Jumatatu, 30 Septemba 2013

Safu ya James Kalekwa: Umejenga Juu ya Mwamba au Mchanga? - Part II


James Kalekwa
Somo linaendelea....
Mwamba 1: Tawala nafsi yako kwa kuongoza milango yako ya fahamu.
Mithali 4:23
"Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima."
Ili uweze kusaidika juu ya habari ya nafsi ni muhimu sana kutambua na kukumbuka siku zote mwanadamu ni nani, wewe ni nani au ni kiumbe wa namna gani. Wewe niroho yenye nafsi inayoishi ndani ya mwili. Rejea kitabu cha Mwanzo 2:7, " BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai." Ambapo utaona mwanadamu ni muunganiko wa mavumbi ya ardhi, pumzi ya uhai na nafsi hai… Kwa msingi huo basi mavumbi ndiyo mwili, pumzi ya uhai ni roho na nafsi hai ni nafsi!www.hakileo.blogspot.com

Ukienda ndani ya neno la Mungu utakuta lile eneo la nafsi linazungumziwa kwa lugha au tafsiri tofauti tofauti kwa maana ileile. Kuna nyakati Biblia inatumia neno “moyo”, “nafsi”, “ufahamu”, “roho” kuelezea eneo moja tu la mwanadamu nalo ni nafsi. Kwasababu hiyo nakuomba ufungue macho yako kuyatazama maandiko kwa maana pana zaidi. Hebu tazama mstari huo kwa tafsiri za kiingereza: “Guard your heart above all else for it determines the course of your life." (NLT)


"Linda moyo wako zaidi ya vitu vyote kwasababu moyo wako ndiyo huamua mwenendo/mtiririko wa maisha yako."


"keep your heart with all diligence, for out of it springs out the issues of life." (KJV)


"Linda moyo wako kwa umakini mkubwa sana ,kwasababu moyo wako hububujisha mambo yahusianayo na maisha."


Kimsingi tafsiri zote zinatuelekeza kwenye uelewa kwamba maisha ya mwanadamu huamuliwa na moyo wake, mwenendo/mtiririko wa maisha hujengwa ndani ya moyo, chemchemi/chanzo cha maisha ya mwanadamu ni moyo! Natamani uone kwa ukubwa ambao mwandishi wa Mithali anaukusudia uuone… Ya kwamba chochote kinachotokea kwenye maisha yako, kimetokea moyoni mwako. Yaani kama moyo wako ni kiwanda na maisha yako ni bidhaa itokayo ndani ya kiwanda hicho na kwa uelewa huo basi, ni dhahiri ya kwamba kama hupendi bidhaa fulani usikurupuke kuiangamiza bidhaa hiyo kwasababu utakuwa umetatua tatizo kwa muda (immediate solution), bali unapaswa kudhibiti uzalishaji unaofanywa kiwandani. Au kama hupendi mazao yaliyomo gharani mwako, tafadhali usiyachome mazao hayo kwasababu utakuwa unatatua kwa muda, bali chukua hatua ya kudhibiti shughuli za shamba… Mungu akusaidie sana uelewe hapa!


Kwakuwa moyo ni sehemu muhimu kiasi hiki, basi tunapaswa kujua bayana na kwa uhakika tunaposema moyo tunamaanisha nini hasa ili tusijikute tunazungumza mambo tusiyoyajua “vague”…


Ukishauelewa moyo basi umepata mtaji wa ushindi! Kila mara ninapozungumza na vijana wenzangu huwa napenda kuwapa tahadhari ya kwamba moyo wa mwanadamu, huu unaozungumwa hapa si ule wa kwenye masomo ya sayansi hasa somo la Baiolojia….


Ninachofundisha hapa ni zaidi ya ule moyo wenye kazi ya kusambaza damu mwilini, kwasababu moyo usambazao damu umeumbwa kwa damu na nyama, yaani huo ni sehemu ya mwili na kwa uelewa nilioujenga kwako ni kwamba mwili ni mavumbi ya ardhi. Si kazi ngumu sana kung’amua kwamba moyo usambazao damu mwilini nao ni nyama (ni mwili) kwasababu baada ya roho kutoka, mtu kufariki, mavumbi (mwili) hurudi mavumbini… na moyo huo wa kwenye somo la Baiolojia huwa sehemu ya virudivyo mavumbini.


Kwahiyo kwa kutazama kuwa mwanadamu ni roho yenye nafsi inayoishi ndani ya mwili….uwe na uhakika Biblia inaposema "moyo" katika andiko hili haimaanishi moyo wa nyama na haimaanishi roho bali inamaanisha nafsi. Kwahiyo unapojifunza katika eneo hili naomba ubebe mtazamo wa nafsi ili uelewe vizuri zaidi.


Neno la Mungu linatanabaisha kuwa moyo/nafsi ndiyo huamua mwenendo wa maisha yetu na hububujisha mambo yahusianayo na maisha yetu kwa tafsiri nyepesi ni kwamba jinsi ulivyo ndivyo ulivyoamua kuwa; na uamuzi huo umefanyika ndani ya nafsi yako Mithali 23:7a,"Maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo." Hakuna mtu anapaswa kulaumiwa bali ndivyo ulivyoamua.Basi kama nafsi ni sehemu ya muhimu kiasi hicho, tunawajibu mkubwa sana kulinda sana nafsi zetu.


Hebu tuitazamae nafsi kwa mfano wa hazina…. Naomba uyaelekeze mawazo yako kwenye maisha ya kawaida kabisa, maisha ya kila siku. Ninaamini kwamba umeshawahi kusikia ama wewe au mtu anayekuhusu ni mtumiaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu ya mkononi. Kwa hapa Tanzania kuna huduma ya M-Pesa, Z Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa…


Kwa mfano huo basi, hebu mfikirie mtu ambaye hufunga safari kwenda kutoa pesa (kwa mtoa huduma) wakati anajua fika ya kwamba hana akiba/salio kwenye akaunti yake. Huyo ni sawa na mkulima ambaye wakati wa msimu wa mavuno unapofika yeye hufunga safari kwenda shambani ili akaanze shughuli ya kuvuna wakati anafahamu wazi ya kwamba hakuna siku ambayo aliwahi kuweka mbengu ndani ya shamba hilo… Inawezekanaje kuvuna wakati hujapanda? Kwa lugha ya kiingereza wanasema “you can not give what you do not have.”.


Ni ukosefu wa akili timamu ndiyo utamwongoza mtu kwenda kutoa pesa kwenye akaunti ambayo haina pesa (na muhusika hajawahi kuongeza pesa); ni upumbavu kwenda kuvuna kwenye shamba ambalo hujawahi kupanda mbegu yoyote.


Nimetumia mifano hiyo kukuleta kwenye dhana moja ya Muhimu sana ya kwamba kabla ya kutoa pesa kwenye akaunti unapaswa kuweka pesa; kabla ya kuvuna unapaswa kupanda mbegu. Kama basi inaonekana ni hekima kwa mkulima na mtumiaji wa huduma za pesa kwenye simu ya mkononi… ni hekima zaidi kwa mtumiaji wa moyo, mtumiaji wa nafsi ambaye ni wewe. Kabla hujavuna au hujatoa chochote kutoka kwenye nafsi yako, ni wajibu wako kuweka kitu.



Somo litaendelea Jumatatu Ijayo....




Mafundisho haya yameandaliwa na James Kalekwa
Mwanataaluma, Mwandishi wa vitabu, na Mwalimu wa Neno la Mungu
+255 714 762 669
+255 754 917 764
jameskalekwa@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni