Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Somo: Je Unafahamu uzuri wa Mbinguni?
Mpendwa msomaji, pole sana na shughuli nyingi za kila siku. Ninajua kwamba muda wako ni mchache sana, kutokana na shughuli zako nyingi. Hata hivyo ninakuomba muda wako mfupi tu, ili tuzungumze juu ya jambo muhimu ambalo nimeona kwamba ni vema nikushirikishe. Je umekubali ombi langu? Natumaini umekubali. Asante sana. Basi ninakusihi tufuatane pamoja katika mazungumzo haya.
Mpendwa msomaji, huenda utakuwa umewasikia watu wengi wanaofiwa na ndugu, jamaa au marafiki zao wapendwa, wakisema, “Mungu waweke mahali pema peponi“. Jambo hili linadhihirisha jinsi kila mmoja wetu anavyoamini kwamba kuna mahali pema peponi yaani mbinguni na tena inaonyesha jinsi sisi sote tunavyopenda kwenda huko, sisi na jamaa zetu. Je wewe una shauku ya kwenda mahali pema peponi au mbinguni, baada ya kuiaga dunia hii? Najua wewe pia una shauku ya kwenda mbinguni siku moja. Hata hivyo, shauku yako itaongezeka zaidi utakapokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu uzuri wa mbinguni. Peponi au mbinguni, ni wapi na kukoje? Peponi au mbinguni, kuna uzuri usioweza kufananishwa. Tukifahamu jinsi mbinguni kulivyo kuzuri, kila mmoja wetu atazidi kuwa na shauku ya kufika huko siku moja. Mpendwa msomaji, tufuatane basi ili upate ufahamu wa kutosha kuhusu mbinguni au peponi.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Peponi au mbinguni ni wapi na kukoje?
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Mbinguni au peponi, ni juu sana, mbingu ya tatu. Biblia inasema katika 2 WAKORINTHO 12: 2-4,“Namjua mtu mmoja katika kristo,……Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo…….ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi………” Mbingu ya tatu ni wapi? Mbingu ya kwanza, ni hii iliyo na mawingu yanayoleta mvua, na mawingu mengine. Ni anga hili lililo juu ambalo sehemu yake huonekana kwa macho ya kawaida. Ndege au eropleni zote zinazobeba abiria, huruka katika mbingu hii ya kwanza. Mbingu ya pili, ni mbingu iliyo mbali zaidi yenye sayari na nyota zote. Sayari zilizoko katika mbingu ya pili ni pamoja na Zebaki, Zuhura, Mars, Mshtarii, Zahali, Uranus, Neptune, na Pluto. Sayari nyingine ziko mbali sana. Kwa mfano umbali wa dunia yetu kutoka kwenye jua ni maili 93 milioni (kilometa 148,800,000), lakini umbali wa sayari ya pluto kutoka kwenye jua ni maili 3,666 milioni (Karibu kilometa 5,900 milioni). Nyota ziko nyingi sana, zinakisiwa kufikia 400 bilioni! Nyota ziko mbali sana na dunia yetu. Nyota iliyo karibu zaidi na dunia, iko karibu maili 26,000 bilioni (karibu kilometa 42,000 bilioni). Sasa basi, baada ya sayari zote hizi na nyota hizi, ndiyo tunafika mbingu ya tatu. Mbingu ya tatu, au mbinguni, au Peponi, kwa msingi huu ni kilometa mabilioni kwa mabilioni kutoka hapa duniani. Yesu kristo alipopokelewa na wingu, na kupaa kwenda juu mbinguni (MATENDO 1:9-11), alikwenda mbali sana kiasi hiki. Huko ndiko waliko watakatifu waliotutangulia.
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . Mbinguni au peponi, ni kilometa mabilioni kwa mabilioni kutoka hapa duniani
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Tupige hatua tena na kuangalia mambo mengine. Sasa je, mtu anapokufa, anasafirije kwenda mbinguni, mbali kiasi hiki? Hatupaswi kuogopa kifo, ikiwa tunaishi maisha yaliyo mbali na dhambi. Biblia inasema katika ZABURI 116:15, ”Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake”. Kufa kwa watakatifu ni faida (WAFILIPI 1:21). Ni heri kwa wafu wafao katika Bwana (UFUNUOWA YOHANA 14:13). Kufa kwa mtu anayeishi maisha yaliyo mbali na dhambi, ni mwanzo tu wa utukufu. Mtu anayeishi maisha mbali na dhambi, anapokufa, roho yake humiminwa katika mwili mwingine wa roho unaitwa mwili wa mbinguni, kama mafuta yaliyo katika chombo kibovu kinachovuja, yanavyoweza kumiminwa katika chombo kingine kilicho kizuri. Kufa ni kumiminwa! Mtume Paulo aliyepata neema ya kuchukuliwa na kupelekwa mpaka mbingu ya tatu wakati wa uhai wake (2 WAKORINTHO 12:2-4), ulipofika wakati wa kufariki kwake, alijua ni wakati mzuri wa kumiminwa. Kwa maneno yake, katika 2 TIMOTHEO 4:6, alisema, “Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika”.
Kuhusu miili ya mbinguni, Biblia inasema katika 1 WAKORINTHO 15:40-41, 44, “Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani, lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko”. Miili hii tuliyo nayo ni mibaya sana. Ni kama vyombo vibovu. Fahari yake, yaani uzuri wa ile miili ya mbinguni ni zaidi sana kuliko miili hii tuliyo nayo. Miili ya mbinguni inang`aa mno na kupendeza sana. Mtu huwa na mwili mzuri zaidi ya ule wa malaika! Mtakatifu anapokata roho, roho yake mara moja humiminwa katika mwili mzuri wa jinsi hii. Mtu akiwa katika mwili wa mbinguni, atapenda kujitazama wakati wote. Mwili huu hauna makovu wala ulema wala hauna makunyanzi ya uzee! Baada ya mtu kuwa na mwili mzuri wa jinsi hii, huvikwa mavazi mazuri meupe sana yanayometameta sana. Weupe wa mavazi haya, ni weupe usio na mfano duniani (UFUNUO WA YOHANA 3:4-5; UFUNUO WA YOHANA 7:9; MARKO 9:2-3). Baada ya kuvikwa mavazi haya, mtu hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa katika gari zuri sana lisilokuwa na mfano duniani. Yako mabilioni ya magari ya Mungu, yanayowasubiri watakatifu. Biblia inasema katika ZABURI 68:17, “Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu”. Mtu huchukuliwa na malaika katika magari haya yanayoitwa magari ya moto, yanayoambatana na farasi wa moto na kuchukuliwa kwenda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli (LUKA 16:22; 2 WAFALME 2:11).
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Mtu hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa katika gari zuri sana