Mfano wa mtu aliyejinyonga©pconormanning
Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
Leo, tunaendelea kujifunza Biblia yetu kwa kuzidi kukichambua Kitabu cha MATHAYO. Leo, tutajifunza kwa undani, MATHAYO 27:1-26. Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya KUJINYONGA KWA YUDA. Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vitano:-
(1) KUPELEKWA KWA YESU MBELE YA PILATO (MST 1-2)
(2) KUJUTA NA KUTUBU KWA YUDA (MST 3-5)
(3) KUJINYONGA KWA YUDA (MST 5)
(4) KONDE LA DAMU AU KONDE LA MFINYANZI (MST 6-10)
(5) YESU MBELE YA KITI CHA HUKUMU (MST 11-26)
(1) KUPELEKWA KWA YESU MBELE YA PILATO (MST 1-2)
Katika kipindi chote cha usiku kama tulivyoona katika MATHAYO 26:57-66, Yesu aliletwa katika baraza la wakuu wa makuhani, waandishi na wazee. Mahali hapa, walitafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu na wakatoa hukumu ya kumuua. Hata hivyo, baraza hili, halikuwa na uwezo wa kisheria wa kutoa hukumu ya kifo kwa mtu, kama jinsi Mahakama ya Mwanzo katika nchi yetu isivyokuwa na uwezo huo. Uyahudi yote ilikuwa chini ya utawala wa Kaisari wa Rumi. Kaisari huyu, ndiye aliyekuwa Mtawala Mkuu wa sehemu kubwa ya dunia ya wakati huo. Chini yake, walikuwepo Wakuu wengine wa Majimbo au Mikoa mbalimbali. Pontio Pilato, alikuwa Mkuu wa Jimbo au Mkoa wa Uyahudi ambaye cheo chake katika Biblia kinajulikana kwa jina la LIWALI (MST 2; LUKA 3:1). Huyu ndiye aliyekuwa na uwezo wa kisheria wa kutoa hukumu ya kifo.
Hivyo, mapema asubuhi, wakuu wa makuhani walimfunga Yesu, wakamchukua na kumpeleka kwa Liwali wa Uyahudi, Pontio Pilato. Kutoka kwa Kayafa Kuhani Mkuu mpaka kwa Pilato ilikuwa karibu MAILI MOJA. Mikono ya Yesu ilifungwa kwa kamba ikiwa nyuma mgongoni kama ilivyokuwa desturi ya wafungwa wa nyakati zile. Kamba hiyo ilifungwa kiunoni pia. Akiwa ametemewa mate na kupigwa makonde na kufungwa hivyo, aliongozwa barabarani mapema asubuhi, kwa maili moja, na kundi kubwa la watu wakiwa nyuma yake wakimdhihaki. Pilato hakuwa Myahudi, bali Mataifa. Hapa tunaona Mataifa na Wayahudi wakishirikiana katika dhambi ya kumhukumu Yesu, ili Yesu awe Mwokozi wa Mataifa na Wayahudi pia.
(2) KUJUTA NA KUTUBU KWA YUDA (MST 3-5)
Yuda alipoona ya kuwa Yesu amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akasema, NALIKOSA. Yuda, hakutegemea kwamba matokeo ya kumsaliti Yesu yangekuwa hivi. Alidhani Yesu angetoka mikononi mwao baada ya kukamatwa kama alivyofanya awali (YOHANA 8:59; 10:39; LUKA 4:28-30), hivyo akajua kwamba angekuwa amepata zile pesa, na tena Yesu asingekuwa amedhurika kwa lolote. Baada ya kuona sasa kwamba Yesu hapa amekubali kuuawa na sasa anafungwa na kupelekwa kwa Pilato, ndipo akajua kwamba kweli Yesu anauawa, NIPO AKAJUTA. Dhambi huja kwetu namna hiyo. Unapofanya dhambi, dhambi huwa tamu kama asali kinywani, na mtu huwa hategemei kwamba litatokea lolote baya, hata akionywa, huona wanaomuonya kwamba ni wapumbavu.
Matokeo mabaya ya dhambi yanapoonekana kwa mtu, huwa siyo matamu tena. Kile kilichokuwa kitamu kinywani, kinabadilika tumboni, kinakuwa ni nyongo za majoka (AYUBU 20:12-14). Ndipo mtu anapojuta. Mtu anapofanya uasherati au uzinzi anajiona bingwa, akipata mimba asiyotegemea au akipata UKIMWI, NDIPO anapojaa majuto. Vivyo hivyo kwa mwizi, mlevi, mvuta sigara au bangi au anayekula madawa ya kulevya, mpokea rushwa n.k. Yuda, hapa alijuta, akasema, “Nimekosa” na akafanya malipizo kwa kurudisha fedha zisizo halali, hata hivyo hakuwa na toba iliomletea wokovu! Yako maneno mengi ya Kiyunani yanayozungumzia toba . Toba ya Yuda inaitwa “METAMELOMA”. Hii siyo toba ya kweli iletayo wokovu. Ni toba inayotokana na majuto ya MATOKEO ya dhambi na siyo majuto ya CHANZO cha matokeo hayo ya dhambi.
Mtu mwenye toba ya namna hii huwa hana nia ya kuacha dhambi hiyo. Hujuta binafsi tu, wala hamwendei Mungu na kusema “Nimekosa mbele ya mbingu na nchi” kama mwana mpotevu. Yuda aliwaendea watu wa nchi tu na kuwaambia “Nimekosa”, hakumwendea Mungu kama alivyofanya Petrio alipomkana Yesu. Toba halisi inayoleta wokovu inaitwa “METANOIA”. Mtu hujuta binafsi na kuchukia dhambi ambayo ndicho chanzo cha matokeo yake ya dhambi. Kisha humwendea Mungu wa mbingu na kutubu kwake, kisha huwa tayari kuacha kabisa dhambi ZOTE kuanzia wakati huo na kutenda yanayompendeza Mungu, na pia kuwa tayari kufanya malipizo au marekebisho ya kosa lake kwa WATU wa nchi kwa kuwaambia nao, “Nimekosa”. Yuda pamoja na “toba” yake hakumaanisha kuacha dhambi zote, kwa jinsi ambavyo alivyokwenda kujinyonga baada ya “toba” hiyo.
(3) KUJINYONGA KWA YUDA (MST 5)
KUJIUA kwa namna yoyote, ni sawa na dhambi ya KUUA, na hukumu yake ni kutupwa katika moto wa milele, mara tu baada ya kujiua huko. Mtu anapojiua kwa kujinyonga, kunywa sumu, kujitupa chini kutoka orofani, kujaribu kutoa mimba, kunywa vidonge vingi n.k; mtu wa namna hii hujipeleka mwenyewe moja kwa moja Jehanum. Roho zote ni mali ya Mungu (EZEKIELI 18:4). Mwanadamu hana ruhusa ya kuitoa roho yake au ya mtu mwingine. Kufanya hivyo ni kufanya dhambi. Yuda alijinyonga kwa sababu ya kukubali kwenda mahali pa peke yake, akiwa na fadhaiko kubwa moyoni. Fadhaiko kubwa la moyo linatokana na sababu mbalimbali, huwafanya wanadamu wengi kujiua (ANGALIA MIFANO YA KUJIUA: 1 SAMWELI 31:2-6; 2 SAMWELI 17:23; 1 WAFALME 16:18). Yuda aliposhikwa na fadhaiko hili, badala ya kwenda kwa mitume wenzake 11, aliamua kwenda mahali pa peke yake bondeni. Hili lilikuwa kosa kubwa, lililomsababisha ajinyonge. Tunapopatwa na fadhaiko, ni vema kuwa pamoja na watu wa Mungu ambao “watachukuliana mizigo” pamoja nasi.
Yuda angekwenda kwa mitume wenzake asingejinyonga. Mtu akiwa peke yake katika fadhaiko, Shetani humpa mawazo ya kujiua na akishindwa kumpinga, basi hujiua kama Yuda. Kufa kwa Yuda kulikuwa kwa kuhuzunisha. Alikwenda bondeni halafu akapanda juu sana na kujinyonga huko. Kisha mwili wake ukadondoka chini bondeni, kwa kasi sana ukitanguliza kichwa, tumbo lake lilipopiga chini, matumbo yake yote yalitoka nje kama kuku aliyekanyagwa na gari! (MATENDO 1:16-19). Hatupaswi kufikiri kama Yuda kwamba kuna dhambi kubwa ambayo hatuwezi kusamehewa na Mungu au kwamba hatuwezi kukubalika tena kwa watu wa Mungu Kanisani tukifanya hili au lile (ISAYA 1:18; LUKA 15:3-32).
(4) KONDE LA DAMU AU KONDE LA MFINYANZI (MST 47)
Wakuu wa Makuhani katika unafiki wao walikataa fedha alizozirudisha Yuda wakasema hawawezi kuziweka kwenye sanduku la sadaka, ni kima cha damu, yaani fedha iliyopatikana kwa kumwaga damu! Wakaona kuwa ni sawa na ujira wa kahaba au mbwa (mwanamume anayefanywa mambo ya uasherati) ambao hauruhusiwi kupokewa kama sadaka – KUMBUKUMBU 23:17-18. Mbona fedha hizo hizo walizitoa wao kutoka kwenye sanduku ya sadaka? Wakanunua konde (shamba) la mtu mmoja mfinyanzi na kulifanya mahali pa kuzikia wageni (watu wasio Wayahudi) waliokuja kuabudu Yerusalemu! Wayahudi waliwatenga Mataifa hata walipokuwa maiti! Walijiona watakatifu kuliko wao (ISAYA 65:5). Lakini kwa kufanya hivyo pia mataifa walinunuliwa kwa damu ya Yesu!
(5) YESU MBELE YA KITI CHA HUKUMU (MST 11-26)
Yesu alikubali kwamba ni Mfalme wa Wayahudi, jambo ambalo lilitafsiriwa tofauti na Wayahudi, kwamba, yuko kinyume na Kaisari. Hata hivyo, pamoja na ushahidi wote wa uongo juu ya Yesu, mashahidi wengi walithibitisha kwamba Yesu hakuwa na hatia yoyote. Mashahidi hao ni (a) Pilato (LUKA 23:13-14), (b) Herode (LUKA 23:15), (c) Mkewe Pilato (MATHAYO 27:19), (d) Yuda (MATHAYO 27:3), (e) Wakuu wa Makuhani na baraza lao (MATHAYO 26:59-60). Bila dhambi, Yesu alisimama mbele ya kiti cha hukumu ili amwaminiye asihukumiwe tena (YOHANA 3:18; 5:24). Baraba aliwekwa gerezani kwa makosa matatu: (a) FITINA (LUKA 23:19) – Fitina inayotajwa hapa, ni kuchochea watu ili waiasi serikali au UHAINI (b) UUAJI (LUKA 23:19), (c) UNYANG’ANYI (YOHANA 18:40). Ndiyo maana alikuwa mfungwa “mashuhuri” mwenye makosa nyeti ambayo hukumu yake ya dhahiri ni kifo. Hata hivyo ndiye aliyefunguliwa na Yesu kufa badala yake, kinyume kabisa na matarajio. Baraba alituwakilisha wanadamu wote. Yesu alikufa kwa niaba yetu, ili kila amwaminiye apate uzima wa milele bure, kwa neema, bila kustahili kabisa. Baraba aliokolewa kutoka katika hukumu ya mauti kwa neema! Sisi nasi kwa jinsi hiyo hiyo, tunaokolewa kwa neema kwa njia ya imani tu bila matendo yoyote ya kutustahilisha (WAEFESO 2:8-9).
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni