Jumanne, 18 Februari 2014

SOMO : MIUJIZA YA WATU KUANGUKA CHINI NA ASKOFU KAKOBE


Askofu Zachary Kakobe
Katika miaka ya hivi karibuni, kumezuka wimbi kubwa la miujiza ya “watu kuanguka chini”. Wimbi hili limezagaa sehemu nyingi duniani na hivi sasa, nchi yetu Tanzania imekubwa tayari na wimbi la “miujiza hii. Watu hawa wanaojiita watumishi wa Mungu, watasema kwa kiingereza,
“RELEASE THE POWER OF GOD” wakimaanisha “NAFUNGULIA AU NAACHIA NGUVU YA MUNGU”, na baada ya kurusha mikono yao, au kupuliza hewa kwa mdomo, watu wataanguka chini kwa wingi wao, wakati mwingine kusanyiko zima, na watu watasema wameuona uwepo wa Mungu! Watu hawa wanafanya kile wanachokiita, “DEMONSTRATION S OF THE POWER OF GOD”, au “MAONYESHO YA NGUVU YA MUNGU”, huko na kule, na kuwaarika watu waje “kuona nguvu ya Mungu”. Kanisa la Mungu, lazima liwe macho. Hatupaswi kuwa watoto wachanga wa kiroho, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za uda nganyifu (WAEFESO 4:14 ). Kwa sababu hii, leo, tunachukua muda wa kutosha, kujifunza kwa undani juu ya mambo haya, ili Shetani asije akapata kutushinda kwa kukosa kuzijua fikra zake (2 WAKORINTHO 2:11 ). Tutaligawa somo hili katika vipengele saba:

( 1 ). UMUHIMU WA KUZIJARIBU ROHO.

( 2 ). JINSI YA KUZIJARIBU ROHO

( 3 ). MAKUSUDI YA MIUJIZA YA MUNGU.

( 4 ). MAFUNDISHO YANAYOTOKANA NA MIFANO YA WATU KUANGUKA CHINI KATIKA BIBLIA.

( 5 ). JINSI YA KUKWEPA MADHARA YA ROHO YA UPOTEVU.

( 6 ). JINSI YA KUMPA IBILISI NAFASI YA KUTUTUMIA.

( 7 ). JINSI YA KUWASAIDIA WALIOKUMBWA NA ROHO YA UPOTEVU.

( 1 ). UMUHIMU WA KUZIJARIBU ROHO.

Ni muhimu kufahamu kwamba, siyo kila muujiza niwa Mungu, na siyo kila anayejiita Mtumishi wa Mungu, ni Mtumishi wa Mungu kweli. Shetani anaweza kufanya miujiza pia, kwa kutumia Watumishi wake, na wakawashangaza watu wengi, hata watu wengi wakawasikiliza na kusema, watu hawa ni uweza wa Mungu ule mkuu ( MATENDO 8:9-11; KUTOKA 7:8-11). Wakati wote, miujiza ya Shetani ina lengo la kuwapoteza kama yamkini au ikiwezekana, hata Wateule wa Mungu ( MATHAYO 24:24 ). Ili Shetani afanikiwe kuwapoteza Wateule hatakuja kwetu kwa kuwatumia Wachawi au Waganga wa kienyeji. Akifanya hivyo tutashituka mapema. Atajigeuza awe mfano wa Malaika wa nuru, na Watumishi wake watajigeuza wawe mfano wa Watumishi wa haki ( 2 WAKORINTHO 11:13-15 ). Watumishi wake, watakuja kwetu wakishika Biblia na kuharibu Wokovu, ingawa hawatakuwa na msisitizo mkubwa kwenye Neno la Mungu na Utakatifu. Muda mfupi sana watautenga kwenye Neno la Mungu na muda muda mwingine utatumika kufanya maonesho ya “miujiza” yao. Ndiyo maana ni muhimu sana kuzijaribu roho na kutokuamini kila roho ( 1YOHANA 4:1 ). Roho zote zinazotokana na Mungu, ziko chini ya Roho wa Kweli, Roho Mtakatifu, na roho zote zinazotokana na Shetani ziko chini ya ROHO YA UPOTEVU, Shetani mwenyewe ( 1YOHANA 4:6 ). Chochote kinachofanyka lazima tukijaribu na kujua kwamba kiko kundi lipi kati ya hayo mawili ( 1WATHESALONIKE 5:21 ).

( 2 ). JINSI YA KUZIJARIBU ROHO.

Tutawezaje kuzijaribu roho hizi na kufahamu kwamba zinatokana na Mungu au la? Jinsi ya kuzijaribu, SIYO KUOMBA WALA KUFUNGA, bali tunazijaribu kwa NENO LA MUNGU!Roho zinazotokana na Mungu, ziko chini ya ROHO WA KWELI. Neno la Mungu,ndiyo KWELI ( YOHANA 17:17 ). Neno la Mungu ndiyo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu. Kwa kutumia taa na mwanga huu, tunamulika na kuona vitu vya hatari na kuviepuka! Roho ya upotevu, haiendani na Kweli ya Neno la Mungu ( YOHANA 8:44-47 ). Roho ya upotevu hupotosha tafsiri ya Neno la Mungu na kulitumia isivyo ( MATHAYO 4:5-7; ZABURI 91:10-12 ). Tuchukue muda basi kuiangalia tafsiri ya kweli ya Neno la Mungu kuhusu miujiza.

( 3 ). MAKUSUDI YA MIUJIZA YA MUNGU.

Miujiza ya Mungu wakati wote, hufanyka ili KULIONDOA TATIZO na kamwe haifanyiki kama MAONYESHO YA NGUVU YA MUNGU! Miujiza yote ya Mungu kwa mkono wa Musa, katika nchi ya Misri, ilikuwa na lengo la kumfanya Farao awaachie wana wa Israeli na kuacha kuwatumikisha; miujiza hiyo haikufanywa kama maonyesho ya nguvu ya Mungu! Musa aliponyoosha Fimbo yake juu ya Bahari ya Shamu na kuigawanya, muujiza huo ulikuwa na lengo la kuondoa tatizo, siyo “SHOW”! Maji machungu ya Mara yalipogeuzwa kuwa matamu, haikuwa “SHOW” au onyesho! Bwana alipoleta “Mana” kutoka Mbingu au Kwale, miujiza hiyo haikuwa “show” ilikuwa na lengo la kuondoa matatizo. Jua liliposimama kimya na likachelewa kuchwa kama muda wa siku nzima wakati wa Yoshua, muujiza huo haukuwa onyesho la nguvu za mungu bali lilikuwqa na lengo la kuondoa tatizo la kukosa mwanga wakati wa vita.



Jaribu kutaja kila muujiza! Danieli kukaa pamoja na simba katika tundu, haikuwa “SHOW”! Shadraka na Meshaki na Abedinego walipotupwa kwenye moto wasiteketee, muujiza huo haukuwa onyesho ya nguvu ya Mungu bali kulikuwa na tatizo la kuondoa. Yesu alipobadili maji yakawa divai, muujiza huo haukuwa onyesho ya nguvu ya Mungu bali walikuwepo watu waliokuwa na tatizo la kutindikiwa divai wakati wa harusi.


SHETANI NDIYE MFANYA MAONYESHO (MATHAYO 4:8). Mazingaombwe ni maonyesho ya Shetani! Mungu hafanyi maonyesho ya nguvu yake ili kutafuta watu wamwamini. Yeye anadumu wa kuaminiwa hata kama hatutamwamini ni kwa kungoja afanye maonyesho ( 2TIMOTHEO 2:12-13 ). Mafarisayo na Masadukayo walipomuomba Yesu AWAONYESHE ishara itokayo Mbinguni, hakuwapa ishara, aliwaacha akaenda zake! ( MATHAYO 16:4 ). Je, alipowaacha walionekana hana nguvu ya Mungu? Yeye hudumu wa kuaminiwa. Miujiza ya Mungu hutumika kutuondolea mizigo yetu na kutufanya tumwamini kuhusiana na upendo wake,huruma zake, ahadi zake n.k. Watu wakisema watuombee ili twende Mbinguni kutalii na kurudi, huyu siye mungu wa Biblia, ni mungu wa dunia hii, baba wa uongo, Ibilisi.

( 4 ). MAFUNDISHO YANAYOTOKANA NA MIFANO YA WATU KUANGUKA CHINI KATIKA BIBLIA.

Mahali pote katika Biblia tunapoona watu wasio na mapepo wakianguka chini mbele ya utukufu wa Mungu, hakukuwa na mikutano ya Injili, wala watu wa kuwaombea na kuanguka wenyewe, na kulikuwa na kusudi au sababu, aidha walianguka na kuwekwa tayari kuisikia sauti ya Mungu, wengine walianguka wenyewe kwa hofu au kwa hiari yao ili wamuombe Mungu au kumsihi Yesu awaponye n.k. Kamwe, kuanguka kwao hakukutokana na onyesho la nguvu ya Mungu au maombezi ya mtu yeyote.. ( MIFANO: EZEKIELI 1:8; 3:22-23; 43:1-7; 44:4-5; MATHAYO 17:1-8; 26:38-39; LUKA 5:12-13; YOHANA 18:2-6; MATENDO 9:1-6; 26:12-18; 16:26-30 ). Watu pekee walioanguka chini baada ya mtumishi wa Mungu kufanya maombezi, walikuwa ni watu wenye mapepo.. Mapepo ndiyo yaliyokuwa yanaanguka ( LUKA 8:26-29; MARKO 3:11 ). Iweje basi kwa watu hawa kwamba KILA MTU katika mikutano yao, sharti aanguke chini, hata kama anataka kutoka kwa Mungu, kazi, fedha, kurudiana na mumewe, kushinda mitihani, chumba cha kupanga, mchumba n.k? La kushangaza ni kwamba wengi huanguka chini na matatizo na kuinuka wakiwa na matatizo hayohayo! Ni Mungu yupi huyo!

( 5 ). JINSI YA KUKWEPA MADHARA YA ROHO YA UPOTEVU.

Kama tulivyojifunza, roho ya upotevu inajaribiwa kwa Neno la Mungu. Yesu alimshinda Shetani kwa IMEANDIKWA NA TENA IMEANDIKWA! ( MATHAYO 4:4-11 ). Neno la Mungu ni upanga wa Roho wa kumshindia adui Ibilisi ( WAEFESO 6:17 ; WAEBRANIA 4:12-13 ). Kwa sababu hii baada ya kuokoka hatupaswi kukimbizana na mikutano ya Injili huku na kule na kutafuta misisimuko tu bali tutafute na kutulia mahali tunapoweza kujifunza Neno la Mungu kipengele kwa kipengele, amri juu ya amri, kanuni juu ya kanuni, huku kidogo na huku kidogo katika Biblia nzima ( ISAYA 28:9-10 ).

( 6 ). JINSI YA KUMPA IBILISI NAFASI YA KUTUTUMIA

Watu wengi wanaotumiwa na Shetani kufanya miujiza hii, wamempa Ibilisi nafasi kuwatumia ingawa hapo mwanzo wengi wao walikuwa watoto wa Mungu hasa. Wamempa Ibilisi kwa jinsi ifuatavyo:-


1. KUTAKA KARAMA ZA MUNGU BILA UTAKATIFU-Njia iliyo bara ya kutaka karama zilizo kuu, ni kutafuta KWANZA upendo wa ki-Mungu ulio mbali na kiburi, majivuno, kukosa adabu, kufurahia udharimu n.k. Upendo hufurahia pamoja na KWELI. Ni utakatifu ( 1 WAKORINTHO 12:28-31 ). Karama za Mungu ni za Roho MTAKATIFU, hivyo hutenda kazi kikamilifu katika utakatifu. Kutaka karama bila kutaka utakatifu, na kutaka kutumiwa na Shetani!


2. KUWA RAFIKI WA DUNIA-Ukiwa rafiki wa dunia yaani kuwa sawa na watu wa dunia katika kusema, kuvaa, kutenda n.k, unakuwa ADUI wa Mungu. Hawezi kukutumia. Atakutumia Ibilisi ( YAKOBO 4:4 ).

3. KUWA NA KIBURI NA KUKATAA USHAURI- Wengi wao Roho Mtakatifu amewaonya kwa njia mbalimbali na pia akiwatumia wat wa Mungu kuwaeleza kuwa huduma hiyo siyo ya Mungu, lakini kwa kiburi wamedhani wanaonewa wivu wakaendelea ( METHALI 11:2; YEREMIA 50:31-32; METHALI 16:18; 11:14; 19:20; 20:18 )

( 7 ). JINSI YA KUWASAIDIA WALIOKUMBWA NA ROHO YA UPOTEVU..

Tuwarejeze upya kwa roho ya upole huku tukijiangalia nafsi zetu wenyewe tusijaribiwe kama wao na pia kuwaombea ( WAGALATIA 6:1; 1YOHANA 5:14-16; YAKOBO 5:16 ). Kuna Baraka tele kufanya hivi ( YAKOBO 5:19-20 ).

OMBI LANGU KWAKO.

Share ujumbe huu na marafiki zako wa “facebook” na “twitter” kwa kubonyeza kitufe chenye neno “share” hapa chini ya maneno haya. Ukifanya hivyo, utakuwa mmoja kati ya maelfu ya watu wengine watakaopokea baraka za Mungu kwa kusambaza somo hili kwa maelfu ya watu katika mitandao mbalimbali ya internet.

MUNGU AKUBARIKI SANA!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni