Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : http://www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : http://www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : http://www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO: ISHARA ZA ZAMANI HIZI (MATHAYO 16:1-4)
Katika MATHAYO 16:1-4, tunaona Yesu akizungumza juu ya watu ambao ni mabingwa wa kutambua majira ya mvua kwa kuangalia ishara za kutanda mawingu, au ishara nyinginezo na kufanya maandalizi mapema ya kuanua nguo zilizowekwa nje au kuuingiza ndani unga uliotandazwa nje kwenye jamvi au mkeka ili ukauke n.k.; lakini hawajui kuzitambua ishara za majira waliyo nayo, na kufanya maandalizi ya kujikinga na madhara yatakayowapata. Ujumbe huu ni hai kabisa kwetu
leo. Majira tuliyo nayo, ni ya ukingoni sana ishara zote za kuja kwa Yesu kulinyakua Kanisa lake au watu waliookoka zinaonekana wazi kama mawingu yaliyotanda angani tayari kwa mvua kubwa. Gharika inakuja kama wakati wa Nuhu na kwa wale wanaozitambua ishara za zamani hizi, ni wakati wa kujificha haraka katika safina, kukwepa maangamizo. Ni muhimu basi kama tunapenda nasi kukwepa maangamizo, kuzifahamu ishara zilizopo za zamani hizi. Ni makusudi ya somo letu la leo kupata mwanga juu ya jambo hili na kujua jinsi ya kufanya. Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele vinne:-
(1) KUJA KWA YESU KULINYAKUA KANISA;
(2) MADHARA YATAKAYOWAPATA WALE WASIONYAKULIWA;
(3) ISHARA ZA ZAMANI HIZI;
(4) JINSI YA KUFANYA ILI KUKWEPA MAANGAMIZO.
(1) KUJA YESU KULINYAKUA KANISA
Yesu alisema wazi kwamba atarudi tena kuwachukua wale watakatifu walio wake
(YOHANA 14:1-3; 16:16-19, 22). Wakati wa kupaa kwake Yesu kwenda mbinguni malaika waliwaambia wanafunzi wa Yesu kwamba Yesu atarudi (MATENDO 1:9-10). Maandiko yanasema wazi kwamba walio wake Yesu watanyakuliwa na Bwana Yesu na watatoka duniani hapa kumlaki Yesu hewani (1 WATHESALONIKE 4:15-17; 1 WAKORINTHO 15:51-54). Yesu atakuja kulinyakua Kanisa saa ambayo watu hawaidhani (MATHAYO 24:44). Kwa watu wengi, siku ile itawajia ghafla kama mtego unasavyo (LUKA 21:34-35). Wawili watakuwako kitandani au shambani mmoja atanyakuliwa, mwingine ataachwa (MATHAYO 24:40-41).
(2) MADHARA YATAKAYOWAPATA WALE WASIONYAKULIWA
Baada tu ya kunyakuliwa Kanisa, wote waliobaki duniani watakabiliana na dhiki kubwa ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa (MATHAYO 24:21). Watu watatafuta mauti siku hizo, lakini kufa hakutakuwako ila kuteswa tu mateso makuu yasiyoelezeka (UFUNUO 9:1-6).
(3) ISHARA ZA ZAMANI HIZI
Haitupasi kuchukuliwa na gharika kama ilivyokuwa watu wale wakati wa Nuhu (MATHAYO 24:36-39). Ni muhimu kuzitambua ishara za ukaribu wa kuja kwake Yesu na kujiweka tayari (MATHAYO 24:32-35). Sasa basi ni ishara zipi za zamani hizi zinazoonyesha wazi kwamba Yesu yu karibu, malangoni?
ISHARA 10 (KUMI) ZA ZAMANI HIZI:-
1. Vita na matetesi ya vita, njaa na matetemeko ya nchi mahalimahali, haya ndiyo mwanzo wa utungu (MATHAYO 24:3, 6-8);
2. Manabii wengi wa uongo watatokea na kudanganya wengi (MATHAYO 24:11). Nabii wa uongo ni yule anayehubiri au kufundisha mapokeo ya wanadamu tu mbali kabisa na Neno la Mungu. Nabii wa kweli huyanena yaliyo sawa na Neno la Mungu (YOHANA 3:34);
3. Kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa (MATHAYO 24:12);
4. Wengine wanaojiita wakristo, watamkana Mungu kama wakati wa Nuhu kwa matendo yao (2 TIMOTHEO 3:1, 4-5; LUKA 17:26; TITO 1:16);
5. Wengine wanaojiita wakristo watampinga Kristo kwamba haokoi na kusema kwamba hakuna kuokoka ( 1 YOHANA 2:18);
6. Wengine wanaotumia Biblia na kuonekana kama ni wacha Mungu hawatamkiri Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na kwamba ni Mungu. Watasema ni mtu wa kawaida. Hii ndiyo Roho ya Mpinga Kristo (1 YOHANA 4:3);
7. Wengine wanaojiita wakristo watapinga kwa nguvu na kukataa kuyasikiliza mafundisho ya kurudi kwa Yesu kulinyakua Kanisa na kusema tangu tusikie habari hizo na kuzifundisha, mbona hayajatokea (2 PETRO 3:8-9);
8. Wengine wanaojiita Wakristo, watapenda kujulikana na kuitwa kwamba wameokoka, lakini watayakataa na kuyapinga kwa nguvu mafundisho mengi yenye uzima yaliyo katika Biblia na kwa kuzifuata nia zao, watajipatia waalimu katika wao wenyewe na kuanzisha makundi makundi mengi yanayopinga mafundisho ya kweli (2 TIMOTHEO 4:3-4);
9. Wengine wanaojiita wameokoka watapinga kuishi maisha yanayompasa kuishi mtu aliyeokoka kulingana na viwango vya Biblia, na kujitungia namna yao wenyewe ya maisha kulingana na tamaa zao na viwango vyao; na wengi watajitenga na Imani na kuwa wepesi kusikiliza roho hizo zidanganyazo na mafundisho ya mashetani yanayowafundisha wakristo kuishi sawa na viwango vyao wanavyovitaka au wanavyoviona ni rahisi (2 TIMOTHEO 3:1-8; YUDA 1:18; 1 TIMOTHEO 4:1-5). Kutakuwa na kuachana kwingi katika ndoa na kuoa wake wengi na kuolewa na waume wengi kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu (MATHAYO 24:37-39);
10. Wengine wanaojiita Wakristo watapinga kuwa chini ya mamlaka na kuelekezwa kwa maagizo kufanya wajibu Kikristo. Watasaliti mamlaka na kuonyesha ukaidi wa wazi ( 2 TIMOTHEO 3:4).
(4) JINSI YA KUFANYA ILI KUKWEPA MAANGAMIZO
1. Kuwa na hakika kwamba umeokolewa na kupewa nguvu ya kushinda dhambi na ulimwengu. Mtu aliyeokoka, amri za Mungu siyo nzito kwake, maana anawezeshwa na Yesu Kristo mwenyewe (TITO 3:3-6; 1 YOHANA 5:3-4);
2. Baada ya kuokoka, hatupaswi kurejea tena kwenye mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge na upungufu kwa sababu ya kuzipenda dini zetu tu (WAGALATIA 4:9). Agizo la Mungu ni PANA MNO hivyo inatupasa tuwe mahali ambapo kuna waalimu wanaofundisha kweli yote (ZABURI 119:96);
3. Kuvumilia mpaka mwisho bila kujali maudhi na mateso tunayoyapata kwa ajili ya wokovu au kutengwa na ndugu na jamaa (MATHAYO 24:13);
4. Kukesha yaani kuwa tayari wakati wote, kuomba siku zote tusiingie majaribuni na kujifunza Neno la Mungu na KULITENDA (LUKA 21:34-36; MATHAYO 7:24-27).
………………………………………………………………………….
Mpendwa msomaji, wewe nawe, unaweza ukawa mtakatifu, mtu unayempendeza Mungu, ukifuatisha sala ifuatayo ya kukiri makosa na kuomba msamaha kwa dhati kutoka moyoni. Yesu Kristo atakupenda sana na kukusamehe kwa hakika, na kukupa wokovu, bila kujali kwamba umefanya dhambi nyingi kiasi gani; kwa maana Yeye ni hakimu wa tofauti. Sema hivi, “Mungu Baba, hakika mimi ni mkosaji, ni mwenye dhambi. Siwezi kupuuza ukweli huu. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha leo. Yesu Kristo, nakusihi unisamehe dhambi zangu, na kunipa uwezo wa kushinda dhambi. Futa jina langu katika kitabu cha hukumu, liandike katika kitabu cha uzima mbinguni. Asante kwa kunisamehe na kuniokoa katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji tayari umesamehewa dhambi zako, na kuokolewa. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho ya Neno la Mungu; katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.
www.mwakasegebibilia.blogspot.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni