Jumapili, 8 Septemba 2013
NDIMI ZITEMAZO KWELI!
Mimi si mwanasiasa, japo siwezi kujitenga na siasa kwani ndio mustakabali wa maisha ya mwanadamu kwenye ulimwengu wa mwili.
Ukiachilia ulimwengu wa kiroho, hivi nilivyo leo naakisi siasa za Tanzania, kwa kuwa ndizo zilizozaa sera ya elimu niliyosoma, hospitali niliyotibiwa nilipougua na sasa kazi ninayofanya. Hii ndiyo maana napata ujasiri wa kusema wazi kwamba japo si mwanasiasa lakini siwezi kujitenga na siasa.
Hoja yangu leo imejikita katika siasa, nikimulika kurunzi yangu katika ndimi za aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Tanzania), Bw. Edward Ngoyai Lowassa, pamoja na wenzake wanaotajwa sasa katika kasi ya kuwania kiti cha heshima ndani ya jumba jeupe “Ikulu”.
Kimsingi Lowassa anasura nyingi, wengine wamethubutu kumwita shujaa, na baadhi kumwita majina ambayo sina ujasiri wa kuyataja. Wanaomuita shujaa wanadai eti ni mwenye maamuzi, si mnafiki akisema ndio anamaanisha ndio, na hapana anamaanisha hapana.www.mwakasegebibilia.blogspot.com
Wiki jana alivuta hisia zangu nikaamua kumualika kwenye safu hii nikitafakari jambo moja kwa kina miongoni mwa mambo ya kustaajabisha aliyothubutu kufanya.
Akiwa katika kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na Luninga ya ITV, ya jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema kamwe hakubaliani na sera ya Kilimo kwanza inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa nchi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Lowassa, kilichodhamini ubunge wake.
Kwa madai yake, Lowassa, anasema hakubaliani na sera ya Kilimo kwanza kupewa kipaumbele, badala yake angependelea ‘Elimu Kwanza’. Nikiweka kando ubora wa hoja wanazozungumzia wawili hawa ambao mwaka 1995, walipanda ndege moja wakasafiri nchini kusaka uungwaji mkono ili wawanie urais, wakabatizwa jina la ‘Boys II Men’ ingawa kura hazikutosha na ‘mr. Clean’ Benjamin William, Mkapa akashinda kwa msaada wa Mwl. Nyerere.
Msimu wa uchaguzi ulipowadia tena (2005) nyota ya wawili hawa ikawaka tena, mmoja akawa Rais na mwingine Waziri Mkuu, ingawa mmoja alipata ajali ya kisiasa kwa kujikwaa kwenye furushi la kashfa ya Richmond na kulazimika kujiuzulu.
Lakini ninalotazama hapa ni moja kubwa! Ujasiri wa kusimama mbele ya hadhira na kumpinga ‘mshirika’ wako wa zamani, tena ukijua ni mwenyekiti wa Chama chako, Rais na Amiri Jeshi. Ni lazima mtu anayefanya hivyo awe jasiri na shujaa wa kweli anayeweza kusema kweli hata mbele ya upanga.
Katika moja ya tafiti bora zilizowahi kufanywa kuhusu uongozi na viongozi wa bara la Afrika ilitoa majibu haya:
“Bara la Afrika linaangamizwa na dhambi ya unafiki, idadi kubwa ya viongozi na hata waongozwa wanacheka usoni wakati mioyo yao imenuna. Wanasema karibu machoni, wakati moyoni wanatamani uage haraka na kuondoka. Ni wanafiki waliopindukia mipaka.” (utafiti huu ulifanywa na Dk. Moses Herman, wa Oxford University ya Uingereza.
Katika utafiti huo uliohusisha mataifa kadhaa ya Afrika, Dk. Herman anasema wanasiasa wengi wanakataa matokeo ya baada ya kura na hata kuingia msituni kwa kuwa wapiga kura wanafiki waliwapa matumaini ya ushindi mkuu kwa kuwashangilia kwenye mikutano ya kampeni, wakati kwenye masanduku ya kura walichangua wengine na hilo huwafanya wagombea kudhani wameibiwa kura zao.
Naamini watafiti hao wangemkuta Lowassa, wangeweza kuwa na mtazamo tofauti kwa kuwa yeye amethubutu kuonesha msimamo wa kile anachoamini, hata kama ni kinyume na matakwa ya wengi ikiwa ni pamoja na Amiri Jeshi Mkuu.
Nasema hivyo kwa kuwa msingi wa siasa safi ni ukweli, hata kama ukweli huo unapingwa na wengi, utasalia kuwa ukweli unaodhihirisha imani ya kweli.
Lowassa katika hoja yake anasema anapingana na hoja ya Kilimo Kwanza kwa kuwa haitekelezeki bila wakulima kuwa na elimu ya kutosha.
Akipingana naye, Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka, alisema: “Watu kijijini hawawezi kupokea elimu wakati wana njaa.”
Lo! Hili ni jibu jepesi katika hoja nzito. Nasema hivyo kwa kuwa kilimo cha leo sio kile cha mwaka 47 cha jembe la mkono, kilimo cha leo katika ardhi iliyochoka, kinahitaji zana za kisasa, mbolea kutoka viwandani inayohitaji maelezo ya kitaalam, maofisa ugani walio na ujuzi wa kitaalamu.
Mfano; leo hii tunakula matunda Apple kutoka Afrika Kusini na Israel, tunda moja linauzwa kati ya shilingi 600-1000, Tanzania tuna ardhi kubwa na bora kuliko Israeli, tuna maji ya kutosha na watu wengi kuliko wao, lakini tunapungukiwa jambo moja tu ‘elimu bora ‘ ni tofauti hiyo, kwamba wao wanajua mbinu za kutumia ardhi kidogo kuzalisha sana, wakapaki vyema na kusafirisha hadi kwetu watuuzie.
Sisi tunalima mananasi tukivuna tunauza bei chee, na asilimia kubwa yanaoza, kidogo yananunuliwa na waarabu wanakwenda nayo jangwani wanakamua juice na kutuletea kwenye supermarket tununue kwa bei ya shilingi 3000.
Tuungane na Lowassa kusema kweli kuwa elimu ni ufunguo wa mafanikio katika kila nyanja, kikiwepo kilimo na vinginevyo. Ndio maana hata Biblia takatifu inatutaka kuzingatia elimu.
Tena mahali pengine inasema: “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.” Sehemu ya maarifa tunayokosa hadi tuangamie kwa njaa na ukosefu wa virutubisho muhimu miilini mwetu ni elimu bora, inayotuwezesha kulima kwa kuzingatia tafiti za kisayansi, zinazoamua udongo gani ulimwe mazao gani, kwa wakati gani, yakishalimwa yalindwe dhidi ya wadudu kwa mbinu gani, na yakishavunwa yahifadhiwe kwa mbinu gani. Bila elimu Kilimo Kwanza ni sawa na kuhifadhi maji kwenye pakacha, hakika yataishia chini hata kama utayakumbatia kama mwana mchanga.
Nimalizie kwa kuwaasa watanzania kuacha unafiki, nyeusi waiite nyeusi na nyeupe waiite nyeupe, hata kama aliyeileta ni bora na mwenye mvuto kiasi gani. Lazima tukue tufikie mahali pa kujadili hoja badala ya mtoa hoja. Tukatae hoja kwa ubaya wake, bila kujali sura ya mtoa hoja.
Nawashauri watanzania wenzangu tutubu dhambi ya kuwa wanafiki, kushangilia huku mioyo imenuna na kununa huku mioyo inacheka. Tabia ya unafiki au kuwa vugu vugu, kujipendekeza kila upande ni ya ushetani na Biblia inaonya watu vuguvugu ikisema:
“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. ……..Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii ukatubu.” (Ufunuo 3: 15-19).
Ingawa andiko lililenga kwa watu wanaoishi maisha ya mseto baina ya shetani na Mungu, lafaa kujifunza leo na kuukimbia unafiki wa aina yoyote ile, kama vile Msafiri alivyopiga mbio kuukimbia mji wa dhambi. (rejea kitabu na filamu ya ‘Safari ya Msafiri’)
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni