Jumanne, 12 Novemba 2013

MAKALA: KUMBE SHETANI NAE ANA MASHABIKI WA KUTOSHA


©Desktop Nexus
Weekend hii ilikuwa njema na chungu kwa baadhi ya wadau wa soka. Nazungumza hivyo nikitazama matokeo ya mechi la ligi kuu kadhaa kuanzia ya nyumbani ambayo pazia la msimu wa kwanza limehitimishwa, huku pia kwa Uingereza, ligi yenye wadau wengi duniani - ikikutanisha Manchester United na Arsenal, ambapo matokeo, ni ushindi kwa Man U, goli moja kwa bila. Si nia yangu kujadili matokeo wala kuwakumbusha baadhi ya watu machungu, nia haswa ni kutazama ushabiki wetu na majina ya hizi timu.


Timu zote zina historia ya namna zilivyoanzishwa, na kila jina la timu lina maana yake, mfano - Mbeya City, hapa moja kwa moja utajua hii timu ya wapi, ama ukisema Manchester City, pia ni rahisi kujua ni timu ya upande gani. Kuachia hayo, Karibu timu zote zina majina yake ya kando, tuite a.k.a - ni majina ambayo aidha huonyesha umwamba/ukali wa timu hizo, na mashabki kupata nafasi ya kutambiana mtaani.

Arsenal wao wanajiita The Gunners, na hapa nyumbani tunawaita washika bunduki, jina lao linaendana nao kwa kuwa maana ya neno arsenal, ni ghala la kuhifadhia silaha. Ukitazama Chelsea, wao wanajiita The Blues ama The Pensioners - hii inatokana na jezi zao za nyumbani kuwa na rangi ya bluu. Liverpool wao wanajiita The Reds, na Manchester United, wao wanajiita Red Devils, yaani Mashetani Wekundu. Hapo ndio chanzo cha mjadala wetu wa wazi.

Machester United ni klabu yenye mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa soka duniani, na mfao kwa vilabu vingi, huku chipukizi kadhaa wakiota kuichezea, jambo ambalo linawafanya wajitume kila wanapoiona inacheza.



©Devian Art
Lakini, kinachonikereketa ni wao kujiita Red Devils, na alama ya kikaragosi chenye mapembe na silaha (jambo linaloonyesha kuwa wako tayari kwa mpambano muda wowote) na hapo bado wana wa Mungu tunawashangilia saaaana, yaani tunaonekana kukoshwa na mbwembwe na ubabe wa mfumo huo.

Sawa, utasema kuwa huu ni mchezo tu, na hauna maana yoyote, lakini hivi ilikuwa ina maana gani kwenye Biblia ilipoandika kwenyeUfunuo kuhusu chapa? Rejea Ufunuo 13: 16-18 na ujaribu kuonanisha - namba za kibinadamu, 666. Hivi na hapa hakuna jambo nyuma yake? Hili ni swali ambalo nitahitaji msaada na ufafanuzi wako. Maana kwa hakika kila mtu anajua kuwa shetani ana mbinu nyingi, hivi ni kweli hii sio mbinu yake mojawapo? Au unadhani huwa anasema labda 'Hawa watu wanashangilia wakati sio mimi, yule ni shetani mwekundu tu wa kimichezo'. Huenda, ila ninachofahamu ni kuwa shetani ni 'opportunist' na atatumia nafasi yoyote hasahasa kwenye udhaifu wako (weakest link) ili akupate tu.



Man Utd, wana msemo wao, ambao kwenye mitandao pia ni maarufu hasahasa kutokana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasaliano na kuongezeka kwa maarifa, Glory Glory Man Utd, kwenye mitandao utakuta #GGMU. Kwa kuwa ukisema The Red Devils - ni sawasawa na kama umesema Manchester United, je huo utukufu ambao watu wanautaja hapo unaenda kwa nani, shetani mwekundu? Nauliza tu. Si ajabu huko aliko anafurahia kila mara anapotajwa na utukufu kuelekezwa kwake. Hebu na tutafakari kwa kina.

Glory glory red devils? Kweli ndio tumeendelea kiasi cha kuanza kumsifu na kumuabudu shetani? ama pengine labda ni ushamba wangu tu, nahitaji ufafanuzi kutoka kwako unalitizama jambo hili kwa namna gani, pengine siko peke yangu, ama pengine hauko peke yako ambaye pia una shaka na hili jambo, basi jambo lenye mashaka mashaka na lijadiliwe, vinginevyo ni kama tunaendelea kushangilia kajitu kaliko na mkia, mapembe, na kana silaha mfano wa kuchomea vitu.

Huu ni mtazamo wangu kwenye hili, ningependa pia kukusikia, tuandikie maoni yako hapo chini, na mjadala uendelee.


Elie John,
GK Staff Writer

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni