Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe Tovuti : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SOMO LA MAKANISA YA NYUMBANI
SOMO LA 111 : YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA?
NENO LA MSINGI:
MATENDO YA MITUME 16:30, 32
“Kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA? Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake”.
<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><
W
atu waliookoka katika Kanisa la Kwanza lililokuwa linaongozwa na Mitume, walijua sana jinsi ya kumweleza mtu maana ya wokovu hata yeye naye akaokolewa. Katika Neno hili la msingi, tunaona mtu mmoja akiuliza afanye nini apate kuokoka, na hapohapo anaambiwa neno la Bwana na kuelewa analopaswa kulifanya. Watu wote tuliookoka, ni wajibu wetu kuwaambia watu wote neno la Bwana linalohusu wokovu ili yamkini wote wapate kuokolewa. Jambo la huzuni ni kwamba watu wengi waliookoka, hawawezi kumweleza mtu mwingine neno la BWANA hata akaelewa, na yeye akaokolewa. Kanisa la Mungu halipaswi kuwa hivi na kuwaacha wengi wakiangamia! Basi, ni makusudi ya somo la leo la Kanisa la Nyumbani, kujifunza hatua kwa hatua yanayotupasa kufahamu katika kumwambia mtu neno la BWANA hata na yeye aokolewe. Ikiwa wewe uliyehudhuria leo katika Kanisa la Nyumbani hujaokolewa basi unapokuwa unajifunza somo hili hujaokolewa basi ni siku yako pia kuokolewa baada ya kufahamu yote yanayokupasa kufahamu na kuyafanya.
A: NINI MAANA YA NENO “KUOKOKA” AU “KUOKOLEWA?“
Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kukupata. Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri. Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika hapo inasemekana umeokoka.
ANGALIA MIFANO KATIKA BIBLIA:
Baada ya Yusufu kuuzwa na ndugu zake na kupelekwa kuwa mtumwa huko Misri,
ilitokea njaa kubwa sana katika ulimwengu wote wa wakati huo. Watu wengi mno walikufa kwa kukosa chakula, na kulikuwa hakuna matumaini. Ndugu zake Yusufu nao walikuwa katika hatari ya kifo. Kabla ya njaa, huko Misri Yusufu kwa uwezo wa ajabu wa Mungu, aliaminiwa na kuwa Waziri Mkuu wa nchi ya Misri na akatumiwa na Mungu kuhifadhi chakula kingi ambacho hatimaye, kilitumika kuwaokoa ndugu zake katika maafa ya kufa kwa njaa.
MWANZO 45: 5 – 7:
“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi,NA KUWAOKOA NINYI KWA WOKOVU MKUU“.
Daudi akiwa katika hali ya hatari anaelezea juu ya hali ya mtu anayehitajika kuokolewa mtu ambaye yuko katika hatari ya kufa baada ya kuzama katika matope mengi na maji yakiwa yamefika nafsini mwake.
ZABURI 69:1 – 2:
“Ee Mungu, UNIOKOE, maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi, pasipowezekana kusimama. Nimefika penye maji ya vilindi, mkondo wa maji unanigharikisha.”
Wakati wa Nuhu, Mungu akiwa amechukizwa na dhambi za watu wa wakati ule, aliwaonya watu juu ya maafa yatakayokuja, kuwaangamiza wote wasiomtii Mungu. Watu wote wakapuuza ujumbe huo, isipokuwa Nuhu aliyetii na kuunda Safina iliyotumika kumwokoa yeye na watu wa nyumba yake kutoka katika maafa ya kufa kwa gharika kuu. Watu wote walikufa kutokana na gharika hiyo isipokuwa Nuhu na wenzake saba waliookolewa katika maafa hayo.
WAEBRANIA 11:7:
“Kwa Imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu aliunda safina, APATE KUOKOA NYUMBA YAKE”.
B: MAISHA YA BAADAYE YA MTU MWENYE DHAMBI:
Mtu yeyote mwenye dhambi lazima atapata adhabu ya milele. Adhabu yake inaitwa MAUTI YA PILI auMAUTI YA MILELE ambayo ni kutupwa motoni na kuteswa milele. Hakuna mwenye dhambi atakayekwepa adhabu. Kila mmoja atapata mshahara huu wa dhambi, mauti ya milele au kutupwa Jehanum ya moto.
MITHALI 11:19 – 21:
“——- Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe—— Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu——-”.
EZEKIELI 18:4, 20:
“—-Roho itendayo dhambi itakufa————-”.
WARUMI 6:25:
“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti.”
UFUNUO 21:8:
“Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao, ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo MAUTI YA PILI.”
Hakuna mtu yeyote mwenye dhambi yaani asiyekuwa na haki mbele za Mungu atakayeokoka katika maangamizo hayo. Kwa sasa mtu mwenye dhambi anaona kwamba yuko salama na kwamba amani iko kwake, lakini ghafla uharibifu wake utamwijia.
1 WATHESALONIKE 5:3:
“Wakati wasemapo, kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile uchungu umjiavyo mwenye mimba wala hakika hawataokolewa.”
ZABURI 119:155:
“Wokovu u mbali na wasio haki kwa maana hawajifunzi amri zako (na kuzitenda)”.
C. NI NANI MWENYE DHAMBI?
Jibu ni kwamba kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, kutokana na asili ya Adamu, yuko miongoni mwa wenye dhambi. Wote wamefanya dhambi. Kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni; na WATU WOTE wakahesabiwa kuwa wenye dhambi. Kutokana na kila mtu kuzaliwa akiwa na asili ya dhambi, kila mtu anatenda dhambi pia. Hivyo watu wote pamoja, na wewe, wanazaliwa katika dhambi na pia wote wanatenda dhambi.
MHUBIRI 7:20:
“Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.”
ZABURI 53:3:
“Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, hakuna atendaye mema, La! hata mmoja.”
ISAYA 53:6:
“Sisi sote kama kondoo tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe———”.
WARUMI 3:23:
“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”
WARUMI 5:12:
“Kwa hiyo kama kwa mtu mmoja (Adamu) dhambi iliingia ulimwenguni na kwa dhambi hiyo mauti na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi”.
1 YOHANA 1:8, 10:
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”
Unaona basi! Kila mtu anakuwa mwenye dhambi kutokana na uzao wa Adamu. Kila mtu anazaliwa akiwa ana asili ya dhambi. Kama Adamu alivyofanya dhambi, wote tunazaliwa na dhambi ya asili.



















































