Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO: AMRI MPYA
L
eo, tena, Bwana ametupa neema ya kuendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA, katika Biblia zetu. Leo, tutatafakari YOHANA 13:33-38, na YOHANA 14:1-3. Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza kuhusu “AMRI MPYA“. Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele tisa:-
(1) ENYI WATOTO WADOGO (MST. 33);
(2) BADO KITAMBO KIDOGO NIPO PAMOJA NANYI (MST. 33);
(3) MIMI NIENDAKO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33, 36-37);
(4) AMRI MPYA (MST. 34-35);
(5) KUUTOA UHAI KWA AJILI YA YESU (MST. 37-38);
(6) MSIFADHAIKE MIOYONI MWENU (MST. 1);
(7) MAKAO MENGI MBINGUNI (MST. 2);
(8) NAKWENDA KUWAANDALIA MAHALI (MST. 2);
(9) NITAKUJA TENA NIWAKARIBISHE (MST. 3).
(1) ENYI WATOTO WADOGO (MST. 33)
Hapa Yesu, alikuwa amekaa na mitume hawa, akiwafundisha kwa zaidi ya miaka mitatu. Alikuwa amewapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina, na kufufua watu (MATHAYO 10:1,8). Pamoja na yote haya, Yesu bado anaawaita “WATOTO WADOGO“. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu, kujifunza jambo la muhimu hapa. Hata kama sisi ni Mitume, Manabii, Wainjilisti, Wachungaji, Waalimu, Viongozi wa Zoni, Seksheni au Makanisa ya Nyumbani, hata kama tumepewa mafunuo au karama za namna ipi na tunatumiwa jinsi gani na ungu, ni muhimu kufahamu kwamba Yesu, bado anatuita “WATOTO WADOGO“. Ni watoto wadogo kwa msingi kwamba hatujajua lolote bado, kama itupasavyo kujua (1 WAKORINTHO 8:2); na tena pasipo Yesu Kristo, sisi hatuwezi kufanya neno lolote (YOHANA 15:5). Bdo wakati wote tunahitaji msaada kutoka kwake Yesu. Hatuna haja ya kuwa na kiburi wakati wowote ule. Kadri tunavyokumbuka wakati wote kwamba sisi ni “Watoto wadogo“, na kumtegemea Mungu katika kushinda kwetu, na kufanya lolote lile, ndivyo tunavyojiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutumiwa sana na Mungu.
(2) BADO KITAMBO KIDOGO NIPO PAMOJA NANYI (MST. 33)
Yesu hapa, anawaambia wanafunzi wake kwamba, bado kitambo au muda mchache, ataondoka na kufa na kuzikwa; kisha kufufuka na kupaa mbinguni. Anawaonya watumie vizuri muda waliobaki nao kwa kumwuliza maswai, kuhusiana na yale aliyowafundisha, au siyo, watamtafuta wasimwone. Kuna jambo la kujifunza hapa. Kila mmoja wetu hana budi kufahamu kwamba bado kitambo kidogo sana Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia (WAEBRANIA 10:37). Hivyo ni juu ya kila mmoja wetu, kuukomboa wakati, na kufanya mapenzi ya Bwana (WAEFESO 5:15-17); na siyo, atakuja kulinyakua Kanisa na kutukuta hatujajiandaa. Leo yuko pamoja nasi akitufundisha na kutuonya kila siku. Hatuna budi kuyazingatia maonyo yake na kuyafuata wakati bado neema hii haijaondoka kwetu.
(3) MIMI NIENDAKO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 3, 36-37)
Katika YOHANA 7:33-34; Yesu aliwaambvia Wayahudi kwamba hawawezi kwenda pale anapokwenda (mbinguni) kwa sababu walikuwa hawakubali kwamba Yeye ni Masihi na kuokoka. Sasa hapa tena, anawaambia wanafunzi wake. Kwa wanafunzi wake, anamaanisha kwamba, hawawezi kumfuata atakapokuwa anakwenda kuteswa na kisha kusulibishwa. Ndivyo ilivyokuwa, wanafunzi wote walimwacha na kukimbia (MATHAYO 26:56). Hata hivyo, Yesu alimwambia Petro kwamba atamfuata baadaye, akimaanisha kwamba yeye naye baadaye atasulibishwa (YOHANA 2:17-19). Ndivyo ilivyokuwa kulingana na historia ya Kanisa la Kwanza, Petro naye alisulibishwa. Hata hivyo, alikataa kusulibishwa kichwa juu miguu chini kama Bwana wake Yesu, akasulibishwa miguu juu kichwa chini.
(4) AMRI MPYA (MST. 34-35)
Yesu hapa, anatoa amri mpya kwa wanafunzi wake akisema, “Mpendane, kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo“. Mtu yeyote aliyeokoka, anatazamiwa kuitekeleza ami hii kwa kuwapenda wenzake waliokoka kama Yesu naye alivyoonyesha upendo huo. Upendo kwa watu wenzake waliokoka, ndiyo alama kuu inayomtambulisha mtu kwamba ameokoka. Kwa alama hii, mtu aliyeokoka, ATAJIJUA MWENYEWE kwamba ameokoka (1 YOHANA 3:14). Kwa alama hii pia, WATU WOTE WATAJUA kwamba sisi tumeokoka (YOHANA 13:35). Vivyo hivyo, kwa alama hii, MUNGU HUWAJUA watoto wake ( 1 YOHANA 3:10). Hatuwezi kudai kwamba tunampenda Mungu tusiyemowna, ikiwa hatuawezi kuwapenda ndugu zetu waliookoka ( 1 YOHANA 4:20). Kumwamini Yesu au kuokolewa, wakati wote huambaana na kuwapenda watu waliokokaka (1 YOHANA 3:25; 4:21). Yeyote yule anayedai kwamba ameokoka, lakini anawachukia ndugu zake waliookoka, huyu ni mwuaji kwa msingi uleule ambao Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake Habili (1 YOHANA 3:11-12, 15). Imetupasa kupendana sisi kwa sisi kama Yesu alivyotupenda sisi kwa kuzingatia yafuatayo:- (a) Yesu alijishughulisha na ugonjwa wa mkwewe Petro, mwanafunzi wake (MARKO 1:30-31). Sisi nasi kama kweli tumeokoka hatuna budi kuangaliana katika magonjwa na matatizo. (b) Yesu alijishughulisha na msiba wa wanafunzi wake Martha na Mariamu na kufadhaika pamoja nao juu ya kifo cha Lazaro (YOHANA 11:33-36), sisi nasi upendo wetu kwa wengine unapaswa kudhihirika katika misiba (c) Yesu aliwatembelea wanafunzi wake majumbani kwao (MARKO 1:29). Sisi nasi ikiwa kweli tumeokoka, imetupasa kutembeleana majumbani kwetu (d) Yesu alihusika kumsaidia mwanafunzi Petro alipokuwa ana tatizo la kifedha wakati yeye alikuwa ana uwezo wa kumsaidia (MATHAYO 17:27). Sisi nasi inatupasa kusaidiana katika matatizo ya kifedha, ikiwa kweli tumeokoka. Mtu akiwa na riziki ya dunia inampasa kumwangalia ndugu yake aliyeokoka asiyekuwa na riziki (1 YOHANA 3:17-19). (e) Yesu aliutoa uhai wake kwa ajili yetu, sisi nasi imetupasa kuutoa uhai wetu kwa ajili ya wenzetu waliookoka, katika kuwahudumia wanpokosa nauli hata kama sisi nasi tumebakiwa na kidogo tu, na kuwapa huduma nyingine kwa msingi huu (1 YOHANA 3:16). (f) Yesu aliwapenda na kuwajali wanafunzi wake kuliko wazazi na ndugu zake wa kimwili (MATHAYO 12:46-50). Sisi nasi hatuna budi kuwapenda watu wenzetu waliookoka katika mambo yote, KULIKO ndugu zetu wa kimwili. Ikiwa mtu anadai ameokoka, na hana upendo wa jinsi hii, madai yake si ya kweli.
(5) KUUTOA UHAI KWA AJILI YA YESU (MST. 37-38)
Watu tuliookoka, hatuna budi kuwa waaminifu katika imani ya Yesu hata ibidi kufa, kama alivyowaza Petro hapa. Siyo tu kupigwa na kuwekwa gereani, bali tuwe tayari hata kufa katika kuishindania imani (UFUNUO 2:10). Hatupaswi kuyahesabu maisha yetu kuwa kitu cha thamani kuliko wokovu wetu (MATENDO 20:24). Mitume walipigwa na kuaibishwa lakini hawakuahca wokovu (MATENDO 5:40-42; 16:19-23). Hata hivyo, tusijivunie akili au kutumainia nafsi zetu katika kutenda haya, bali tumtumaini Mungu mwenye kutupa neema ya kutuwezesha; ili tusije kuwa kama Petro aliyejigamba kisha akamkana Yesu mara tatu.
(6) MSIFADHAIKE MIOYONI MWENU (MST. 1)
Wanafunzi wa Yesu waliposikia Yesu akisema anawaacha kitambo kidogo, walifadhaika mioyoni mwao. Akawaambia, “Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi“. Hatupaswi kufadhaika mioyoni mwetu wala kuwa na woga, bali tumtegemee na kumwamini Yesu kwamba ana uwezo wa kutushindia katika magumu yoyote yanayotukabili (YOHANA 14:27).
(7) MAKAO MENGI MBINGUNI (MST. 2)
Neno la Kiyunani linalotafsiriwa hapa “Makao“, ni “MONE“. Neno linalotumika katika Biblia ya Kiingereza ya KJV, “MANSIONS“, lina maana inayoleta picha halisi ya Neno “MONE“, kuliko neno la Kiswahili “MAKAO“, “MANSION“, ni jumba kubwa la kifahari. Jumba la Meya wa Jiji la London, Uingereza (Lord Mayor of London), linaitwa “MANSION HOUSE“. Kila mtu aliyeokoka, ameandaliwa jumba kubwa la kifahari sana huko mbinguni. Mpaka sasa majumba haya au makao haya, bado mengi sana yakitungojea kuyaingia. Yesu anatuhakikishia jambo hili. Jumba lako linakungoja, Je, utaliingia?
(8) NAKWENDA KUWAANDALIA MAHALI (MST. 2)
Yesu amekwenda kutuandalia mahali kama mtu anayeandaa vyakula mezani. Hatimaye atakuja kutukaribisha wote tule na kunywa mezani pake (LUKA 22:29-30).
(9) NITAKUJA TENA NIWAKARIBISHENI (MST. 3)
Yesu atakuja kutukaribisha mezani wakati wa Kunyakuliwa kwa Kanisa (1 WATHESALONIKE 4:16-17). Baada tu ya kunyakuliwa, tutafanyiwa Karamu katika Harusi ya Mwanakondoo. Tujiweke tayari maana hatuijui siku wala saa (LUKA 12:37,40).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..
www.mwakasegebibilia.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni