Jumapili, 2 Februari 2014

HARUSI YA KANA (Wedding in Cana of Galilee) *sehemu ya nne*

Na Mtumishi Gasper Madumla
Shalom...
Bwana Yesu asifiwe...
Nasema;
Haleluya...,Haleluya...

Fundisho hili sio la kukosa,maana lipo kusudi kwako wewe usomaye ujumbe huu.
Ni kweli umeshawahi kusoma mafundisho mengi sehemu mbali mbali,lakini mimi nakuhakikishia kabisa,kwamba utapokea mambo makubwa sana usomapo fundisho hili mahali hapa,na Bwana mwenyewe anakwenda kukuhudumia sasa.
Harusi ya Kana huzungumziwa mara chache sana,yaani ni vigumu kuwaona watumishi wa Mungu wakizungumzia harusi hii,lakini ipo NEEMA ya pekee tena siku ya leo,ikiwa ni siku ya nne ya fundisho hili zuri,kulileta kwako.

*Msingi wa fundisho hili hunatoka Yoh.2:1-11.

Na leo tunaendelea katika mstari huu,tunasoma;

"Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu." Yoh.2:7.

Haleluya...

Biblia yangu ina niambia, mara tu Yesu alipowaambia wanafunzi wake wayajalize mabalasi maji,wakayajaliza papo hapo,pasipo mahojiano. Tazama labda katika Biblia yako imeandikwaje.
Utaona pale Yesu alipowaambia wayajalize maji,tendo lilofuata ni kuyajaliza maji,hatuoni wanafunzi wa Bwana wakilalamika au huoni wanafunzi wakifanya jambo liwalo lote isipokuwa walitii kile alichosema Bwana.

Ndiposa nikajifunza;
KUTII SAUTI YA BWANA
Naomba utizame vizuri tena kwa mara nyingine zaidi katika Biblia yako(katika andiko hilo)pale Yesu alipowaagiza wanafunzi wake wayajalize maji yale mabalasi.
Katika biblia yangu ipo alama ya nukta pale Yesu alipomaliza kusema ( Yoh.2:7)kisha neno linalofuata biblia inasema;
"Nao wakayajaliza hata juu". Yoh.2:7

Ooh..,
Kumbe UTII WA SAUTI YA MUNGU ni mlango wa muujiza.

Wanafunzi wa Bwana Yesu walifanikiwa kuisikia sauti ya Bwana,kisha wakatii kile alichokisema Bwana.Kile walichokifanya hawa wanafunzi wa Bwana,ni kuyajaza maji hadi juu,pasipo manunguniko yoyote yale,sababu walichokijua ni kwamba Bwana amesema,nao wanapaswa KUTII.

Yesu alikuwa na uweza mkuu wa kufanya muujiza wa kuleta divai iliyo bora pasipo hata ya uwepo wa maji,lakini tunaona Bwana Yesu akiwaagiza walete maji ili muujiza utendeke,alichokitafuta hapa ni ;
KUTUFUNDISHA SISI NAMNA IPASAVYO KUTII SAUTI YAKE.
*Yeyote yule anaitii sauti ya Bwana,mafanikio,muujiza ni mali yake.

Wakristo wengi leo tunaangaika na hali ngumu ya kimaisha,pamoja na kuteswa na nguvu za giza kwa sababu tumekataa kutii sauti ya Mungu.
Nasema tumekataa,maana kweli tumeisikia tayari lakini hatutaki kutii,kisha tumeishia kuomba maombi ya " kuvunja na kubomoa ".
Maombi ya kuvunja na kuharibu kazi za ibilisi ni maombi mazuri sana,lakini kama tumeshindwa kuishi maisha ya kutii kweli ya Bwana,basi maombi hayo hayana maana kabisa.

Haleluya...

Maandiko yako wazi kabisa kwa habari ya UTII.Biblia inasema;
"kutii ni bora kuliko dhabihu" (to obey is better than sacrifice) 1 Samweli 15:22.
Bwana hupenda mtu mtiifu wa sauti yake.
Katika harusi ya Kana,wanafunzi hawakuitii sauti ya mwanadamu bali waliitii sauti ya Mungu,ndio maana walifanikiwa.

Leo tunaisikia sauti ya Mungu mara nyingi sana ikisema nasi kupitia watumishi wake aliowaweka hapa duniani. Watumishi wa Mungu wanasema nasi juu ya mambo mengi ambayo ni miujiza kwetu,lakini shida bado ni ile ile,tumekataa kusikia sauti ya Mungu pamoja na kutii.

Fikiria ni kwa namna gani ambayo mchungaji wako asemavyo juu ya maisha yako,lakini kwa nini upo vile vile,yaani hakuna ongezeko lolote lile la kiroho wala la kimwili,Na wala la kiuchumi. Na hapo utagundua kwamba ipo shida. Shida haipo kwa mchungaji wako,shida ipo kwako.UMEKATAA KUITII SAUTI YA MUNGU,Ndio maana unapata msoto.
Maisha ya Ibrahimu baba wa imani,yalikuwa katika msingi wa kutii sauti ya Bwana Mungu,na ndio maana akafaulu kuishi maisha ya UTELE.

Ibrahimu alitii sauti ya Mungu pale Mungu alipomuambia amtoe mwanaye wa pekee,AMPENDAYE,Isaka,awe sadaka ya kuteketezwa.
Unajua ndugu haikuwa rahisi jambo hili hata kidogo,lakini Ibrahimu alilishinda JARIBU hili kwanza kwa KUTII. Labda ngoja tusome kidogo hapo;

" Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu,akamwambia,Ee Ibrahimu! Naye akasema,Mimi hapa. Akasema,Umchukue mwanao,mwana wako wa pekee,umpendaye,Isaka,ukaende zako mpaka nchi ya Moria,ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia." Mwanzo 22:1-2

Mungu anamjaribu Ibrahimu kwa mara ya kwanza. Ibrahimu hakuwahi kujaribiwa,lakini hapo tunaona Mungu akimjaribu Ibrahimu kwa mara ya kwanza baada ya mambo mengi kupita.
Ikiwa ndio hivyo basi yale mambo yote ambayo Ibrahimu aliyokuwa akiyapitia (kuanzia Mwanzo sura ya12,mpaka sura ya 21) hayakuwa majaribu kwake. Lakini sasa ndipo anajaribiwa baada ya mambo hayo kupita.

Haleluya...

Ndiposa nikajifunza kwamba ;
MUNGU HAWEZI KUMTUMIA YEYOTE YULE PASIPO KUMJARIBU.
Mtu yule mtii ni lazima apitishwe katika moto,moto ni majaribu.

Lakini tunaona Ibrahimu akabarikiwa sana,baada ya kuitii sauti ya Mungu iliyomwambia akamtoe mwanaye AMPENDAYE, sadaka ya kuteketezwa.


Ile namna ya kukubali kumtoa Isaka awe sadaka ya kuteketezwa ilikuwa ni UTII wa hali ya juu sana.
Emu,pata picha kama sauti hiyo ya Mungu ingemjia mlokole mmoja wa kizazi hiki,mlokole yule asiyeisikia sauti ya Bwana kwamba Mungu ndio aseme mtu huyo amtoe mwanaye ampendaye awe sadaka ya kuteketezwa,

Mimi nakuambia mlokole huyo ni lazima akemee sauti hiyo,na kusema kwamba ni sauti ya Ibilisi,Na wala sio sauti ya Mungu.

Ooh, Haleluya...
Haleluya...

Sasa angalia, nikupe akili ya mwisho,tazama;
Yesu yupo harusini na huku akitufundisha namna ya kuitii sauti yake, Biblia inasema;
Yesu anawatuma wanafunzi wake waende kuteka maji,nao wale wanafunzi WANATII ile sauti,kisha moyo wa Bwana unafunguka na kuachilia muujiza wa kwanza wa kubadilisha maji kuwa divai.

Oooh...!Kumbe mtu akitii sauti ya Mungu,Mungu hufungua moyo wake na kumuhudumia mtu huyo,kadri apendavyo...

ITAENDELEA...

*Ikiwa umeguswa na nguvu za Mungu kupitia fundisho hili linaloendelea mahali hapa,usisite kunipigia simu ili tuombe kwa pamoja.
* Fursa ya kumpa Bwana maisha yako,awe Bwana na mwokozi wako,aje kwako nawe uokoke,fulsa hiyo ndio sasa,itumie vizuri na usisite kunipigia.

*Pia kwa huduma ya maombi na maombezi,mawasiliano yangu ni;
0655-111149.

*Usikose fundisho lijalo.

UBARIKIWE.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni