Jumapili, 9 Februari 2014

HOJA YA ASKOFU GAMANYWA: FALSAFA YA UMILIKAJI KWA MUJIBU WA BIBLIA (4)


Rais wa WAPO Mission International, Aksofu Sylvester Gamanywa
Katika makala yaliyopita tulisoma habari Utoaji unaotambulika; na Mtindo wa utoaji wa “Injili ya utajirisho”. Kisha tukajifunza juu ya Tofuati kati ya “Injili ya utajirisho” na“Falsafa ya kumilikisha” kwa mujibu wa Biblia. Leo tunaendelea kuchambua katika maeneo haya haya ukiwa ni mwendelezo wa somo lililopita:
Sipingani na imani sahihi ya kumtolea Mungu ili kubarikiwa
Hebu nianze kwanza kwa kujitetea mapema kwamba, sipingani kabisa na imani ya kumtolea Mungu katika maana yake halisi. Na pia sipingi kwamba kutoa kwa imani ya kubarikiwa ni makosa. Dhana ya kutoa ili kubarikiwa ni ya kibiblia na haina ubishi wala utata. Makanisa yote yanafundisha utoaji na kunukuu maandiko stahili kuhusu ahadi za Baraka zitokanazo na kumheshimu Mungu kwa matoleo na sadaka.

Ninachotahadharisha ni nadharia ya kuugeuza utoaji njia ya “kufanya biashara na Mungu” kwa kutumia maandiko vibaya! Na wahusika wanafanya hivyo hali wakijua wanawadanganya watu watoe fedha kwa ahadi za “kuvunjiwa laana za umaskini wa kipato”; wakati umaskini wenyewe unazidi kuendelea katika maisha ya watoaji; wakati waliopokea matoleo hayo wao wanainuka kiuchumi peke yao kama watu binafsi

Mitume walilijua hili wakatahadharisha waamini kujilinda na jamii ya watu wanaoibuka kutumia mwavuli wa maandiko kukusanya fedha kwa madai ya kuwaombea wapokee miujiza . Ushahidi wa tahadhari hii ni kama alivyaondika Mtume Petro akisema:

“Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na Wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambayo hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.” (2Pet.2:1-3)
Unaona katika maandiko haya? Soma maneno kama “Kuingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza”; na “Wengi watafuata ufisadi wao” na “..njia ya kweli itatukanwa..” na “watajipatia faida kwenu kwa maneno ya kutunga.”! Huu ndio ushahidi unaoidhirisha “itikadi ya Injili ya Utajirisho” ambayo kwa werevu wananukuu maandiko yanayohusu utoaji, na “kuingiza kwa ujanja maneno yao ya kutunga” yakiwa na kishawishi cha kuhamasisha watu kutoa lakini, matokeo yake huja kinyume na matarajio!

Kwanza, tahadhari muhimu ni kutambua mapema kwamba wakusanyaji na wapokeaji wa matoleo/sadaka ya injili ya utajirisho, kwa kupitia “mwavuli wa maombezi” hukusanya fedha kutoka kwa watu binafsi katika jamii, Lakini fedha hizo hubaki kuwa ni mali yao binafsi na sio fedha za taasisi kwa malengo ya kitaasisi. (huu ni uvunjaji wa sheria za nchi na uhalifu wa kiimani)

Athari sio tu “wapakwa mafuta wa Injili ya Utajirisho” kuchukua fedha kutoka kwa “watu binafsi” kwa “matumizi yao binafsi”; bali ni “kishawishi wanachotumia kukusanya fedha“ kutoka kwa watu binafsi katika jamii cha madai ya kuwa na “upako wa kuvunja laana ya umaskini wa kipato” katika maisha ya watoaji lakini kwa sharti la “kutoa fedha kama kanuni pekee ya kuvunjiwa laana ya umaskini” (hili fundisho potofu la imani)

Matokeo yake, wengi wasiolijua Neno sahihi la Mungu wamewaendea kama waganga wa kienyeji wakitoa mali na fedha zao kwa “matarajio ya kuvunjiwa laana za umaskini wa kipato” lakini bado maisha yao huendelea kuwa duni siku zote; wakati hao “wapakwa mafutwa wa utajirisho” ndio huinuka kiuchumi kuliko jamii ya watu waliochukua fedha zao! (Huu ni udanganyifu wa mapato ya aibu)

Matokeo yake ni nini? Wale wasiopokea utajiri kama walivyoahidiwa kwa sababu ya uelewa mdogo wa tafsiri za maandiko, huishia kuitukana imani ya kweli, kwa kutafsiri kwamba wahubiri wote ni waongo na matapeli kitu ambacho huo nao ni “upotofu wa upande wa pili”



Ufunuo wa mfumo wa utajiri shirikishi na sio watu binafsi wachache
Kama nilivyotangulia kujuza kwenye matoleo yaliyopita, ufunuo wa falsafa ya kumilikisha kwa mujibu wa Biblia unalenga kuturejesha kwenye ramani ya ujenzi wa kanisa la kwanza! Makosa mengi na ukengeufu mwingi katika jamii ya Kikristo, ni kutokuujua ufunuo wa kanisa la kwanza ambalo mitume wa kwanza waliutumia kuendesha huduma za kikanisa.

Najua kwamba kuna nadharia nyingi na itikadi zinazokinzana kuhusu utendaji wa kanisa la kwanza, na hili nii somo jingine linalohitaji makala tofauti na hoja hii. Lakini msingi wangu na uteteaji wangu kuhusu falsafa ya kumilkisha umejikita katika msingi wa kanisa la kwanza. Nirejee kusisitiza kwamba, mitume hawakutenganisha maadili ya kiimani na uchumi kwa waamini kanisani. Ndiyo maana kanisa hilo lilidumu kwa muda wa miaka 40 likiwa na zaidi ya waamini 30,000 na imeandikwa hapakuwepo hata mmoja aliyekuwa na umaskini wa kipato: “Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.” (Mdo.4:32)
hii ni kuonnesha kwamba waamini waliendelea kumiliki mali zao lakini hapakuwepo na kutambiana kati ya walio nacho dhidi ya wasio nacho. Maneno kama “walikuwa na vitu vyote shirika” yanamaanisha kwamba “matumizi ya mali za waamini binafsi yaliwajumuisha na wengine pia pasipo masharti.”

Huu ulikuwa ndio mfumo wa maisha ya waamini wa kanisa la kwanza. Kila mmoja alimhesabu mwenzake kuwa ni ndugu na kumjali kama ndugu na hivyo hapakuwepo na matabaka ya kiuchumi kanisani.

Kana kwamba hii haitoshi, tofuati na “Injili ya utajirisho” inayohubiriwa siku hizi, ambapo, watoaji huishia kufilisika na wapokeaji huinuka kiuchumi peke yao kama watu binafsi; Ufunuo wa kiuchumi wa kanisa la kwanza uliwanufaisha wote!

“Na Mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.” (Mdo.4:33-35)
Ukisoma maandiko unakutana na maneno kama haya: “ ..neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenyewe mahitaji;…” Maana yake, walishirikiana kwa kupitia mfumo wa vikundi vya ushirika vya nyumba kwa nyumba kuwezesha kiuchumi. Waliokuwa na mali za ziada waliziuza na kuwapatia mitaji wasiokuwa na uwezo, kila mtu akazalisha na mapato yakaongezeka kwa wingi, na matoleo yakaongezeka kwa wingi kanisani! Matokeo yake, Mitume nao wakawezeshwa kiuchumi wakajitoa kuhubiri Injili ya miujiza na maelfu ya watu wakazidi kuokolewa na kuongeza kila siiku.

Kama mfumo huu ulifanya kazi katika kanisa la kwanza, iweje ushindikane katika kanisa la leo? Kwa vyovyote kanisa la leo haliko kwenye msingi wa ufunuo wa kanisa la kwanza. Falsafa ya kumilisha kwa mujibu wa Biblia, ndiko inakotuelekeza kurejea!

Itaendelea wiki ijayo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni