Ijumaa, 20 Septemba 2013

KESHO ILIYOCHELEWESHWA


Mchungaji Josephat Gwajima.
Utangulizi:

Hii ni sehemu ya pili ya somo la hatua iliyocheleweshwa. Ni muhimu kujua kuwa Mungu ni Mungu wa makusudi na hakuna kitu anachofanya pasipo kusudi. Mbele za Mungu; Maisha ya mtu hayaanzi tumboni mwa mama yake bali yanaanza kabla ya mtu kuwa tumboni yaani Mungu huyaona maisha ya mtu kabla ya kuwa tumboni. Kimsingi, Mungu anajua kesho ya mtu kabla haijafika; katika ulimwengu wa roho kusudi la maisha ya mtu laweza kuonekana.

Kwa kuwa shetani ni roho anaweza kuona kesho ya mtu na pia aweza kuichelewesha; leo tunaangalia watu waliowahi kucheleweshwa katika Biblia.

Mchungaji aliyecheleweshwa katika Biblia:
Luka 8:26-39; “…akihubiri katika mji wote” tuangalie pia, habari hiyo katika kitabu cha Marko 5:18-20 “…akaenda kuhubiri katika Dekapoli” maana ya neno Dekapoli, ni “miji kumi” yaani tafsiri ya deka ni kumi, polis ni mji. Kumbe huyu aliyekuwa ameponywa akawa mhubiri katika miji kumi. Na ndio maana baadaye Yesu naye alienda kuhubiri Dekapili kwasababu alishamtanguliza mtu huyo kule, Marko 7:31. Inawezekana kabisa kuwa Yesu alikuwa anaenda Dekapoli kumtembelea huyo Mchungaji wa huko.

Mambo yote ambayo Mchungaji huyu aliyafanya yalikuwa yamecheleweshwa kwa zaidi ya miaka kumi. Ukisoma katika Marko 5:1-8; tunaona Mchungaji huyu alihamishwa na shetani kutoka sehemu alipokuwa anaishi na kuishi makaburini. Pia tunaona kuwa mtu huyu ambaye alikuwa na huduma ya uchungaji na uwezo wa kuhubiri ndani yake alitupiwa mashetani ili asiweze kumtumikia BWANA. Katika hili tunapata picha hii kuwa kuna uwezekano wa mtu ambaye Mungu alimpangia kuwa ama mchungaji, mfanyabiashara maarufu, mwimbaji au kiongozi; kucheleweshwa na shetani ili asiifikie hatma yake kwa wakati sahihi. Pepo wabaya wanaweza kumchelewesha mtu asifikie kusudi ambalo Mungu amemwekea mtu. Ndio maana ukifuatilia maisha ya watumishi wa Mungu wengi walianza tangu wakiwa na umri mdogo.

Kesho Iliyocheweshwa:
Kama tulivyomuona huyo mhubiri alivyocheleweshwa; vivyohivyo maisha ya watu wengi yamecheleweshwa ili wasiishi maisha ambayo BWANA aliwawekea wayaishi. Mashetani wanaweza kuchelewesha hatma njema ya maisha ya mtu. Unaweza kucheleweshewa utajiri, watoto, ndoa au kazi; na ndio maana Yesu baada ya kumfungua yule aliyekuwa na pepo wachafu hakutaka ajiunge naye bali akamwambia aende akahubiri injili Dekapoli. Kumbe tangu mwanzo Mungu alimwekea kusudi la kuwa mhubiri ndani yake.

Unaweza ukajiuliza; kwanini shetani anaendelea kukufuatilia ingawa umeshaokoka? Jibu ni kuwa, una kitu kikubwa cha Mungu ndani yako; hivyo anachoweza kufanya ni kukuchelewesha usikifikie na kwa njia hii shetani ameteka maisha ya watu wengi.

Mwanamke tajiri aliyecheleweshwa:
Jina Mariamu Magdalene limetajwa mara nyingi katika Biblia, na huyu ndiye aliyekuwa wa kwanza kukutana na Yesu baada ya kukufuka. Mwanamke huyu ndiye aliyekwenda kuwapasha habari mitume kuwa Yesu Kristo amefufuka. Tunafahamu kuwa alikuwa tajiri kwenye kitabu cha Luka 8:1-3 “…waliokuwa wakimhudumia Yesu kwa mali zao” inawezekana mtu, alishapewa neema ya kupata utajiri tangu alipoumbwa; lakini pepo wabaya ambao mtu huyo umetumiwa wanaweza kuchelewesha utajiri huo. Marko 15:40-41, Mariamu Magdalene alipotolewa pepo wabaya akapata utajiri na kwa utajiri huo akamtumikia Mungu.

Marko 16:1-8; Mariamu Magdalene ndiye aliyeendelea kumhudumia Yesu kwa fedha baada ya kutolewa pepo saba. Kumbe inawezekana ulipangiwa uwe tajiri wa kuwezesha kazi ya Mungu au wa kuwasaidia watu lakini shetani amekuchelesha na kukufanya uwe maskini.

Yesu aweza kukuokoa:
Ni kweli kuwa kuna watu wamecheleweshwa kimasomo, kimaendeleo, kiajira au kimahusiano. Na wengine wanaishi kwenye matatizo kwasababu ya kucheleweshewa kesho yao lakini ni muhimu kujua kuwa Yesu Kristo aweza kukuokoa kutoka katika kesho iliyocheleweshwa na kukuweka huru. Kama vile alivyomwokoa Mariamu Magdalene ndivyo atakavyokuokoa nawe. Uwe huru katika Jina la Yesu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni