Jumanne, 25 Machi 2014

SOMO: HUBIRINI MANENO LAINI YADANGANYAYO NA ASKOFU KAKOBE


Askofu Zachary Kakobe.
Wengi wetu tayari tunafahamu kwamba moja ya kazi zilizo kuu kabisa za ibilisi ni kudanganya. Yeye anaitwa baba wa uongo, kazi yake kubwa ni kuudanganya ulimwengu wote. ( UFUNUO 12:9 ), “…………audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata nchi na malaika zake wakatupwa pamoja naye”. Tangu wakati ule kazi yao kubwa ni kuudanganya ulimwengu yamkini kama ikiwezekana walimwengu wote wawe mbali na kweli. Kweli ni neno la Mungu. Kweli ni neno lote la Mungu. Kazi ya Shetani ni kuhakikisha wanadamu wote wanakuwa mbali na kweli. Atafanya juu chini kulipotosha neno la Mungu. Ikiwa neno la Mungu kwa mfano linazungumza juu ya Wokovu na Utakatifu hapa duniani.. Shetani atataka watu wafahamu kwamba haiwezekani kuokoka duniani. Atawadanganya kwamba wokovu siyo hapa duniani ni mpaka mbinguni ili wakifa wakute hakuna nafasi yoyote ya kuokoka na kujikuta wakiwa Jehanum. Shetani anajua kuwa mtu amewekewa kufa mara moja na baada ya kufa ni hukumu ( WAEBRANIA 9:27 ). Hakuna nafasi yoyote ya kusikia Injili baada ya kufa na ndiyo maana neno linasema “heri wafu wafao katika Bwana maana matendo yao yawatangulia”. Atawadanganya walimwengu ili wajue kwamba Utakatifu siyo hapa duniani ni baada ya kufa na watakatifu ni wachache tu, na wanateuliwa kwa vikao maalumu na mchakato fulani wa kutafuta watakatifu.. Baada ya mtu kufa ndipo mchakato unaanza na kuitwa mwenye heri na hatimaye vikao hivyo vitaendelea na mtu mmoja atatangaza kuwa mtu huyo ni mtakatifu wakati alishakufa. Watu wataamini hivyo wakati Biblia haisemi hivyo. Biblia inasema kwamba kila mtu anayetaka kuingia mbinguni na kukaa na Mungu milele anatakiwa kuwa mtakatifu.
( 1 PETRO 1:15-16 )
“Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu”.Hili ni agizo kwa kila mmoja wetu kwamba tunatakiwa kuwa watakatifu tukiwa hapahapa duniani. ( TITO 2:12 ), “Nayo yatufundisha kukataaa ubaya na tama za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa”.Utauwa maana yake utakatifu. Neno la Mungu linatuagiza kuishi aisha ya uauwa hapahapa duniani katika ulimwengu huu wa sasa. ( ZABURI 16:3 ),”Watakatifu waliopo duniani ndio waliobora, hao ndio ninaopendezwa nao”.

Nyakati za kanisa la kwanza haikuwa hivi kama leo katika madhehebu fulanifulani. Watakatifu walikuwa ni watu waliookoka kwa kutubu dhambi zao kwa kumaanisha kuziacha kabisa na kutafuta utakaso. Tunaona watakatifu wengi wakiwa na majina ya kizungu na hao ndio watakatifu wa leo katika madhehebu hayo ingawa wengine walikuwa waovu wakubwa kabla ya kufa kwao. Mungu anataka kumuona kila aliyeokoka akiwa mtakatifu. Tunaona nyaraka za Paulo Mtume ziliandikwa kwa watakatifu waliokuwepo duniani nyakati za kanisa la kwanza:

(WAFILIPI 1:1 ),”Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, waliopo Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi’. ( WAKOLOSAI 1:1-2 ),” Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yake, kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu”.

Hiyo ndiyo kweli kwamba pasipo kuishi maisha matakatifu hapa duniani mtu hawezi kuingia mbinguni. ( WAEBRANIA 12:14 ), “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu ambao hapana mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao”.

Shetani sasa anataka kuwafanya watu wadanganyike kuona utakatifu ni wa watu wachache sana, tena watu fulanifulani. Anawafanya kuona kwamba kuokoka na kuishi maisha matakatifu hapa duniani haiwezekani. Watu wanaoitwa eti ni watakatifu ni waovu wakubwa. Wameishi maisha hapa duniani wakiwa mbali na Wokovu. Kazi ya Shetani sasa ni kuudanganya ulimwengu wote, si wawili watatu ambao watadanganywa bali ni watu wengi kila mahali duniani. Kutakuwa na umati mkubwa wa watu kila mahal duniani , watachukuliwa na uongo huo.

Shetani anafanya kazi hii namna gani? Anafanya kazi hii kwa kutuia pepo wa uongo.

Mungu alivyo kama mtu ameamua mwenyewe kutokutaka kweli, anaachia roho ya upotevu kwake , anamwingiza vizuri kabisa na kumwachia kudanganyika . Tunaona mfano hapa:

Wakati wa Ahabu mfalme wa Israeli alikuwa hataki kuwaongoza Waisraeli katika kweli , alikuwa amechagua kukaa katika uongo na akatamani Waisraeli wote wawe waabudu miungu. Na kwa sababu alichagua kudanganyika , akapenda uongo kuliko kuipenda kweli . Mungu alimwachilia roho ya upotevu. Roho hiyo ya upotevu ilizidi kumfunika ili hatimaye aangamizwe. Mungu mwenyewe ndiye aliyewaruhusu roho hawa wa uongo kutenda kazi.

( 1 WAFALME 22:20-22 )

“Bwana akasema, ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi. Akatoka pepo, akasimama mbele za BWANA, akasema,Mimi nitamdanganya. BWANA akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabiii wake wote. Akasema, Utamdanganya na kudiliki pia; ondoka ukafanye hivyo”.

Maandiko yananena waziwazi ya kwamba siku za mwisho zitakuwa siku za hatari, roho zidanganyazo zitakuwa zinatenda kazi kwa namna isiyo ya kawaida. Watu watakuwa wakiupenda uongo kuliko kuipenda kweli. Watu wengi watapenda na kufurahia kukaa katika mafundisho ya mashetani. Siku za mwisho wadanganyaji watazidi kudanganya na wale wanaodanganywa kuzidi kudanganywa. Na neno la Mungu halikutuficha.

( 1 TIMOTHEO 4:1 ), “Basi roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo,na mafundishoya mashetani”. ( 2 TIMOTHEO 3:1,), “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako na nyakati za hatari”. Mstari 13 “ Lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”.

Nyakati za mwisho ni nyakati za hatari sana. Sehemu nyingine katika Biblia inasema kuwa, Shetani ameshuka mwenye ghadhabu nyingi sana akijua muda wake uliobaki ni mchache sana. Kwa sababu hiyo, amemwaga roho zidanganyazo kwa namna isiyo ya kawaida akiwa na lengo la kuudanganya ulimwengu wote waiache imani . Watoke katika kweli halisi.

Kutokana na roho hizi ambazo zitawafanya watu kudanganywa na kudanganyika , kama ilivyokuwa kwa Ahabu Pepo wa uongo aliingia katika vinywa vya manabii wake wote. Watu wanaoitwa watumishi wa Mungu, wahubiri, ndani ya vinywa vyao kutakuwa na pepo wa uongo. Watakuwa wanadanganya watu kwa wingi wao. Lakini si hilo tu, kutakuwa na umati mkubwa wa watu ambao wanataka kudanganywa. Watawaambia wahubiri “hubirini maneno laini yadanganyayo”. Hawataki kusikia kweli wanataka kudanganywa. Watu wa namna hi watawatia moyo wahubiri, yatakuwepo makanisa yanayojaa na kufulika kila kona kila mahali. Na itaonekana kana kwamba kuna uamsho kumbe ni roho zidanganyazo zinafanya kazi. Ni pepo wa uongo wanafanya kazi.

Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wanataka kudanganywa na hawapendi kweli, wanafurahia kukaa kwa mhubiri anayehubiri maneno laini yanayodanganya na kumtia mtu faraja kwamba anaenda mbinguni wakati mhubiri ni chafu nay eye anayehubiriwa wote ni wachafu. Nyakati tulizonazo zinaitwa nyakati za hatari kwa sababu maasi yameongezeka kwa namna ya kutisha. Watu wengi, wachungaji, wainjilisti, walimu na wengine ambao mwanzo walikuwa wakifundisha kweli yote bila kuchuja neno lolote, wengi wao wamebadilika siku hizi. Upendo wao wa kwanza umeshaibiwa na Adui. Zamani walikuwa wakikemea dhambi ya kusuka nywele, kuvaa mapambo n.k kama yanenavyo maandiko leo kiko wapi? ( 1 TIMOTHEO 2:9-10; 1 PETRO 3:3-5 ). Yesu alisema siku za mwisho wengi upendo wao utapoa kwa sababu ya kuongezeka maasi ( MATHAYO 24:12 ).

Maasi yatakuwa yameongezeka kama nyakati za nabii Isaya. Nabiin Isaya hakuwa na mchezo na dhambi kama tunavyoona kwa watumishi wengine nyakati hizi. Isaya alikuwa anahubiri kweli na watu hawakutaka kumsikia kwa kuwa walipenda kudanganywa. Historia ya nyakati zile za nabii Isaya inaeleza kuwa kweli aliyokuwa akiihubiri iliwaudhi sana watu. Watu wa nyakati zile hawakutaka kuyasikia mafundisho yake kiasi kwamba aliitwa na kuambiwa ‘utaendelea kufundisha maneno haya mazito ya kukwaza na kuwafanya watu kila wakati kuambiwa wachafu na waovu?”. Unaweza kuona kwa mfano mahubiri yake yalivyokuwa ( ISAYA 1:3-18 ). Nabii Isaya aliwaitwa watu wale kuwa ni watu wa Sodoma tena ni watu wa Gommora. Aliwaita watu wachafu kwa namna ileile ya watu wa Sodoma na Gomora.. Kutokana na mahubiri yake ya usafi ( utakatifu ) watu wengi walikwazika. Hatimaye Isaya aliitwa na wakuu, wakamwambia mahubiri yake yanakwaza watu, wakati wote dhambi dhambi dhambi dhambi. Acha kuhubiri dhambi, acha kuhubiri maneno hayo, hubiri tu maneno laini yadanganyayo. Lakini nabii wa Mungu Isaya hakutaka kuchuja viwango vya utakatifu na waka,wambia kama hutaki tutakukata pingili moja ya kidole kimoja kimoja mpaka tumalize vidole vyote. Lakini Isaya alisema siko tayari kuchuja viwango. Historia hiyo inaeleza kuwa walimkata pingili mojamoja ya kila kidole kwa msumeno, damu ikichuluzika huku akiulizwa “ Isaya hutaki kuchuja viwango? Hutaki kuhubiri maneno laini?”. Isaya alisema kila neno ambalo Bwana ananipa ndilo nitakalolihubiri. Walipomaliza kukata vidole vya mikono waliendelea na vidole vya miguu mpaka alipokata roho na kufa.

Nyakati za nabii Isaya walikuwepo watu waasi ambao walitaka wahubiriwe maneno laini yadanganyayo

( ISAYA 30:9-10 )

“Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kusikia sheria ya BWANA; Wawaambiao waonaji, Msione, na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo”.

Hawakumtaka Isaya lakini waliwataka wahubiri watakaokuwa tayari kuwahubiri laini yadanganyayo. Hao ndio waliowapenda, hao ndio waliowatukuza, waliowasifu kwamba wana upako, hao ndio waliowasifia kwamba ndio watumishi wa Mungu. Mhubiri Isaya hakuwa kati yao, alipingana nao. Na sisi wahubiri wa leo tusiwe miongoni mwa walimu wengi wanaochuja neno na kufundisha maneno laini yadanganyayo. Tusifundishe mafundisho ya kuwapendezesha watu bali tufundishe kweli ya neno la Mungu kama ilivyo bila kujali lolote litakalotokea kwa viwango hivyo.

Wakati wa Paulo mtume walikuwepo watu waliohubiri maneno laini yadanganyayo na Paulo mtume alipambana wao. Paulo alisema watu wanaohubiri maneno laini yadanganyayo hawamtumikiii Kristo bali wanatumikia matumbo yao wenyewe.

( WARUMI 16:17-18 )

“Ndugu zangu, nawasihi, wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza, mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao yenyewe; na kwa maneno laini nay a kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.”

Walikuwepo wahubiri nyakatiza Paulo waliopingana na Paulo katika kufundisha neno la Mungu. Wahubiri hao waliwaambia watu kuwa wanaweza kufanya dhambi na wakaingia mbinguni. Kwamba wanaweza kuazini lakini wakaingia mbinguni. Paulo mtume yeye alizidi kusisitiza katika mafundisho akisema “msidanganyike”

( WAEFESO 5:3,5-6 ; 1 WAKORINTHO 6:9-10 )

Watu wapendao uongo na kuufanya hawawezi kuingia mbinguni

( UFUNUO 22:14-15 )

“Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mji wa uzima na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya” Watu wanaoufanya uongo ni wale wanaoigiza maigizo. Mtu anaigiza uchungaji akiwa yeye siyo mchungaji, anawadanganya watu wanaotazama. Namna yoyote ya kuigiza yaisha ya watu wengine kwa mfano watakatifu wa zamani. Tunaweza kuona filamu zinazoitwa za Musa, Paulo,, n.k jambo la kushangaza ni kwamba nyakati zao haikuwepo teknolojia ya video tulionayo leo. Hazikuwepo video camera wakati ule. Neno la Mungu latosha kwa kujifunza na kuamini si mpaka kuona. Yesu alisema wa heri wale watakaosadiki pasipo kuona.. Imani huja kwa kusikia na siyo kwa kuona. Watu wote wanaoangalia filamu zote na maigizo wote wanaupenda uongo. Hata kama wewe ni mchungaji au mtu unayesema umeokoka hauna nafasi katika nji ule wa mbinguni kama unapenda uongo wa ect za maigizo na filamu. Wanaocheza bahati na sibu katika simu n.k wote wanaupenda uongo. Wanatuma sms kwa Tsh 150 n.k kwa kudanganywa eti watashinda Gari la mamilioni lakini mtu mmoja katika nchi nzima ndiye anakuwa mshindi na watu wote wanaliwa . Wachungaji wana wanaoshusha viwango vya neno la Mungu na kuwaambia watu kusuka nywele siyo shida kiroho, kupaka wanja, kujichubua, kuvaa wigi, kuvaa laster, suruali kwa wanawake, mapambo n.k wote hawa wanaufanya uongo. Mbona Pentekeoste ya miaka ya nyuma ilikuwa ikikemea mambo hayo tena msisitizo na hatua kali zikichukuliwa kwa watu waliofanya hivyo. Wote wanaovaa mavazi hayo kinyume na neno la Mungu kwa kuwasikiliza walimu wao wa madhehebu yao au mengine wote wanapenda uongo. Watu wa namna hii hawana nafasi katika uzima wa milele ( UFUNUO 22;14-15 )

Mtu anaweza kuhama kanisa kwa kukimbia viwango vya neno la Mungu na kutafuta kanisa lingine ambalo linaruhusu hicho anachotaka kufanya. Ni kweli makanisa yako mengi lakini kweli ya neno la Mungu ni moja tu. Madhehebu ni mengi lakini kanisa la Yesu ni moja tu nalo ni lile linaloongozwa na kweli yote. Njia ya kutufikisha mbinguni ni moja tu, Yesu Kristo Mwana wa Mungu. Tunaingia mbinguni kwa kutii maagizo yote ya Mungu katika Neno lake ( ZABURI 119:6 ).

Wapo walimu wengi ( wahubiri ) watakaofundisha maneno laini yadanganyayo na kusema Mungu haangalii mambo ya mwili , anaangalia mambo ya roho tu. Watu watafurahia kuwepo kwa wahubiri hao kwa kwa sababu wanawatia moyo kuendelea kuvaa vyovyote na chochote katika mwili. Je, ni kweli kwamba utakatifu ni rohoni tu na siyo katika mwili na roho? Ukweli wa jambo hili unapatikana katika maandiko yenyewe. Biblia inasema utakatifu ni mwili na roho( 1 WAKORINTHO 7:34; 2WAKORINTHO 7:1; 1WATHESALONIKE 5:23; MATHAYO 23:25-26 ).. Wanawatia moyo watu na kuwaambia “msimsikilize Kakobe Mungu haangalii mambo ya mwili anaangalia mambo ya roho”. Huo ni uongo wa mchana kweupe. Je uasherati na uzinzi ni mambo ya roho. Unafikiri roho ndizo zinafanya uasherati? Kama Mungu haangalii mambo ya mwili wahubiri kuwa uasherati siyo shida. Je mtu anapo muua mwenzie kinachokufa ni roho? Kama ni mwili basi hata mauaji siyo shida. Je watu wanapopigana zinapigana roho? Kama ni miili mbona wahubiri hao wanahubiri kuwa kupigana ni dhambi?

Hapa Full Gospel yupo Isaya, hakuna maneno laini. Tunaishi kwa kweli yote kama mtu hataki kuishi sawasawa na Neno lote la Mungu tusimuone jumapili ijayo. Sipo tayari kuhubiri uongo na kuwafariji watu eti wanaweza kwenda mbinguni na kuchubua ngozi, na mawigi yao,na heleni, mikufu, bangili, na uchafu wote wa kila namna.. Hivyo ni vifaa vya makahaba. Hakuna watu wanaocheza rapu, wanaonengua viungo makanisani, wanaocheza karata, wanaocheza drafti, wanaocheza bahati na sibu, n.k watakaoingia mbinguni. Bahati na sibu zote ni kamali. Chochote kilicho kinyonge hakitaingia katika mji ule.

Ikiwa umeamua kuokolewa utakuwa tofauti kabisa na ulimwengu. Watu wengine wanasema, “Kakobe inamaana wewe tu na kanisa lako la Full Gospel ndiyo watakatifu tu?”. Ni kweli watakatifu hawako Full Gospel peke yake tu lakini hata wakiwa popote tutawatambua kwa matunda yao. Kweli ni moja tu aliyoihubiri Paulo mtume.

( WAGALATIA 1:6-9 )

“Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliye waita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena mtu awayeyote akiwahubiri ninyi injili yoyote isipokuwa hiyo mliyopokea, na alaaniwe”.

Yeyote ambaye haihubiri injili ya Paulo mtume tayari amekwisha kulaaniwa sawasawa na andiko hilo hapo juu. Paulo mtume anahubiri injili ya namna gani?

“Wanawake wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri sikwa kusuka nywele wala kwa dhahabu na lulu kama wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu ( 1 TIMOTHEO 2:9-10 )

Mume amefungwa na mkewe mpaka kifo kiwatenganishe. Ikiwa wameachana wakae hakuna kuoa wala kuolewa au wapatane tena na kuishi pamoja ( wasameheane).

( 1 WAKORINTHO 7:10-11,; WARUMI 7:2-3 )

Kwa hiyo imempasa mwanamke ( imempasa yaani ni lazima ) awe na dalili ya kumilikiwa kichwani kwa ajili ya malaika ( 1 WAKORINTHO 11:10 ).

Mwanamke anapaswa kufunika kichwa chake kwa kilemba ( kitambaa ) wakati wote awapo kanisani na wakati wote wa kuomba au katika ibada ya aina yoyote. Tumezoea kuona wanaume wakivua kofia lakini tunashindwa kujua kuwa sheria hiyohiyo ndiyo inamtaka mwanamke kufunika kichwa. Malaika wanataka order ( utaratibu ) ili mamlaka ya Kristo ambaye ni Kichwa cha Kanisa iweze kutenda kazi.

Yeyote ambaye hahubiri injili hii amelaaniwa na watu ambao wanamfuata wamedanganyika, wameuamini uongo. Siku ile ya mwisho kila mtu bila kujali yuko Assemblies of God, Church of God, Full Gospel, Cathoric, Anglican n.k, atahukumiwa kwa injili ya Paulo mtume na siyo kwa injili anayohubiriwa na Pandrii wake, siyo kwa injili inayohubiriwa na Askofu wake anayehubiri uongo.

( WARUMI 2:16 )

“Katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu wote sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu” Watu wote watahukumi kwa injili hiyohiyo ya Paulo mtume inayokataza mapambo, inayowaagiza wanawake kufunika vichwa wawapo kanisani na wakati wote wa ibada. Unapokimbia injli hiyo ya Paulo na kusema na sisi kwetu kuna inahubiriwa injili. Hiyo ni injili ya namna nyingine. Kweli nin injli iliyohubiriwa na Paulo mtume. Tunapaswa kuwa mbali na walimu wengi wa uongo wanaotuzunguka, watu wanaolipindisha Neno la Mungu kwa kusudi ili wawe na washirika wengi na kupata sadaka nyingi. Mungu wao ni tumbo kama Paulo alivyosema ( WARUMI 16:17-18 )

Watu ambao hawataki kweli lakini wanataka kuendelea kuona uwepo wa Mungu kwao ili wajifariji kwamba Mungu anakubaliana na mawigi na kujikoboa ngozi. Mungu atawaachilia pepo wafanye miujiza ili wazidi kupotea hatimaye waweze kuangamizwa. Unafikiri mapepo hayawezi kufanya miujiza ? Kumbuka wakati wa Musa na Haruni, waganga na wachawi wa Haruni waliweza kufanya miujiza..

Siku hizi za mwisho roho ya Asi ( mpinga Kristo ) inafanya kazi na tunaona uasi wa kila namna hata makanisani. Watu hawataki kukaa katika Neno la Mungu. Ni kizazi cha Laudikia. Neno Laudikia katika lugha ya asili maana yake ni “freedom of the right” kwa Kiswahili “Uhuru wa washirika kutakakufanya wanachotakakufanya na wasiambiwe na wasikemewe kwa lolote” Kanisa Laudikia liko hivyo. Makanisa mengi siku hizi za mwisho yamekuwa vuguvugu na yanaelekea kuwa baridi kabisa ( UFUNUO 3:15-16 ). Ukweli ni kwamba na washirika wa akanisa hayo wamepoa kutokana na mafundisho laini yadanganyayo wanayohubiriwa kinyume na Kweli ya Paulo mtume. Msingi wa mmafundisho ya mitume umeachwa na ndiyo maana kazi zilizofanywa na mitume na matokeo yake hatuzioni maishani mwetu. Mitume waliweza kuupindua ulimwengu bila vyombo vya usafirsi kama vile ndege, magari, pikipiki, baiskeli n.k.( MATENDO 17:6 )

Paulo mtume alitabiri juu ya nyakati hizi tulizonazo. Alisema kuwa watu wengi hawatapenda kweli, watapenda kudanganywa hivyo watajitafutia walimu makundimakundi kwa sababu wana masikio ya utafiti. ( 2TIMOTHEO 4:3-4 )

Mpendwa msomaji, baada ya kusikia yote haya kutoka kwa nabii aliyetumwa kukuletea ujumbe huu, usifanye moyo wako kuwa mgumu. Hii ni nafasi ya kipekee ya kuokoka. Je, unajuaje kama utaamka kitandani baada ya kulala usiku wa leo? Wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (2 WAKORINTHO 6:2). Labda utaniuliza, ili uokoke, ufanyeje? Jibu ni rahisi, kwa imani ukitubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, na kumwambia Yesu Kristo akusamehe, utasamehewa sasa hivi, na msamaha wa dhambi, huambatana na wokovu (LUKA 1:77). Je, uko tayari kuokoka sasa hivi? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati toka moyoni,“Mungu baba asante kwa kuniletea ujumbe huu.Natubu dhambi zangu zote, kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo nakuomba unisamehe dhambi zangu na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa kutoka katika mateso ya moto wa milele. Asante, kwa kuniokoa katika Jina la Yesu. Amen”. Tayari sasa umeokoka, na kwa hakika unakwenda mbinguni sasa, hata ukifa leo. Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .


Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe
Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni