Jumatatu, 14 Aprili 2014

MAHOJIANO MAALUM KUHUSU MADAI DHIDI YA OPERESHENI MILIKISHA KUWA KIBIASHARA ZAIDI (2)

Msomaji mpendwa, toleo lililopita tulichapisha sehemu ya kwanza ya mahojiano maalum kuhusu kampeni za Askofu Gamnaywa za OPERESHENI MILIKISHA ambazo zimetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa zimekaa kibiashara zaidi badala ya Injili ya Yesu. Pamoja na majibu yaliyotolewa na Askofu Gamanywa bado yalijitokeza maswali ya nyongeza ambayo imebidi tumwombe ayatolee ufafanuzi kwa manufaa ya wasomaji wetu:

SWALI
Askofu Gamanywa, katika sehemu ya kwanza ya mahojiano yetu ulijieleza vizuri sana kiasi ambacho majibu yako yalijitosheresha kwa wale ambao waliosoma toleo lililopita. Lakini kwa leo tunapenda kumalizia mahojiano haya kwa maswali ya nyongeza. La kwanza kabisa ni je! Kwa hisia zako unadhani sababu ipi kubwa inayowasukuma baadhi ya watumishi kuwa na mtazamo hasi dhidi ya OPERESHENI MILIKISHA kwa kuitafsiri kuwa imekaa kibiashara?
MAJIBU
Kutokana na uzoefu wangu wa miaka 30 kwenye huduma za kikanisa, ninaifahamu saaana kuwepo nadharia kongwe yenye “kupinga na kuzuia maaskofu watumishi wa injili wa aina yangu kufanya shughuli yoyote ya uzalishaji wa kiuchumi”! Nadharia hii inawataka watumishi wa Injili kuishi kwa kutegemea miujiza ya Mungu kama Eliya; au kuishi kwa sadaka na zaka wa waumini peke yake.

Ndiyo maana, kwa mujibu wa nadharia hii, kigezo pekee cha “wito na utumishi kwa Mungu”ni huyu aliyeitwa lazima aache kufanya kazi na kujitenga kabisa na shughuli zote za kiuchumi; na kujikita katika kazi ya kuhubiri na kufundisha Biblia peke yake. Na pale ambapo mtumishi wa aina hii anapoonekana katika shughuli za kiuchumi mara hutafsiriwa kuwa “ameacha wito wake”, au “amekiuka maadili ya utumishi” au “amekuwa mfanya biashara”, na kisha kumtangaza kuwa ni “mtafuta fedha badala ya kuokoka roho za watu”!

Pamoja na haya yote, tukilisoma kwa makini Agano Jipya katika Biblia, tunakuta kwamba hakuna aina moja ya wito na mtindo mmoja wa utumishi wa Injili. Japokuwa Injili ni moja, lakini kila anayeitwa “hupewa ufunuo maalum wa kuhubiria watu maalum ambao ndio walengwa wake, na kisha hufunuliwa mikakati ya kiuchumi ya kuifikisha injili kwa wahusika.

Wakati jamii kubwa ya watumishi wanaishi kwa nadharia hii; miye wito na utendaji wangu tangu mwanzo ulikuwa tofauti. Hii ni kutokana na aina ya walengwa niliofunuliwa kuwafikia katika kizazi changu. Aidha, nilipewa ujumbe wa kuwasilisha kwa mujibu wa wito wangu na aina ya walengwa wangu.

Hata hii Kampeni ya OPERESHENI MILIKISHA, haya kama inatangazwa hadharani kwa watu wote wanaosikia; bado nayo si kwa ajili watu wote. Ina walengwa wake ambao Mungu amewakusudia kuwafikia kwa ufunuo huu. Sasa kama kuna watumishi ambao wanapata shida na hawaoni mantiki katika kampeni hii; maana yake wao “si walengwa” na wala “si washiriki” pamoja nami katika wito huu; kwa hiyo wasisumbuke kufuatilia wito ambao hauwahusu, maana watakuwa wanapoteza muda wao bure.

SWALI
Askofu Gamanywa, wanaokutuhumu nao wanatumia kigezo cha maandiko wakisema Yesu Kristo aliwakataza mitume wake wahubiri Injili peke yake, tena wasibebe mikoba kwenye injili, na kwamba Mungu atawalisha huko huko huduma za Injili. Hata Mtume Paulo alisisitiza kwamba wahubiri wa Injili wanastahili kula madhabahuni katika huduma za Injili. Wewe umeitwa mfanyabiashara kwa kampeni za kumilikisha watu mali badala ya kumilikisha ufalme wa mbinguni. Unalisemeaje hili?


MAJIBU
Nina majibu ya upande wa pili wa sarafu kuhusu mifano ya maandiko na hao uliowataja. Ni kweli Bwana Yesu hapo mwanzo alipowatuma aliwakataza mitume wake kubeba mikoba na kwamba watalishwa na kuhudumiwa huko huko waendako. Lakini wanaoihukumu wamesahau kwamba Bwana Yesu huyo huyo alilitengua agizo lake la kwanza la kutokubeba mikoba na mtindo wa kutegemea kulishwa huko huko kama hapo awali. Tunasoma katika maandiko kwamba:

Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La! Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue. (LK. 22:35, 36)

Je unasikia maneno ya Yesu akisema: “Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue; na mkoba vivyo hivyo…”? Huoni kwamba agizo la kwanza lilikuwa na ukomo wa muda na ndio maana Yesu akatoa agizo jingine? Huoni kwamba kuendelea kushikilia agizo la kwanza ni sawa na kwenda kinyume na agizo hili la pili?

Haya tukirejea kwa Mtume Paulo aliyesema kwamba, kila mhubiri wa Injili anastahili kula katika Injili, yeye mwenyewe alikuwa “mfanyabiashara” mkubwa wa kushona mahema na sehemu kubwa ya utumishi wake alifanya kazi kwa mikono yake mwenyewe:

Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea. (MDO 20:33-35)

Kana kwamba hii haikutosha, Paulo aliweka bayana kwamba kila alipokwenda na timu yake, alihakikisha kwamba hawawi mzigo kwa wale wanaowapelekea Injili, lakini pia walilazimika kufanya biashara ili kuwa kielelzo kwa wafuasi hao wachanga:

Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yeyote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. (2 THE. 3:7-10)

Bila shaka unayasikia maneno haya ya “..hatukula chakula kwa mtu yeyote bure” maana yake walilipia kama vile tunavyolipia twendapo hotelini; haya anaongeza kusema; “…usiku na mchana tulitenda kazi.” Maana walikuwa katika shughuli za uzalishaji haswaa! Kisha Paulo anasema; “…ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yeyote..” maana yake hawakutaka kuwa mzigo wa mahitaji kwa mtu, na sababu ya pili anasema, “…lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate! Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwa kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi - basi, asile chakula.”

Kwa ushahidi huu wa maandiko, napenda kukuhakikisha kwamba kampeni za Operesheni Milikisha lazima ziongozwe kwa mimi mwenyewe “kuwaongoza watu kufanya kazi” kwa “kwa mimi mwenyewe kufanya kazi” na sio na “nadharia ya maneno tu kuhusu kufanya kazi” !

Tukimsoma Paulo vizuri tunamkuta yuko kila mahali, akitumia maneno “usiku na mchana” huku alihubiri:“Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi…” Mdo. 20:31; Lakini mara tunamkuta akisema tena “usiku na mchana akifanya kazi: “bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, (2 Thes.3:8)
Hii ina maana kwamba Paulo alifanya mambo yote! Kuna wakati alihubiri sana mfululizo na kuna wakati alifanya biashara sana lakini bado tunapata ushuhuda wa huduma zake za maombezi pale ilipoandikwa:
“Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.” (Mdo.19:11-12)
Unaona hapa mwandishi? Inaonesha waziwazi kwamba, kuna wakati alishindwa kuwafikia wagonjwa na walemavu na badala yake akawa akituma vitambaa wapelekewe wagonjwa huko huko waliko na uponyaji ukadhihirika wa wagonjwa.

Kwa hiyo, sio sahihi kwamba, kufanya shughuli za kiuchumi ni haramu katika huduma za Injili kama inavyodaiwa. Tena basi, kufanya shughuli za kiuchumi ni mfano bora wa kuigwa na waamini pale waonapo kiongozi yuko mstari wa mbele kuzalisha pamoja nao!
SWALI
Askofu Gamanywa, baadhi ya watumishi wamekwisha kutoa tahadhari juu yako kwamba kutaka kuwa na mali kwako kunapingana na maonyo ya Mtume Paulo kwa Timotheo yasemayo:
“Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatozaso wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.” (1 Tim.6:9-10) Askofu Huoni kwamba Kampeni zako za kumilikisha mali zinakinzana na maandiko haya?

MAJIBU
Duu! Mnajua jinsi ya kupindisha maandiko kwa namna ya ajabu sana! Hivi kweli, kama “kufanya kazi halali” na “shughuli za kiuchumi” kungekuwa tafsiri yake ati ndio “kutaka kuwa na mali kunakoangusha katika majaribu na tamaa zisizo na maana”; basi Paulo mwenyewe ndiye angelikuwa wa kwanza kutafsiriiwa kuwa kapotea na pia kawapoteza wafuasi wake aliokuwa akiwahimiza kufanya kazi kwa bidii.

Tatizo kubwa hapa ni uelewa mdogo wa kusoma na kutafsiri maandiko. Mahali ulipoanzia kunukuu maandiko na tafsiri uliyotoa vyote kwangu ni ushahidi kamili unaonidhihirishia baadhi ya hao waitwao watumishi jinsi ambavyo wanapindisha na kupotosha maana ya maandiko!

Wewe umenukuu kuanzia msitari wa 9 unaposema “…lakini hao watakao kuwa na mali…” wakati bado hujatafuta kujua sifa zao ni akina nani "hao watakao kuwa na mali" tayari “unanibandika mimi kuwa mimi ndiye mlengwa wa maandiko hayo na kwamba ninataka kuwa na mali”

Lakini Paulo kupitia maandiko hayo alikuwa na aina ya watu aliowalenga! Tena kabla ya kuandika uliyoyanukuu wewe, tayari Paulo alikwisha kutaja sifa zao pale juu kwenye msitari wa 5 unaosema:

“…watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida…” (1 Tim. 6:5)

Unaona? Hawa “Wanaotaka kuwa na mali” wameainishwa kwa sifa tatu: Kwanza, “walioharibika akili zao”; Pili, “walioikosa kweli”, Tatu, “wanaodhani kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.”! Je na mimi unaniona nimeangukia katika sifa hizi?

Je unataka nikwambie hawa ni akina nani? Hii ni jamii ya watu ambao wameingia katika imani; wakaijua kweli, lakini kwa sababu ya tamaa ya fedha zisizo na jasho; wakaona mahali pazuri pa kujipatia utajiri ni kupitia madhabahu za huduma za injili.

Kwa tamaa hizi wakapoteza uadilifu na kuharibika akili zao na kujikita katika kujitajirisha kupitia kukusanya fedha kutoka kwa watu wanaowadhania ni wacha Mungu. Hawa ndio Paulo aliokuwa akiwazungumuzia kwenye maandiko yako ya awali kwamba, “watakao kuwa na mali” hujikuta wameharibikiwa kwa sababu wameingiwa na roho ya “kupenda fedha”!

OPERESHENI MILIKISHA imelenga sio kunitajirisha mimi binafsi, na wala sitafuti utajiri binafsi kupitia MVIMAUTA. Sitafuti kutajirika kupitia sadaka na matoleo ya waamini, badala yake miye mwenyewe natumia vipawa na uwezo alionijalia Mungu kuinua viwango vya uchumi vya wale ninaowaongoza! Mwenye kutafuta kujitajirisha kibinafsi hapotezi muda wake kuhangaika na maisha ya wengine, labda pale ambapo atanufaika kupitia kwao.
Itaendelea toleo lijalo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni