Jumamosi, 1 Machi 2014
SOMO : MAONO NA NDOTO * sehemu ya pili *
Mtumishi Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe...
"Itakuwa siku za mwisho,asema Mungu,nitawamwagia watu wote Roho yangu,na wana wenu na binti zenu watatabiri ; na vijana wenu wataota maono ; na wazee wenu wataota ndoto" Matendo 2:17
Andiko hilo hapo juu ndilo andiko letu la kusimamia fundisho letu la MAONO na NDOTO.
Biblia inaweka wazi kabisa ya kwamba nyakati za mwisho Bwana Mungu atamwaga Roho yake kwa watu wote,na mara tu ya Roho wa Mungu kuwashukia watu,Biblia inatuambia ya kwamba wana na binti watatabiri.
Nasi tulijifunza kwa undani kidogo juu ya KUTABIRI na tukaangalia watu waliopata kutabiri katika maandiko matakatifu.
Ila jambo moja la msingi ni kwamba;
Wale wote waliotabiri,walitabiri baada ya kushukiwa na nguvu za Roho mtakatifu.
Hivyo suala la kutabiri husimamiwa na kuongozwa na nguvu za Roho mtakatifu,kama vile biblia isemavyo hapo juu (Matendo 2:17)
Kwa lugha nyingine;
ni kwamba, hakuna anayetabiri jambo au mambo ya ki-Mungu kwa kujiongoza yeye mwenyewe.
Haleluya...
naamini tupo pamoja hadi sasa.
Katika andiko letu la Matendo 2:17.Tunaona mambo matatu yakizungumziwa,kwamba yatatoke mara baada ya mwagiko wa Roho wa Mungu.
tukio la kwanza ni KUTABIRI (kama tulivyojifunza katika sehemu ya kwanza)
Tukio la pili na la tatu baada ya Roho wa Mungu kumwagwa kwa watu ni;
*MAONO na
*NDOTO
Haleluyaa...
01.MAONO
Zipo tafsiri nyingi zinazoelezea maana ya neno maono. Na inawezekana hata wewe unatafsiri yako kuhusu maono.
Lakini nakushauri uchukue tafsiri hii nikupayo siku ya leo,kwa maana itaongeza ufahamu wako kwa namna ya tofauti kabisa.
Nami ninakupa tafsiri zaidi ya mbili ili yamkini kama ulikuwa ukielewa moja tu,basi hizo nyingine ziwe faida kwako.
Maono ni nini?
*Kwa mujibu wa maandiko matakatifu;
Maono ni ishara za picha halisi zionekanazo katika ulimwengu wa roho zenye kutambulisha tukio lijalo katika ulimwengu wa kimwili.
Nisemapo kwamba " ishara za picha halisi" ninazungumzia ,picha ambazo sio za maigizo au sio picha za bandia,Bali ni picha halisi. Mfano,mtu anaweza kuona picha yako katika ulimwengu wa roho jinsi ulivyo hivyo hivyo ndani ya tukio fulani ambalo tukio hilo baada kukamilika kiroho,hudhihilika katika ulimwengu wa kimwili.
Na ukumbuke kwamba ;
Jambo lolote ulionalo sasa limetokea ujue limekwisha tokea katika ulimwengu wa roho.
Hivyo,
matukio yote yanayotokea hivi sasa chini ya jua,mfano matukio ya mauaji ya walemavu,na mauaji mbali mbali,matukio kama vile maandamano N.K
Matukio hayo yote yalikuwa katika mfumo wa picha katika ulimwengu wa roho,na baada tu ya picha hizo kukamilishwa katika ulimwengu wa kiroho,sasa yanapewa ruhusa kudhililika katika macho ya damu na nyama
Maandiko yanatuambia;
" ...hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri."Waebrania 11:3
Haleluya...
Nasema; Haleluyaa...
*Maono ni kielelezo kwa njia ya picha ndani ya roho ya mwonaji,kielelezo chenye kueleza tukio lililopita au hata lijalo.
maono yanaweza kuwa ni picha za matukio yaliyopita YENYE HALI YA KUENDELEA.
Mfano wa maono katika matukio yaliyopita yenye hali ya kuendelea.
Mtizame mtume Paulo mtu ambaye hapo awali alikuwa ni mtesaji wa watu wenye imani kwa Kristo Yesu.
Paulo hakuwa mmoja wa mitume kumi na wawili waliochaguliwa na Bwana,lakini sasa tazama baada ya kufanywa awe mtumwa wa Kristo Yesu,mtume kwa watu wote. Ana hubiri habari za Bwana Yesu kana kwamba ni mtu aliyekuwa naye siku zote za Bwana Yesu.
Swali la kujiuliza,
Alipataje kunena habari za Bwana Yesu kwa ufasaha, na kuna kipindi anahubiri injili kana kwamba yupo na Yesu ana kwa ana?
JIBU;
Alikuwa akiwezeshwa na Roho mtakatifu kuona MAONO juu ya maisha ya Bwana Yesu Kristo,ambayo maisha ya Bwana yalikuwa yamepita lakini yalikuwa halisi yakiendelea ndani yake.
Nimekuambia pia maono yanaweza kuwa ishara za matukio yaonekanayo rohoni,matukio yanayotambulisha matukio yajayo katika ulimwengu wa kimwili.
Swali moja la ziada ambalo waweza kujiuliza ;
Je ni kwa njia ipi mtu aweza kuona maono?
JIBU.
Zipo aina kuu mbili za njia ambazo maono hupitia,nazo ni
01.Maono kwa njia ya macho ya wazi wazi.
02.Maono kwa njia ya usingizi-kuzimia kwa roho.
(A)MAONO KWA NJIA YA MACHO YA WAZI WAZI.
Tunasoma;
" Palikuwa na mtu Kaisaria,jina lake Kornelio,akida wa kikosi kilichoitwa kiitalia,mtu mtauwa,mchaji wa Mungu,yeye na nyumba yake yote,naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi,na kumwomba Mungu daima.
Akaona katika maono WAZI WAZI kama saa tisa ya mchana malaika wa Mungu,akimjia na kumwambia,Kornelio!"Matendo 10:1-3
Haleluya...
Biblia inatuambia kwamba;
Kornelio alipata MAONO ya wazi wazi,ikimaanisha kwamba Kornelio hakuwa amelala,Bali alikuwa macho kama hivi wewe ulivyo macho muda huu.
Ndiposa;
Bwana akamtokea katika njia ya maono kwa macho ya wazi wazi kwa msaada wa Roho mtakatifu.
Biblia inatuambia;
"Bwana hujifunua katika maono,pia husema katika ndoto" Hesabu 12:6
Bwana alijifunua kwa Kornelio katika maono. Kwa lugha nyingine ni kwamba;
Bwana hajifunui katika ndoto,Bali katika ndoto Bwana husema,
Lakini kwa njia ya MAONO tu,ndipo Bwana hujifunua....
Kumbuka;
Nazungumzia MAONO.
ITAENDELEA...
Fundisho lijalo nitakupa mfano wa pili wa maono kwa njia ya macho ya wazi wazi,kisha tutaingia kwa undani kuangalia njia ya pili ya maono kwa njia ya USINGIZI.
Maono kwa njia ya usingizi wala sio ndoto Bali ni MAONO.
*Je ungependa kujua zaidi na kujua tofauti kati ya ndoto na maono kwa njia ya usingizi?
BASI,USIKOSE FUNDISHO LIJALO!.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,piga;
0655-111149.
UBARIKIWE.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni