu ya jina hili usiku na mchana. Fanya hivyo na wewe utafanikiwa katika kila ulitendalo kwa jina la Yesu Kristo.
Unapoumwa usitafakari ugonjwa, wala kuwaza maumivu yake, bali tafakari neno la Mungu juu ya uponyaji nalo litakuwa afya mwilini mwako. Ndiyo maana imeandikwa hivi; "Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako,, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; uzihifadhi NDANI YA MOYO WAKO. Maana ni uhai kwa wale wazipatao,na AFYA ya mwili wao wote" (Mithali 4:20 - 22) Unapolitafakari neno la Mungu ndipo unapolihifadhi neno hilo ndani ya moyo wako. Na neno la Mungu likihifadhiwa ndani ya moyo wako litakuwa AFYA mwilini mwako, na magonjwa hayatakusumbua tena. Ukilihifadhi neno la Mungu lenye nguvu za uponyaji ndani ya moyo wako utajua hakika kwamba "kwa kupigwa kwake (Yesu Kristo) sisi tumepona" (Isaya 53:5) Wengi wanapata matatizo katika kupokea uponyaji kwa sababu wanaamini kuwa Mungu atawaponya siku moja akipenda kwa sababu wameomba au wameombewa. Hili ni tumaini na siyo imani. Imani ya uponyaji huja kwa kusikia na kutenda neno la Mungu linalozungumzia uponyaji. Neno linatuambia ya kuwa tulipona siku nyingi zilizopita kwa kupigwa kwake Yesu Kristo na SIYO tutapona siku moja. Unapompokea Kristo moyoni mwako, magonjwa yanakuwa hayana tena mamlaka juu yako. Na ili uwe na uhakika wa afya ya mwili wako kila wakati, inakubidi uwe na tabia ya kulihifadhi neno la Kristo moyoni kwa kulitafakari. (Itaendelea) Siku moja mtu mmoja aliyekuwa anaumwa aliniambia kwa huzuni; "Mimi nimeombewa kwenye mkutano wa injili lakini bado sijapona, ingawa niliwaona wenzangu wengi wakisimama kushuhudia kuwa wamepona". Nikamwambia; "Na wewe umepona lakini tatizo lako ni kwamba hujui ya kuwa umepona".
Akauliza kwa mshangao; "Inawezekana wapi mtu asijijue ya kuwa amepona na huku bado maumivu anayo hata baada ya maombezi?" Roho wa Mungu akanionyesha kwa undani zaidi kwa nini mtu huyo alishindwa kupokea uponyaji. Nikamwambia; "Uponyaji huwa unapokelewa kwanza katika roho na ndipo unajidhihirisha katika mwili. Wewe ulitaka kwanza uone maumivu yamekwisha, ndipo uamini moyoni mwako ya kwamba umepona. Unatakiwa uwe na uhakika kuwa umepona kwa sababu neno la Mungu linasema umepona na siyo mwili unasemaje," Mtu huyu alikuwa na tatizo ambalo watu wengi wanalo. Ni tatizo la kukosa uhakika unaodumu wa kuhusu roho zao na miili yao. Yesu Kristo alisema kwa jina lake tutatoa pepo, na tukiweka mikono yetu juu ya wagonjwa watapata afya - na ndivyo ilivyo. Amini neno la Kristo alilosema juu ya jina lake na utafanikiwa. Neno la Mungu ndilo kweli inayodumu milele. Neno la Mungu ndilo linalompa mtu uhakika wa jambo ambao hauwezi kuyumbishwa na kitu cho chote. Neno la Mungu linahifadhiwa ndani ya moyo wa mtu kwa kulitafakari na siyo kwa kukariri peke yake. Mtu anayekariri mistari ya biblia ni sawa sawa na mtu anayekula mahindi au chakula cho chote bila kutafuna.
"Neno la Kristo na likae moyoni mwako kwa wingi katika hekima yote" (Wakolosai 3:16) Kumbuka, Neno la Mungu moyoni mwako ndilo linalokupa uhakika wa mambo yako yote; (Wokovu, uponyaji, ushindi katika majaribu; mamlaka yako juu ya shetani na kazi zake, uzima wa milele, na kadhalika). Na huo ndio msingi mkubwa wa Imani, kwa kuwa "Imani ni kuwa na hakika ya mambo ........." (Waebrania 11:1). Kabla imani yako katika Kristo haijaonekana katika matendo yako na maneno yako ni lazima ijengeke kwanza katika moyo wako kwa njia ya kulitafakari au kuliwaza neno la Mungu katika mambo yako yote. Matokeo yake ni kwamba utakuwa na uhakika wa jambo lo lote moyoni mwako na kwa ajili hiyo utakuwa na ujasiri wa kulisema na kulitenda. Usipokuwa na uhakika wa jambo moyoni mwako, huwezi ukawa na ujasiri wa kulisema na kulitenda. Neno la Mungu ndilo nuru na taa miguuni petu sisi tulio ndani yake (Zaburi 119:105); na kwa sababu hiyo tunaishi katika imani iliyo na uhakika udumuo, na wala si wa kubahatisha. Kwa sababu ya umuhimu wa kutafakari neno la Kristo, hapa ninaorodhesha baadhi ya mistari inayozungumza juu ya jina la Yesu Kristo. Soma maneno yaliyomo na kuyatafakari mara kwa mara na baada ya muda utaona ushindi wa ajabu utakapokuwa unalitumia jina hili la Yesu Kristo.
Hakuna wokovu katika mwingine: "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo" (Matendo ya Mitume 4:12). "Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao" (Mathayo 1:21). "Bali wote waliompokea (Yesu Kristo) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake, waliozaliwa si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu" (Yohana 1:12 - 13) "Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani, maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, kila atakayeliitia jina la Bwana (Yesu Kristo) ataokoka" (Warumi 10:12 - 13).
Ni amri kuliamini jina la Yesu Kristo - sio ombi: "Na hii ndiyo amri yake, kwamba TULIAMINI JINA LA MWANA WAKE YESU KRISTO, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri" (1Yohana 3:23) "Amwaminiye yeye (Yesu Kristo) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini JINA LA MWANA PEKEE WA MUNGU" (Yohana 3:18)
Kuna uponyaji katika jina la Yesu Kristo: " Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; ........ wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya" (Marko 16:17 - 18) "Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliitia jina la Bwana ataponywa ..." (Yoeli 2:32).
Lolote ulifanyalo - lifanye katika jina la Yesu Kristo: "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye" (Wakolosai 3:17).
Kuomba na kupewa katika jina la Yesu Kristo "Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya ..... Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia" (Yohana 14:13 - 14; 26). "Si ninyi mlionichangua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni" (Yohana 16:23 - 24).
Jina lipitalo kila jina "Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba" (Wafilipi 2:9 - 10) Hii ni baadhi tu ya mistari mingi iliyomo katika Biblia inayozungumza juu ya jina la Yesu Kristo. Waza juu ya jina la Yesu mara kwa mara na hakika utafanikiwa. (Usikose somo hili litaendele wiki ijayo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni